Heynckes: Corona imefichua mabaya katika soka na jamii
3 Mei 2020Heynckes ameliambia gazeti la Welt am Sonntag kwamba ubinafsi na uchoyo umeshuhudiwa ukiwa juu ya maadili kama umoja, ubinadamu na mshikamano.
"Tunatakiwa tufikirie na tubadili hisia zetu tena kwa watu ambao wanakabiliwa na hali ngumu," alisema Heynecknes.
Akiangazia kandanda, alijiunga na wale wanaotaka kuweko na ukarimu zaidi akisema: "Ni muhimu kutafuta njia ya kurejea katika hali ya kawaida zaidi. Gharama za uhamisho na mishahara lazima zipunguzwe tena. Hali ilikuwa ovu kinyume na maadili isiyokubalika wakati mwingine."
Heyneckes, mwenye umri wa miaka 74, ni mshambuliaji wa zamani wa timu ya taifa ya kandanda ya Ujerumani. Kama kocha alishinda kombe la mabingwa Ulaya, Champions, akiwa na Real Madrid ya Uhispania na Bayern Munich. Alikuwa kocha kwa misimu mitatu mjini Munich huku ufanisi mkubwa akiupata mwaka 2013 aliposhinda taji la Bundesliga, kombe la shirikisho DFB Pokal na kombe la mabingwa wa Ulaya.
Ligi ya Bundesliga ilisimamishwa katikati ya mwezi Machi kwa sababu ya janga la corona lakini vilabu vina matumaini ligi hiyo itaanza tena mwezi huu, pakisubiriwa idhini kutoka kwa serikali kuu mjini Berlin.
Hasara kubwa iliyopatikana na timu na utegemezi mkubwa wa mapato kutokana na matangazo ya televisheni yameibua mjadala kuhusu maadili katika soka la Ujerumani.
(dpa)