1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hezbollah yaishutumu Israel kwa mashambulizi Lebanon

Angela Mdungu Wahariri: Mohammed Khelef, Sylvia Mwehozi
18 Septemba 2024

Mamia ya vifaa vya mawasiliano vilivyokuwa vikitumiwa na wanachama wa kundi la wanamgambo wa Hezbollah na raia wa kawaida vilripuka Jumanne katika maeneo mbalimbali kote nchini Lebanon.

Mlipuko wa vifaa vya mawasiliano Lebanon
Taharuki miongoni mwa watu karibu na magari ya kubeba wagonjwa katika eneo la hospitali mjini Beirut baada ya mlipuko wa vifaaa vya mawasiliano vya wanamgambo wa Hezbollah 17.09.2024Picha: Anwar Amro/AFP/Getty Images

Shambulio hilo limesababisha vifo vya watu wasiopungua tisa akiwemo mtoto mmoja. Watu wasiopungua 2,800 wamejeruhiwa katika shambulio hilo na wengine 200 wako katika hali mbaya.

Kundi la wanamgambo wa Hezbollah limeapa kulipa kisasi dhidi ya shambulio hilo la Jumanne liililotokea baada ya vifaa vya mawasiliano kuripuka likisisitiza kuwa Israel imehusika, na kwamba litaiadhibu. Mapema hapo jana, vifaa hivyo ambavyo afisa mmoja wa Hezbollah alivitaja kuwa ni vipya vilianza kupata moto na kisha kuripuka.

Soma zaidi: Lebanon: Watu 9 wauawa, maelfu wajeruhiwa katika mlipuko wa vifaa vya mawasiliano

Kwa upande wake, jeshi la Israel halijazungumza lolote kuhusu shambulio hilo. Hata hivyo, awali Israel ilitangaza kuwa inataka kutanua vita vyake kwenye Ukanda wa Gaza hadi Lebanon. Kiongozi wa Hezbollah, Hassan Nasrallah awali aliwatahadharisha wanachama wa kundi hilo kutotumia simu za viganjani akisema kuwa zinaweza kutumiwa na Israel kufuatilia nyendo zao.

Balozi wa Iran nchini Lebanon amejeruhiwa

Kulingana na shirika la habari la Iran, IRNA, balozi wa nchi hiyo huko Lebanon, Mojtaba Amani, alijeruhiwa na moja ya kifaa kilichoripuka na alikuwa akipatiwa matibabu.

Moja ya kifaa cha mawasiliano kilicholipuka LebanonPicha: Balkis Press/ABACA/IMAGO

Iran yenyewe imeishutumu Israel kwa shambulio hilo la Jumanne na imeliita kuwa ni mauaji ya halaiki. Waziri wa mambo ya kigeni Nasser Kanan, katika taarifa yake amelaani kitendo hicho alichokitaja kuwa cha kigaidi. Urusi, kupitia wizara yake ya mambo ya kigeni, nayo pia imelaani shambulio hilo iliyoliita baya kabisa.

Kwingineko, Waziri wa mambo ya Kigeni wa Marekani Anthoniy Blinken yuko mjini Cairo ili kuokoa juhudi za kupata makubaliano ya kusitisha vita katika Ukanda wa Gaza. Makubaliano hayo yanazidi kukabiliwa na ugumu hasa baada ya shambulio la vifaa vya mawasiliano lililowalenga wanamgambo wa Hezbollah

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW