1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hezbollah yaendelea kukabiliana na Israel

5 Agosti 2024

Watu wawili wameuawa huko Lebanon kufuatia mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Israel baada ya kundi la Hezbollah kuyashambulia kwa droni maeneo ya kaskazini mwa Israel.

Shambulizi la Hezbollah katika eneo linalokaliwa na Israel la milima ya Golan
Kikosi cha zimamoto kikijaribu kuzima moto kufuatia shambulizi la Hezbollah katika eneo linalokaliwa na Israel la milima ya Golan: 04.07.2024Picha: Gil Eliyahu/AP Photo/picture alliance

Kundi la wanamgambo wa Lebanon la Hezbollah limesema mashambulizi yake ya droni mapema leo yaliyoilenga kambi ya jeshi, ni majibu kutokana na mauaji ya Israel yaliyofanywa hivi karibuni nchini humo. Israel imesema mashambulizi hayo yaliwajeruhi askari wawili na kusababisha uharibifu kadhaa.

Israel imejibu mashambulizi na kulenga ngome za Hezbollah kusini mwa Lebanon na kuwaua watu wawili katika kijiji cha Hula. Ghasia hizo zinaongeza hofu ya kutokea kwa vita vya kikanda na kuliathiri eneo lote la Mashariki ya Kati ambalo tayari limenakumbwa na migogoro kadhaa.

Soma pia: Biden aahidi kuilinda Israel na vitisho vyote kutoka Iran

Mzozo kati ya Israel na makundi ya wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran unatishia kutanuka zaidi baada ya mauaji ya wiki iliyopita mjini Beirut ya kamanda mkuu wa Hezbollah Fouad Shukur na mauaji ya kiongozi mkuu wa kisiasa wa Hamas Ismail Hanniyeh mjini Tehran.

Raia wa kigeni waombwa kuondoka Lebanon

Wasafiri wakiangalia ratiba ya safari za ndege katika uwanja wa ndege wa BeirutPicha: Houssam Shbaro/Anadolu/picture alliance

Miito imekuwa ikiongezeka ya kuwataka raia wa kigeni kuondoka mara moja nchini Lebanon, hasa wakati huu Iran na washirika wake wakijiandaa kulipiza kisasi kwa mauaji ya viongozi hao wa Hezbollah na Hamas.

Ufaransa na Saudi Arabia ni mataifa yalitoa miito hiyo hivi karibuni kwa raia wake. Mashirika ya ndege ya Magharibi yamesitisha safari zake kuelekea Lebanon na maeneo mengine ya  Mashariki ya Kati . Raia wa kigeni wameanza kujiandaa kuondoka kama anavyoeleza Sherin Malah:

"Ninasafiri sana, nina pasi ya kusafiria ya Italia na nimekuwa nikiishi Italia kwa miaka 30. Nilikuja hapa kumuona mama yangu. Tulikuwa tumekata tiketi za ndege, lakini safari zilifutwa. Tulikuwa na hofu na tukasisitiza kupata tiketi nyingine. Lakini nilishangaa kuona kuna watu wengi wanaoondoka na nikasikia kwamba huko kusini walifungua njia ya kusafiri kwenda Paris. Eeh Mungu, hali inasikitisha. Tunatoka kwenye mzozo mmoja, tunaingia kwenye mwingine."

Juhudi za kidiplomasia kuepusha vita vya kikanda

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron (kulia) akiwa na Mfalme Abdullah II wa JordanPicha: Yoan Valat/AP/picture alliance

Wanadiplomasia wa mataifa mbalimbali wanaendeleza pia juhudi za kuepusha vita hivyo vya kikanda. Hapo jana, rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alizungumza kwa njia ya simu na Mfalme Abdullah II wa Jordan na kwa pamoja wakaonya kwamba ni lazima kuepusha vita vya kikanda "kwa gharama yoyote".

Soma pia: Marekani kupeleka meli na ndege za kivita Mashariki ya kati

Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin amezungumza na mwenzake wa Israel Yoav Gallant na kumuhakikishia uungwaji mkono usioyumba na kwamba Washington iko tayari kuilinda Israel na vitisho vyote kutoka Iran. Wawili hao walizungumzia pia mikakati ya kuboiresha mifumo ya ulinzi na kuzuia hali ya mivutano.

Austin alitaja pia kuunga mkono mchakato wa makubaliano ya usitishwaji mapigano huko Gaza na kuachiliwa kwa mateka. Marekani ilitangaza kuwa itatuma meli na ndege za kivita huko Mashariki ya Kati ili kuimarisha uwezo wake kijeshi katika eneo hilo.

(Vyanzo: AFP, DPA, AP, Reuters)

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW