1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hezbollah yathibitisha kifo cha kiongozi wake, Nasrallah

28 Septemba 2024

Kundi la wanamgambo la Hezbollah la nchini Lebanon, limethibitisha kuwa kiongozi wake na mmoja wa waanzilishi wake, Hassan Nasrallah ameuawa katika shambulizi la anga la Israel siku ya Ijumaa.

Kiongozi wa Hezbollah Hassan Nasrallah, aliyeuawa na Israel
Kiongozi wa Hezbollah Hassan Nasrallah, aliyeuawa na IsraelPicha: Morteza Nikoubazl/picture alliance/NurPhoto

"Sayyed Hassan Nasrallah, Katibu Mkuu wa Hezbollah, ameungana na mashahidi wenzake na wafiadini ambao aliwaongoza kwa takribani miaka 30," ilieleza taarifa iliyotolewa na kundi hilo linaloungwa mkono na Iran.

Taarifa hiyo ya Hezbollah imeapa kuendeleza "vita vyake vitakatifu" dhidi ya adui yake Israel, na katika kuiunga mkono Palestina.

Mapema jeshi la Israel lilisema Hassan Nasrallah aliuawa katika shambulizi ''sahihi'' la anga wakati wa mkutano wa viongozi wa kundi hilo kwenye makao yake makuu huko Dahiyeh, kusini mwa Beirut.

Israel yatangaza kumuua Nasrallah

''Hassan Nasrallah ameuawa,'' alitangaza msemaji wa jeshi la Israel, Luteni Kanali Nadav Shoshani, katika ukurasa wa mtandao wa X.

Duru karibu na kundi la Hezbollah limeliambia shirika la habari la Ufaransa, AFP kuwa mawasiliano na Nasrallah yalipotea tangu siku ya Ijumaa, wakati shambulizi lilipofanyika.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa imesema kulingana na taarifa walizo nazo ambazo zimethibitishwa, ni kweli Hassan Nasrallah ameuawa.

Mkuu wa majeshi ya Israel, Luteni Jenerali Herzi HaleviPicha: Israeli Defense Forces/IDF/dpa/picture alliance

Aidha, Luteni Kanali Shoshani amesema bado wana kazi kubwa ya kufanya, na mapigano dhidi ya kundi la Hezbollah yanaendelea, hata baada ya kutangaza kumuuwa Nasrallah. ''Hezbollah bado wana roketi na makombora, na kundi hilo lina uwezo wa kuyarusha makombora mengi kwa wakati mmoja,'' alifafanua msemaji huyo wa jeshi la Israel.

Akizungumza Jumamosi na waandishi habari kwa njia ya mtandao, Luteni Kanali Shoshani amesema kundi hilo linaloungwa mkono na Iran, linaaminika kuwa na maelfu ya roketi. Kulingana na Luteni Kanali Shoshani, viongozi wengi wa ngazi ya juu wa Hezbollah pia wameuawa.

Israel yashambulia maeneo 140 ya Hezbollah

Jeshi la Israel IDF pia limesema limeyashambulia zaidi ya maeneo 140 ya Hezbollah tangu usiku wa Ijumaa. ''Tangu Ijumaa usiku, IDF ilishambulia ngome za kigaidi 140 za Hezbollah, ikiwemo mizinga inayotumika kuwalenga raia wa Israel, majengo ambayo silaha zinahifadhiwa, silaha za kimkakati, viwanda vya kutengeneza silaha, na maeneo ya ziada ya miundombinu ya kigaidi,'' taarifa ya jeshi ilieleza.

Soma zaidi: Jeshi la Israel lashambulia miundombinu ya Hezbollah

Naye mkuu wa majeshi ya Israel, Luteni Jenerali Herzi Halevi amesema Israel itaendeleza mashambulizi yake dhidi ya wanamgambo hao wa Hezbollah wanaoungwa mkono na Iran, hata baada ya mauaji ya Nasrallah. ''Kuuawa kwa Nasrallah sio mwisho wa mashambulizi yetu,'' alifafanua Luteni Jenerali Halevi.

Ama kwa upande mwingine, kundi la Hezbollah limesema linahusika na mashambulizi kadhaa ya makombora dhidi ya Israel. Kwa mujibu wa Hezbollah, kundi la wanajeshi wa Israel walishambuliwa kwa mizinga kaskazini mwa Israel.

Roketi kutoka Lebanon lilirushwa kuelekea katika kijiji cha Rosh Pina, Israel Picha: Gil Eliyahu/AFP/Getty Images

Hezbollah imesema roketi lilirushwa kuelekea Kibbutz Sa'ar, na kwamba makombora zaidi yalirushwa katika kijiji cha Rosh Pina, ikiwa ni katika kulipiza kisasi ''mashambulizi ya kikatili ya Israel'' nchini Lebanon.

Kiongozi Mkuu wa kidini na mwenye mamlaka makubwa zaidi nchini Iran, Ayatollah Ali Khamenei amelaani vikali kile alichokitaja kuwa sera ya ''kipumbavu na kijinga'' ya utawala dhalimu wa Israel baada ya mashambulizi yake nchini Lebanon.

Khamenei amesema mauaji ya watu wasio na ulinzi nchini Lebanon kwa mara nyingine tena yanafichua ukatili wa Israel.

Khamenei awataka Waislamu kusimama pamoja

Aidha, Khamenei amewataka Waislamu kusimama pamoja na watu wa Lebanon na Hezbollah kwa njia zozote zile walizonazo na kuwasaidia katika kukabiliana na utawala mbovu wa Israel.

''Hatma ya ukanda huu itaamuliwa na vikosi vya upinzani, huku Hezbollah ikiwa mstari wa mbele,'' alisisitiza Khamenei katika taarifa yake aliyoitoa Jumamosi baada ya Israel kusema imemuuawa kiongozi wa Hezbollah, Hassan Nasrallah.

Kiongozi mkuu wa kidini wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei Picha: picture alliance/ZUMA Press Wire

Wakati huo huo, Umoja wa Ulaya umeyashauri mashirika ya ndege kuepuka kutumia anga ya Lebanon na Israel kwa mwezi ujao, huku kukiwa na ongezeko la mashambulizi ya anga kati ya Israel na Hezbollah.

Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya na Shirika la Usalama wa Anga la Umoja wa Ulaya, EASA, walionya katika taarifa waliyoitoa Jumamosi kuhusu kuongezeka kwa jumla mashambulizi ya anga na kuzorota kwa hali ya usalama.

EASA imesema itaendelea kufuatilia kwa karibu hali katika eneo hilo, kwa nia ya kutathmini kama kuna ongezeko au kupungua kwa hatari kwa mashirika ya ndege ya Umoja wa Ulaya, kutokana na kitisho kinachoendelea.

(AFP, AP, DPA, Reuters)