Hezbollah, Israel zashambuliana kwa makombora, madege
25 Agosti 2024Hezbollah ilirusha mamia ya roketi na droni nchini Israel mapema Jumapili, wakati jeshi la Israel likisema liliipiga Lebanon kwa takriban ndege 100 kuzuia shambulio kubwa zaidi, katika moja ya makabiliano makubwa zaidi ya miezi zaidi ya 10 ya vita vya mpakani.
Makombora yalionekana yakizunguka angani alfajiri, yakiacha nyuma michirizi ya mvuke mweusi, huku king'ora cha anga kikilia nchini Israeli na mlipuko wa mbali ukitanda kwenye upeo, huku moshi ukitanda juu ya nyumba mjini Khiam, kusini mwa Lebanon.
Ukubwa wa hasara haukuwa wazi mara moja na Hezbollah imeashiria kuwa ilikuwa inapanga mashambulizi zaidi, huku waziri wa mambo ya nje wa Israel akisema nchi hiyo haitaki vita kamili.
Kuongezeka kwa aina yoyote kubwa katika mapigano, ambayo yalianza sambamba na vita vya Gaza, kuna hatari ya kubadilika na kuwa mzozo wa kikanda wa waungaji mkono wa Hezbollah, Iran, na mshirika mkuu wa Israel Marekani.
Mashambulizi ya Jumapili yalikuja wakati wapatanishi walikuwa wanakutana mjini Cairo katika juhudi la dakika za mwisho kusitisha mapigano Gaza.
Israel yashambulia maeneo 40 ya urushaji makombora Lebanon
Hezbollah ilisema ilifyatua maroketi 320 chapa ya Katyusa kuelekea Israel na kupiga shabaha 11 za kijeshi katika kile ilichokiita awamu ya kwanza ya kisasi dhidi ya Israel kwa mauaji ya Fuad Shukur, kamanda wa juu wa Hezbollah, mwezi Julai.
Jeshi la Israel lilisema lilizuwia shambulio kubwa zaidi kwa mashambulizi ya kuzuwia, baada ya kutathmini kwamba Hezbollah ilikuwa inajiandaa kufanya mashambulizi makubwa, kwa kutumia ndege 100 kushambulia zaidi ya vituo 40 vya ufyatuaji vya Hezbollah kusini mwa Lebanon.
Mashambulizi hayo yaliharibu mamia ya mifumo ya maroketi yalioelekezwa hasa kaskazini mwa Israel lakini pia yalilenga shabaha katika baadhi ya maeneo ya katikati mwa Israel, lilisema jeshi la Israel.
Soma pia: Mataifa ya Magharibi yaitaka Iran kuacha vitisho vya kuishambulia Israel
Hezbollah ilitupilia mbali taarifa ya Israel kwamba mashambulizi ya kundi hilo yamezimwa na mashambulizi ya kuzuwia, ikisema kuwa imeweza kurusha droni zake kama ilivyopangwa na kwamba majibu yake mengine kwa mauaji ya Shukr yatachukua "muda".
Baraza la mawaziri la Israel lilikutana majira ya moja asubuhi. Waziri wa ulinzi Yoav Gallant alitangaza hali ya dharura na waziri wa mambo ya nje Israel Katz alisema Israel itajibu matukio yanayondelea lakini hakutaka vita kamili.
Safari za ndege zasitishwa kwa muda
Safari za ndege kwenda na kutoka uwanja wa Ben Gurion mjini Tel Aviv zilisitishwa kwa karibu dakika 90.
"Tumedhamiri kufanya kila kitu kinachowezekana kulinda nchi yetu, kuwarejesha salaama wakazi upande wa kaskazini majumbani mwao na kuendelea kushikilia kanuni rahisi: Yeyote anaetudhuru - tunamdhuru," alisema waziri mkuu Benjamin Netanyahu katika taarifa.
Waziri Mkuu wa muda wa Lebanon Najib Mikati alikutana na mawaziri katika kikao cha kamati ya taifa ya dharurua. Kiongozi wa Hezbollah alitarajiwa kuzungumza kupitia televisheni baadae Jumapili, lilisema kundi hilo.
Soma pia: Israel yaendelea kukabiliana na Hezbollah
Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini Lebanion, na ofisi ya mratibu maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini humo zimezoa wito kwa pande zote kusitisha mapigano, zikiyataka matukio ya usiku kuwa "ya kutia wasiwasi."
Matarajio ya kuongezeka kwa mzozo huo yalizuka tangu shambulio la kombora katika eneo linalokaliwa kimabavu na Israel la Milima ya Golan mwezi uliopita, kuuwa vijana 12, na mauaji ya jeshi la Israel dhidi ya Shukr mjini Beirut kujibu shambulio hilo.
Hatari ya mzozo wa kikanda
Ikulu ya Marekani, White House, ilisema Rais Joe Biden alikuwa anafuatilia matukio hayo kwa karibu.
"Kwa maelekezo yake, maafisa wakuu wa Marekani wamekuwa wakiwasiliana mara kwa mara na wenzao wa Israel. Tutaendelea kuunga mkono haki ya Israel kujilinda, na tutaendelea kufanyia kazi utulivu wa kikanda," alisema msemaji wa Baraza la Usalama la Taifa Sean Savett.
Soma pia: Iran yapuuza wito wa mataifa ya Magharibi kutoishambulia Israel
Hezbollah ilirusha makombora dhidi ya Israel mara tu baada mashambulizi ya Oktoba 7 yaliofanywa na wapiganaji wa Hamas dhidi ya Israel. Hezbollah na Israel zimekuwa zikishambuliana mara kwa mara tangu wakati huo, huku zikiepusha ongezeko kubwa wakati vita vikiendelea Gaza.
Mizani hiyo ya hatari ilionekana kubadilika baada ya mashambulizi kwenye Milima ya Golan, ambayo Hezbollah ilikanusha kuhusika nayo, na mauaji yaliyofuatia ya Shukr, mmoja wa makamanda wakuu wa kijeshi wa Hezbollah.
Kifo cha Shukr katika shambulio la anga kilifuatiwa haraka na mauaji ya kiongozi wa kisiasa wa Hamas Ismail Haniyeh mjini Tehran, ambayo yalisababisha viapo kutoka Iran, vya kulipiza kisasi dhidi ya Israel.