1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hichilema akaribia ushindi, upinzani walalamika

17 Agosti 2026

Rais Hakainde Hichilema anaelekea kushinda muhula wa pili Zambia, huku upinzani ukidai dosari katika matokeo na kukataa tuhuma za kuhusika katika shughuli za wanamgambo.

Zimbabwe Harare 2025 | Rais wa Zambia Hakainde Hichilema katika mkutano wa Tume ya Pamoja ya Nchi Mbili
Hakainde Hichilema anaelekea kushinda muhula wa pili baada ya kupata karibu asilimia 61 ya kura katika majimbo 192 kati ya 226.Picha: Matrix Images/picture alliance

Rais wa Zambia Hakainde Hichilema amekaribia kushinda muhula wa pili, baada ya kuongeza uongozi wake katika matokeo ya uchaguzi wa Agosti 13.

Hichilema mwenye umri wa miaka 64 amepata karibu asilimia 61 ya kura, baada ya matokeo kutoka majimbo 192 kati ya 226 kutangazwa hadi Jumatatu jioni.

Mpinzani wake mkuu, Brian Mundubile, amepata karibu asilimia 37. Majimbo 34 pekee ndiyo yalikuwa bado hayajatangaza matokeo.

Mgombea anahitaji zaidi ya asilimia 50 ya kura halali ili kushinda moja kwa moja. Mwelekeo wa sasa unamweka Hichilema katika nafasi ya kupata muhula wake wa mwisho wa miaka mitano bila duru ya pili.

Uchaguzi huo umeonekana kama tathmini ya miaka mitano ya kwanza ya Hichilema madarakani, hasa namna alivyousimamia uchumi wakati uzalishaji wa shaba ukiongezeka.

Mundubile adai matokeo yamebadilishwa

Mundubile, mwenye umri wa miaka 55 na aliyekuwa waziri serikalini, amedai kuwa baadhi ya nyaraka za matokeo zilibadilishwa na hivyo kuhatarisha uadilifu wa zoezi la kuhesabu kura.

Katika ujumbe wa video, amesema pia kuna madai kwamba maafisa katika Mkoa wa Kusini walishinikizwa kubadili takwimu. Hata hivyo, hakutoa ushahidi wa kuthibitisha madai hayo.

Mundubile aliingia katika kinyang’anyiro cha urais mwezi Mei, lakini aliweza kuvuta umati mkubwa katika mikutano yake ya kampeni.

Chama chake cha NRPUP pia kimekanusha madai ya serikali kwamba baadhi ya viongozi na wanachama wake walihusika katika shughuli za wanamgambo au mipango ya uasi.

Serikali imesema polisi waliwakamata watu 11, wakiwemo viongozi sita wa upinzani, katika operesheni dhidi ya watu waliodaiwa kuwa tishio kwa usalama wa taifa.

Kwa mujibu wa serikali, waliokamatwa walikutwa na silaha za kijeshi, risasi na vifaa vilivyokusudiwa kutumiwa katika uasi wenye silaha.

NRPUP imesema operesheni hiyo ilifanyika nyumbani kwa Mundubile, ambako risasi zilifyatuliwa na mbunge mmoja akapigwa. Chama hicho kimezitaja tuhuma za serikali kuwa za uongo.

Mgombea wa upinzani Brian Mundubile anadai matokeo ya uchaguzi yamebadilishwa, baada ya hapo awali kujitangazia ushindiPicha: Gianluigi Guercia/AFP

Kusitishwa kwa hesabu kwakosolewa

Tume ya Uchaguzi ilisimamisha kuhesabu na kutangaza matokeo kwa takriban saa sita Ijumaa, ikitaja mashambulizi dhidi ya maafisa na madai ya kuibwa kwa karatasi za kura.

Zoezi hilo lilirejelewa baada ya tume kusema tishio la usalama lilikuwa limedhibitiwa. Hata hivyo, haijaeleza ikiwa karatasi za kura zilizodaiwa kuibwa zilipatikana.

Waangalizi wa kimataifa, akiwemo Umoja wa Ulaya, wamesema kusitishwa kwa hesabu kulihatarisha uaminifu wa mchakato na imani ya wapiga kura.

Pia wameonya kuwa vizuizi vilivyowekwa dhidi ya upinzani wakati wa kampeni vinaweza kuwa vilisababisha mazingira yasiyo sawa ya ushindani.

Taasisi ya Oxford Economics Africa imesema ukamataji wa viongozi wa upinzani na matukio mengine yaliyouzunguka uchaguzi yameibua maswali mazito kuhusu uadilifu wa matokeo. Taasisi hiyo imeonya kuwa hali nchini Zambia ni ya wasiwasi.

Waangalizi wa uchaguzi wamekosoa hatua ya tume kusitisha zoezi la kuhesabu kwa takribani masaa sita.Picha: Moses Mwape/REUTERS

Uchumi katika mizani

Hichilema anataja kupanga upya madeni na kupunguza mfumuko wa bei kuwa miongoni mwa mafanikio ya serikali yake. Wakosoaji wake wanasema ukuaji wa uchumi bado haujaboresha maisha ya wananchi wengi.

Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, zaidi ya asilimia 70 ya watu milioni 22 nchini Zambia wanaishi kwa chini ya dola tatu kwa siku.

Mundubile aliahidi kuhakikisha mapato yanayotokana na ongezeko la uzalishaji wa shaba yanawanufaisha zaidi wananchi.

Zambiani nchi ya pili kwa uzalishaji wa shaba barani Afrika baada ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Pia ina historia ya kukabidhiana madaraka kwa njia ya amani, huku kila mabadiliko ya urais tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1991 yakifanyika kupitia uchaguzi.

Wakati wetu ni sasa - Vijana wa Zambia wajitosa kwenye siasa

02:41

This browser does not support the video element.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW