1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUswidi

Hifadhi kubwa ya vyuma nadra yagunduliwa Sweden

13 Januari 2023

Hifadhi kubwa ya vyuma nadra vyenye thamani vinavyohitajika kwa matumizi ya bidhaa tofauti ikiwemo magari ya umeme na vifaa vya kuzalisha umeme kupitia upepo, vimegunduliwa kaskazini mwa Sweden.

Critical Raw Materials | Tantalit
Picha: John Cancalosi/Nature Picture Library/imago images

Kampuni ya uchimbaji madini ya Sweden, LKAB, imetangaza hapo Alhamis kwamba zaidi ya tani milioni moja za vyuma hivyo nadra vimepatikana karibu na eneo la Kiruna, jambo linaloifanya hifadhi hiyo kuwa kubwa zaidi kuwahi kugunduliwa barani Ulaya.

Kulingana na mkuu wa kampuni hiyo ya LKAB Jan Moström, hifadhi hiyo inaweza kupiga jeki pakubwa uzalishaji wa mali ghafi muhimu zinazohitajika kwa ajili ya kuingia katika matumizi ya nishati endelevu.

Moström anasema ni vigumu kukadiria ukubwa wa hifadhi hiyo ikilinganishwa na hifadhi zengine nje ya Ulaya.

Mkurugenzi wa kampuni ya LKAB Jan Moström(kushoto) na waziri wa nishati wa Sweden Ebba Busch (kulia)Picha: Jonas Ekstromer/TT News Agency/REUTERS

Kampuni ya Ujerumani kutengeneza mamilioni ya magari yanayotumia umeme

Kampuni hiyo ya Sweden ndiyo inayoendesha mgodi mkubwa zaidi wa chuma huko Kiruna. Na sasa kugunduliwa kwa hifadhi hiyo kunamaanisha kwamba baadhi ya raia wanaoishi huko Kiruna watalazimika kuhamishwa, Inadaiwa kwamba thuluthi moja ya wakaazi elfu sita wa Kiruna wataondolewa na kupelekwa sehemu nyengine.

Mwakilishi wa kampuni ya utengenezaji magari ya Ujerumani ya Schaeffler huko nchini Sweden, Florian Schupp ambaye pia ni meneja wa ununuzi, amesema kampuni yake ina mpango wa kutengeneza mamilioni ya magari ya kutumia umeme na kwa kufanya hivi inahitaji vyuma hivyo.

Anasema hivi sasa kampuni hiyo ya Schaeffler inanunua bidhaa hizo kutoka nje ila inataka kuyakimu mahitaji yake barani Ulaya.

Kulingana na LKAB safari ya kufikia uchimbaji wa vyuma hivyo ni ndefu kutokana na mchakato wa kupata leseni ya kufanya shughuli hiyo. Inadaiwa huenda ikachukua kati ya miaka 10 na 15 kabla ya kuanza kwa uchimbaji wa madini hayo na mali ghafi kufikishwa sokoni.

China yatawala soko la vyuma nadra duniani

Katika msimu ujao wa machipuko, Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya itapendekeza hatua za kuimarisha uwezo wa Ulaya kupata mali ghafi zake, jambo linalomaanisha kwamba miradi kama huo wa Sweden huenda ikapata uungwaji mkono kutoka kwa Umoja wa Ulaya.

Mji wa Kiruna huko Sweden katika kipindi cha majira ya baridiPicha: Johannes Frandsen/Regeringskansliet

Soko la dunia la vyuma nadra vyenye thamani kwa sasa limetawalwa na China na hakuna uchimbaji wa madini kama hayo unaofanyika Ulaya kwa sasa. Kwasababu hiyo, nchi za Ulaya zinategemea kununua vifaa kutoka nchi za nje ya bara hilo kwa ajili ya kutengeneza magari yenye kutumia umeme na vifaa vya kuzalisha umeme kupitia upepo.

Ripoti moja ya umoja huo wa Ulaya mwaka 2020 ilisema kwamba wakati huo, Umoja wa Ulaya ulikuwa unakidhi asilimia 98 ya mahitaji yake ya vyuma hivyo nadra kutoka China. Hii inamaanisha kwamba kutakuwa na tatizo kubwa iwapo China itasitisha mauzo ya bidhaa hizo kwasababu za kisiasa au kimkakati.

Vyuma hivyo nadra pia vinatumiwa kutengeneza vitu kama simu za kisasa, kompyuta na televisheni.

Chanzo: DPA

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW