Hijja yaanza leo
19 Januari 2005
Mamia kwa maelfu ya mahujaji watajumuika kwa ibada katika msikiti wa Namera kwenye mlima wa Mina mahala ambako watakuweko usiku mzima. Msikiti huo uko katika eneo lililozungukwa na milima kila upande.
Kwa siku nzima mahujaji wake kwa waume wakiwa katika mavazi meupe alama ya usawa wa binaadamu wote mbele ya Mwenyezi Mungu- watakua katika ibada kuomba msamaha na kumshukuru Mwenyezi Mungu, mahala Mtume Mohammed (SAW) alipotoa risala ya mwisho karne 14 zilizopita. Wakati wakikaribia mlima Arafat,Mahujaji watakua wakitamka" Niko hapa Allah kujibu wito wako, Niko Hapa. Labaik Allh Huma Labaik.Kuweko katika mlima Arafat ni muhimu kwani bila ya hivyo, Hijja ya mtu huwa ni batili.
Kuhusiana na huduma kwa mahujaji, tayari kuna hospitali kuu tatu zilizojengwa kwa mahema na zahanati karibu 46, kuwatibu watakaohitaji matibabu, huku polisi wakitumia vipaza sauti kutoa muongozo na kudhibiti harakati na nyendo za mahujaji, mwendo wa mabasi pamoja na kuepusha msongamano na mkanyagano.
Mahujaji wamekua na maombi mbali mbali kwa Mola wao. Kijana mmoja wa miaka 28 , Mohammed Tahrio kutoka Nigeria, alisema anamuomba Mola amjaalie Afya njema na maisha marefu, huku raia mmoja wa Irak kwa jina Amer abbas mwenye umri wa miaka 45 akisema namuomba Mweyezi Mungu, Wamarekani waihame nchi yake, akiongeza " wamarekani ndiyo chanzo na sababu ya uharibifu wote ulioikumba Irak hivi sasa".
Kwa mujibu wa Shirika rasmi la habari la Saudi arabia SPA, kuna mahujaji milioni moja, laki tano thelathini na nne elfu na mia saba sitini na tisa waliowasili mwaka huu kutoka nchi za nje, huku wengine wakiwa ni raia wa saudia wenyewe au wafanya kazi wa kigeni wanaotumika nchini humo.
Kwa mujibu wa nguzo ya tano ya Kiislamu, kila Muislamu mwenye uwezo anatakiwa kuhiji alau mara moja katika maisha yake" Wahaji Lbait Manistatwagha Ilayhi Sabila".
Waislamu Saudi Arabia na kwengineko watasherehekea Idd El hajj kesho Alhamisi ,sherehe inayoambatana na tukio la uchinjaji wa nyama kama kondoo na kadhalika, kukumbuka pale Nabii Ibrahim alipokua tayari kumtoa kafara mwanawe kuonyesha utiifu wake kwa Mwenyezi Mungu na hapo Mola kutoa Miujiza na kumshushia kondoo. Ama kwengineko dunia ikiwa ni pamoja na nchi za Afrika mashariki, siku kuu rasmi ya Idd El Haj ni siku ya Ijumaa.