1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hillary Clinton aelekea Korea Kusini

Aboubakary Jumaa Liongo/AFP19 Februari 2009

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton anatarajiwa kuwasili hii leo nchini Korea Kusini katika ziara yake ya kutembelea mataifa manne ya Asia.

Hillary Rodham Clinton akiwa na wanafunzi nchini IndonesiaPicha: AP

Bibi Clinton anatokea Indonesia ambako alikuwa na mazungumzo na wakuu wa nchi hiyo yenye idadi kubwa kabisa ya waumini wa dini ya kiislam duniani.


Bibi Clinton anategemewa kujadiliana na wakuu wa Korea Kusini juu ya mzozo wa nuklia wa jirani yake Korea Kaskazini.


Waziri huyo wa Nje wa Marekani anawasili huku,Korea Kaskazini ikiendeleza tena vita vyake vya maneno kwa kutishia ya kwamba majeshi yake yako katika hali ya tahadhari ya juu kukabiliana na majeshi ya Korea Kusini.


Akiwa nchini Indonesia Bibi Clinton alikuwa na mazungumzo na Rais Susilo Bambang Yudhoyono wa nchi hiyo pamoja na Waziri wa Nje Hassan Wirajuda.


Mazungumzo yao yalijikita zaidi katika kuimarisha uhusiano katika nchi hizo mbili, masuala ya mazingira pamoja na mgogoro wa kiuchumi unaikabili dunia hivi sasa.


Bibi Clinton aliiomba Indonesia kusaidia juhudi za Rais Barack Obama kuimarisha uhusiano na mataifa ya kiislam baada ya uhusiano huo kuwa mbaya kutokana na sera za utawala uliyopita wa Rais George W.Bush.


´´Kujenga uhusiano imara na Indonesia ni hatua muhimu, kwa upande wa dhamira ya Marekani ya kusikiliza pamoja na kuzungumza na wengine duniani, kuiunga mkono nchi ambayo imeonesha wazi ya kwamba Uislam, demokrasia, na hali ya kisasa siyo tu kwamba vinaweza kuishi kwa pamoja lakini pia kustawi kwa pamoja´´

Hata hivyo bado nchini Indonesia kuna makundi ya waislam wenye itikadi kali ambao mwaka 2002 walifanya shambulio kubwa la bomu katika kisiwa cha Bali.Zaidi ya watu 200 wengi wakiwa watalii wa kigeni waliuawa katika shambulizi hilo.


Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Indonesia Hassan Wirajuda alisema kuwa nchi hiyo inaweza kuwa mshirika mzuri wa Marekani katika juhudi za nchi hiyo kuufufua uhusiano na nchi za kiislam.


´´Kwa upande wake Indonesia siyo tu nchi yenye idadi kubwa ya waislam, lakini kama tulivyothibitisha hapa, demokrasia, uislam na hali ya sasa ya kimaisha vinaweza kuwa pamoja,Na ikiwa ni muhamasishaji wa majadiliano katika masuala ya dini, tamaduni, na maisha ya kisasa, Indonesia itakuwa mshirika mzuri wa Marekani katika dunia ya nchi za kiislam´´


Waziri wa nje wa Marekani Bibi Clinton akihitimisha ziara yake huko Indonesia, alishiriki katika kipindi cha mazungumzo kwenye televisheni ya nchi hiyo pamoja na kutembelea miradi mbalimbali ya kimaendeleo inayofadhiliwa na Marekani.


Bibi Clinton alitembelea kwenye mitaa iliyoko katikati ya mji mkuu wa nchi hiyo Jakata, ambako kuna miradi hiyo ikiwemo ya maji pamoja na ya afya.


Akihojiwa katika kipindi hicho cha televisheni, ambacho ni maarufu kwa vijana nchini Indonesia, Bibi Clinton alishangiliwa sana pale aliposema kuwa makundi ya muziki ya The Beatles na Rolling Stones ni miongoni mwa makundi ya muziki anayoyahusudu, lakini alipoombwa kuimba japo wimbo mmoja wa makundi hayo alikataa kwa kutania ya kwamba kama angeimba basi watu wote waliyokuwepo wangeondoka.



Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW