Hillary Clinton ajitangaza mshindi
8 Juni 2016 Akiwatubia wafuasi wake jijini New York mara baada ya kujizolea ushindi wa New Jersey na New Mexico, waziri huyo wa zamani wa mambo ya nje, alijitangaza kuwa mteule wa chama chake, akisema ushindi huo ni kwa ajili ya kila msichana, ambaye ana ndoto za kuwa chochote atakacho maishani, hata rais.
Muda mchache baadaye akizungumza na televisheni ya ABC, Clinton alisema kwamba amefikia hatua kubwa na ya kipekee.
"Nadhani hii itakuwa hatua kubwa sana kwa kuteuliwa kwangu kwa ajili ya nchi yangu. Bali pia itatuma ujumbe duniani kote - mimi ninawajali sana wanawake. Nimekuwa msemaji nisiyechoka kuwatetea kwa miaka mingi hata nikiwa waziri wa mambo ya nje, niliubeba ujumbe huo ulimwengu mzima." Alisema.
Kama atapitishwa, Clinton atakuwa mgombea wa kwanza mwanamke katika historia ya taifa hilo lenye nguvu kubwa ya kijeshi na kiuchumi duniani.
Rais Barack Obama, aliyemshinda Clinton kwenye kinyang’anyiro kama hiki miaka minane iliyopita, anatazamiwa kumuunga mkono rasmi, mke huyo wa rais wa zamani, Bill Clinton.
Sanders ang'ang'ania kusalia kwenye kinyang'anyiro
Hata hivyo, mpinzani wake, Barnie Sanders, ameshinda kwenye jimbo la North Dakota, akiwa mbele kwa zaidi ya asilimia 63, mbele ya Clinton, na amekataa kujiondoa kwenye kinyang'anyiro akisema kwamba atasonga mbele hadi mstari wa mwisho.
"Jumanne ijayo tutaendelea kupambana kwenye kura za mwisho za mchujo Washington, DC. Tutapambana kwelikweli kwenye kura hizo. Na tukitoka hapo, tutaendeleza mapambano kwenye haki za kijamii, kiuchumi, kikabila na kimazingira huko Philadelphia, Pennsylvania."
Kwa kutaja Pennsylvania, hapana shaka, mwanasiasa huyo anayepiga kampeni dhidi ya umiliki wa kile anachokiita asilimia moja, yaani matajiri na makampuni makubwa nchini Marekani, anakusudia mkutano mkuu wa chama cha Democrat, hapo mwezi Julai.
Trump asema atambwaga Clinton
Kwa upande mwengine, mgombea mteule wa chama cha Republican, Donald Trump, amejizolea ushindi mkubwa kwenye majimbo ya New Mexico, New Jersey, North Dakota na Montana.
Akiwa tayari amejihakikishia kuwa mgombea, Trump alitumia hotuba yake ya ushindi kumshambulia Hillary Clinton kwa kutumia vibaya nafasi yake ya uwaziri wa mambo ya nje, na pia Rais Obama kwa kumfichia makosa yake waziri wake huyo wa zamani.
"Kura za maoni za hivi karibuni zinaonesha kuwa namuangusha Hillary Clinton, na pamoja na matatizo yake yote, na makosa makubwa ambayo ameyafanya, na ameyafanya mengi, tunatazamia kuendelea kuongeza ushindi wetu zaidi na zaidi."
Trump amesalia pekee kwenye kinyang'anyiro hicho, na ndiye anayetegemewa kupambana, na mgombea yeyote wa Democrat, kwenye uchaguzi wa Novemba mwaka huu.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AP/Reuters
Mhariri: Oummilkheir Hamidou