Hillary Clinton akanusha kuwahi kukutana na Epstein
27 Februari 2026
Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton, amesema hakumbuki kuwahi kukutana na mhalifu wa makosa ya kingono, Jeffrey Epstein.
Katika ushahidi wake wa faragha mbele ya Kamati ya Uangalizi ya Baraza la Wawakilishi, Clinton amesema hajawahi kusafiri kwa ndege ya Epstein wala kutembelea kisiwa au makazi yake. Aliongeza kuwa hakuwa na taarifa zozote kuhusu shughuli zake za kihalifu.
Baada ya mahojiano ya saa saba, Clinton aliwashutumu wabunge wa chama cha Republican kwa kujaribu kuhamisha mjadala kutoka uhusiano wa Rais Donald Trump na Epstein.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, James Comer, alisema hakuna anayewashutumu kina Clinton kwa kosa lolote kwa sasa, lakini kamati ina maswali mengi ya kujibiwa.
Rais wa zamani Bill Clinton pia anatarajiwa kutoa ushahidi wake mbele ya kamati hiyo leo Ijumaa.