1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hillary Clinton akubali kuwa mgombea urais wa Democrats

Caro Robi29 Julai 2016

Hillary Clinton amekubali rasmi uteuzi wa chama cha Democratic kuwa mgombea wake wa urais na hivyo kuandikisha historia ya kuwa mwanamke wa kwanza nchini Marekani kuwa mgombea urais wa chama kikubwa cha kisiasa.

Picha: Reuters/L. Nicholson

Akikubali uteuzi huo hii leo mbele ya maelfu ya wajumbe waliohudhuriua mkutano mkuu wa chama cha Democratic Philadelphia, Hillary Clinton ameahidi kuwa Rais wa Wamarekani wote, watakaompigia kura na wasiompigia, wafuasi wa vyama vya Repulican, Democratic na wa vyama huru.

Waziri huyo wa zamani wa mambo ya nje ameahidi fursa za kiuchumi kwa kila mmoja na kupinga taswira iliyotolewa na mpinzani wake, mgombea urais wa chama cha Republican Donald Trump kuhusu mustakabali wa siku za usoni wa Marekani.

Clinton ambaye anajinadi kama mgombea anayestahili zaidi kuiongoza Marekani kutokana na tajriba yake ya kushikilia nyadhifa kuu serikalini na katika siasa, amemponda Trump kwa kumtaja mtu anayewatia Wamarekani hofu na asiyekuwa na sera madhubuti.

Amemkosoa Trump kwa kutaka kuwagawanya Wamarekani na kusema mgombea huyo wa Republican hawezi kutatua matatizo ya Wamarekani.

Clinton amponda Trump

Bi Clinton mwenye umri wa miaka 68 amechukua muda mwingi wa hotuba yake kumkejeli Trump akisema mtu ambaye unaweza kumkera kirahisi na ujumbe katika Twitter si mtu wanayeweza kumuamini na silaha zao za nyuklia kwani haiba yake haimuwezeshi kukabiliana na matatizo.

Mgombea urais wa Democrats Hillary ClintonPicha: Reuters/G. Cameron

Katika hotuba yake iliyodumu kwa saa moja, Bi Clinton ameelezea mikakati yake kuhusu namna atakavyoboresha uchumi wa Marekani, kwa kutoa fursa zaidi za kazi na malipo bora.

Na kuangazia nia yake ya kuhakikisha mshikamano na kushirikisha kila upande, akijaribu kuwatuliza wafuasi sugu wa Bernie Sanders na kuwashawishi wapiga kura wasioegemea vyama viwili vikuu vya upinzani katika wakati alioutaja kuwa wa kufanya maamuzi muhimu.

Sera alizoziangazia zimeoekana kuwa muendelezo wa sera za Obama zikiwemo, kushughulikia mabadiliko ya hali ya hewa, kufanyia maguezi sheria za uhamiaji, kudhibiti umiliki wa bunduki, elimu, miundo mbinu na uwekezaji.

Hillary Clinton aandikisha historia

Rais wa Marekani Barack Obama, mumewe Hillary, Bill Clinton watu mashuhuri, viongozi wa kijeshi na wa polisi wamemuidhinisha na kumtaja Bi Clinton kuwa mwenye ujuzi, uwezo, ari na anayestahili zaidi kuiongoza Marekani.

Mgombea urais wa Republican Donald TrumpPicha: Reuters/C. Allegri

Baada ya hotuba yake, katika mkutano huu mkuu wa chama cha Democratic ulioanza tangu Jumatatu, Clinton na mgombea mwenza Tim Kaine wataanza kampeini kabambe leo katika majimbo ya Pennsylvania na Ohio kwa siku tatu zijazo.

Imesalia miezi mitatu tu kabla ya uchaguzi mkuu utakaofanyika tarehe 8 mwezi Novemba, ambapo Wamarekani watafanya maamuzi kati ya kumchagua Hillary Rodham Clinton, mwanamke wa kwanza katika historia ya nchi hiyo kuwa Rais au kumchagua Donald Trump mwenye umri wa miaka 70 ambaye amesema ni yeye tu aliye na uwezo wa kuyatatua matatizo yanayoizonga Marekani.

Mwandishi: Caro Robi/afp/Reuters/ap

Mhariri: Josephat Charo

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi