1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Sheria na HakiMarekani

Hillary Clinton atoa ushahidi kuhusu Epstein

27 Februari 2026

Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton, ametoa ushahidi wa zaidi ya saa sita mbele ya Kamati ya Uangalizi ya Baraza la Wawakilishi kuhusu nyaraka zinazohusiana na kashfa ya Jeffrey Epstein.

Marekani, Washington D.C. 2017 | Hillary na Bill Clinton kabla ya kuapishwa kwa Trump katika Jengo la Bunge la Marekani (US Capitol).
Rais wa zamani Bill Clinton na mke wake Hillary walikuali kutoa ushahidi mbele ya Kamati ya uchunguzi wa bunge kuhusu uhusiano wao na Epstein.Picha: Win McNamee/AFP

Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton, ametoa ushahidi wa zaidi ya saa sita mbele ya Kamati ya Uangalizi ya Baraza la Wawakilishi kuhusu nyaraka zinazohusiana na kashfa ya Jeffrey Epstein. Ushahidi huo umefungua siku mbili za mahojiano ambazo pia zitamhusisha rais wa zamani Bill Clinton.

Akizungumza katika taarifa yake ya ufunguzi, Clinton alisema hakuwa na taarifa zozote kuhusu uhalifu wa Epstein au mshirika wake, Ghislaine Maxwell. Alisisitiza kuwa hakumbuki kuwahi kukutana na Epstein wala kusafiri kwa ndege au kutembelea makazi yake.

"Sijui ni mara ngapi nililazimika kusema kwamba sikumjua Jeffrey Epstein. Sijawahi kwenda katika kisiwa chake. Sijawahi kwenda katika nyumba zake. Sijawahi kwenda katika ofisi zake. Hivyo, hilo liko kwenye kumbukumbu mara nyingi," alisema Clinton katika mazungumzo na waandishi wa habari baada ya kuhojiwa.

Baada ya kikao hicho cha faragha kilichofanyika mjini New York, Clinton aliwaambia waandishi wa habari kuwa alijibu kila swali kwa kadri ya uelewa wake. Alidai kuwa baadhi ya maswali yalikuwa yakijirudia na mengine yaliingia katika nadharia za njama zisizo na msingi.

Hata hivyo, mwenyekiti wa kamati hiyo, James Comer, alisema bado hawajaridhishwa kikamilifu na baadhi ya majibu waliyoyapata. Comer amekuwa akiongoza uchunguzi huo chini ya wabunge wa Republican.

Waathirika zaidi wa kashfa ya ngono ya Epstein. Aliekuwa Mwanamfalme wa Uigereza Andrew alivuliwa nyadhifa zake kabla ya kukamatwa kwa matumizi mabaya ya ofisi.Picha: Gareth Cattermole/Getty Images

"Nadhani haya yalikuwa mahojiano yenye tija leo. Nadhani tulijifunza mengi. Kulikuwa na maswali mengi tuliyouliza ambayo hatukuridhishwa na majibu tuliyopata, lakini tutaendelea kusonga mbele," alisema mwenyekiti huyo wa kamati ya uchungzi kuhusu mahojiano na Clinton.

Miito ya kumhoji pia Rais Trump

Uchunguzi huu unalenga kuelewa kwa nini Wizara ya Sheria haikufungua mashtaka mapya dhidi ya Epstein baada ya makubaliano ya mwaka 2008, na pia kuchunguza uhusiano wake na viongozi wa kisiasa na wafanyabiashara mashuhuri. Epstein alifariki mwaka 2019 akiwa gerezani akisubiri kusikilizwa kwa kesi ya biashara ya ngono, jambo lililoibua maswali mengi nchini Marekani.

Clinton amesisitiza kuwa kama "kila mtu mwenye maadili,” alishtushwa na ukubwa wa uhalifu uliodaiwa kufanywa na Epstein. Amesema alimfahamu Ghislaine Maxwell kama mtu wa kufahamiana tu katika mikutano ya kijamii na hafla za taasisi za hisani.

Nyaraka zilizojumuishwa katika utoaji wa mafaili ya Jeffrey Epstein na Wizara ya Sheria ya Marekani zilipigwa picha Ijumaa, Januari 2, 2026.Picha: Jon Elswick/AP Photo/picture alliance

Wakati huo huo, wabunge wa chama cha upinzani cha Democratic wameitaka kamati hiyo kuhakikisha kuwa ushahidi wote unawekwa wazi kwa umma ili kuondoa uvumi na nadharia za njama. Baadhi yao pia wametaka Rais Donald Trumpnaye ahojiwe ili kutoa maelezo kuhusu uhusiano wake wa zamani na Epstein.

Kamati hiyo imesema itachapisha video na maandishi ya ushahidi wa Clintons katika siku zijazo. Rais wa zamani Bill Clinton anatarajiwa kutoa ushahidi wake leo Ijumaa, huku sakata ya Epstein ikiendelea kuwa mjadala mkubwa wa kisiasa na kisheria nchini Marekani.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW