Hillary Clinton atoa wito wa kuachiwa Suu Kyi
22 Julai 2009Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani, Hillary Rodham Clinton ameitaka Myanmar kumuachia huru kiongozi wa upinzani na mwanadiplomasia Aung San Suu Kyi, akisema kuwa hatua hiyo huenda ikafungua njia ya uwekezaji nchini humo.
Akizungumza siku moja kabla ya kuanza kwa mkutano wa masuala ya usalama wa jumuiya ya nchi za Kusini-Mashariki kwa Asia, ASEAN, katika mji wa Phuket, Thailand, Bibi Clinton amesema kitendo cha kuachiwa huru Suu Kyi, kitafungua fursa, angalau kwa Marekani kuongeza uhusiano wake na Myanmar, ikiwemo kuwekeza nchini humo. Amesema wakati nchi za Kusini-Mashariki mwa Asia zinaelekea katika njia moja, Myanmar inaelekea katika upande tofauti.
Bibi Clinton amesema kuwa Marekani ingependa kuona utawala wa kijeshi wa Myanmar unabadili sera zake mbalimbali, ikiwemo suala la kuachiwa huru Suu Kyi. Mapema leo, Bibi Clinton alisema nchi hizo za Kusini-Mashariki mwa Asia zifikirie kuifukuza uwanachama nchi ya Myanmar, endapo haitamuachia huru mwanadiplomasia huyo, mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel.
Mbali na Marekani kuitaka Myanmar kumuachia huru Suu Kyi, Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Australia, Stephen Smith, amesema kuna haja ya haki za mwanadiplomasia huyo kuheshimiwa.
Katika hatua nyingine, waziri huyo wa mambo ya kigeni wa Marekani amesaini mkataba wa ushirikiano na usalama na nchi hizo za Kusini-Mashariki mwa Asia, ishara inayoonyesha kuwa Marekani imerejea katika eneo hilo. Mkataba huo tayari ulisainiwa na nchi zilizoianzisha jumuiya hiyo ya ASEAN, mnamo mwaka 1976. Aidha, washirika wengine katika mazungumzo ya ASEAN, kama vile Australia, China, India, Japan na Korea Kusini, tayari wamesaini mkataba huo.
Wakati huo huo, Bibi Clinton amezitaka nchi washirika wake kuwa na msimamo wa pamoja kuhakikisha Korea Kaskazini inaachana na mpango wake wa kutengeneza silaha za nyuklia. Wito huo ameutoa baada ya kukutana na mawaziri wa mambo ya kigeni wa China, Russia na Thailand. Amesema mawaziri wote hao wa mambo ya kigeni wamekubaliana kuwa msimamo mmoja usiobadilika ndio njia pekee ya kuifanya Korea Kaskazini iachane na mpango wake huo. Mpango wa nyuklia wa Korea Kaskazini umekua ajenda kuu katika mkutano huo wa kiusalama utakaofanyika kesho.
Mkutano huo utahudhuriwa na wanachama 10 wa ASEAN, ambao ni Brunei, Cambodia, Indonesia, Laos, Malaysia, Myanmar, Ufilipino, Singapore, Thailand na Vietnam. Kundi jingine mshirika wa nchi za ASEAN ni pamoja na Australia, Bangladesh, Canada, China, Umoja wa Ulaya, India, Japan, Korea Kaskazini na Korea Kusini. Nchi nyingine ni Mongolia, New Zealand, Pakistan, Papua Guinea, Russia, Sri Lanka, Timor Mashariki na Marekani.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (DPAE/AFP)
Mhariri:Miraji Othman