1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hillary Clinton awasili Korea Kusini

Aboubakary Jumaa Liongo/AFP19 Februari 2009

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton amewasili Korea Kusini -kituo chake cha tatu cha ziara yake ya mataifa manne barani Asia.

Bibi Hillary Rodham Clinton,Picha: AP

Akizungumza na waandishi wa habari akiwa ndani ya Ndege kuelekea Seol akitokea Jakata Indonesia, Bibi Clinton amesema kuwa wasi wasi wa kuwepo kwa mabadiliko ya uongozi huko Korea Kaskazini kutokana na ripoti juu ya hali mbaya ya afya ya kiongozi wa taifa hilo kunaonekana kuwa kikwazo katika jitihada za kuitaka nchi hiyo isitishe mpango wake nuklea.


Bibi Clinton amesema kuwa kutokana na hali hiyo kuna umuhimu wa kuwepo kwa mkakati mpya ili kuweza kuondoa mkwamo huo.


Amesema kuwa Korea Kaskazini imekuwa ikichukua msimamo mkali kwenye mazungumzo ya pande sita kuhusiana na mpango wa silaha za nuklia, pengine ni kutokana na harakati za kumtafuta mrithi wa kiongozi wa nchi hiyo, Kim Jong-ll ambaye iliarifiwa Agosti mwaka jana kuwa alipatwa na ugonjwa wa kiarusi.


Waziri huyo wa Nje wa Marekani amesema mazingira hayo yanaipatia Korea Kusini ambayo ni mshirika wa nchi za magharibi wakati muhimu na maalum kukabiliana na changamoto za Korea Kaskazini, nani ataweza kuwa mrithi wa kiti cha urais na atakuwa na faida gani kwao.


Korea Kaskazini imetangaza hii leo kuwa majeshi yake yako katika hali ya tahadhari kubwa kupambana na Korea Kusini.


Radio ya taifa ya Korea Kaskazini ilitangaza taarifa ya jeshi la nchi hiyo ikimshutumu Rais Lee Myung-Bak kwa kuandaa mipango ya kutaka kuvamia nchi hiyo na kuonya kuwa jeshi hilo liko tayari kukabiliana na tishio hilo.


Lakini Bibi Clinton amesema kuwa Korea Kusini inaitegemea Marekani katika kusaidia kuirejesha Korea Kaskazini katika meza ya mazungumzo ya kuharibu vinu vyao vya nuklia na kuachana na sera za kibabe.


Amesema kuwa ni lengo la Marekani kuwa na mkakati ambao utaweza kufanikisha azma hiyo mnamo wakati huu ambapo hali jumla ya kiuongozi nchini Korea Kaskazini haifahamiki.


Bibi Clinton anategemewa kuwa na mazungumzo na Rais Lee Myung-Bak pamoja na Waziri wa Nje wa Yu Myung-Bak.Pia atakutana na makamanda wa kikosi cha Marekani nchini humo.Marekani ina kiasi cha wanajeshi elfu 28 na mia tano huko Korea Kusini.


Waziri huyo wa Nje wa Marekani amewasili akitokea Indonesia ambako aliiomba nchi hiyo isaidie mipango ya Rais Barack Obama kurejesha uhusiano mzuri na nchi za kiislam.


Bibi Clinton atahitimisha ziara yake ya Asia nchini China ambako anatarajiwa kuwasili hapo kesho.



►◄




Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW