1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hisia mseto Uganda baada ya shambulio la bomu Kampala

Lubega Emmanuel25 Oktoba 2021

Waganda wana hisia mseto kufuatia kisa cha mripuko wa bomu usiku wa kuamkia Jumapili katika sehemu moja ya starehe ambapo watu wawili wamethibitishwa kuuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa vibaya.

Uganda I Explosion in Kampala
Picha: Abubaker Lubowa/REUTERS

Haya yamefanyika wakati hapo awali mataifa ya kigeni yalikuwa yamewatahadharisha raia wake walioko Uganda kwamba pangetokea shambulio lakini serikali ikadai kuwa habari hizo ni za kupotosha. 

Shambulio hilo la bomu ambalo hadi sasa limefufua  hofu kuhusu hali ya usalama mjini Kampala lilitokea saa tatu hivi za usiku katika baa moja eneo la kitongoji cha Komamboga.

Kulingana na walioshuhudia kisa hicho wakiwemo wafanyakazi wa sehemu hiyo ya starehe, wanaume wanne waliokuja na kitu katika karatasi ya plastiki na kukiweka chini ya meza ndiyo waliofanya shambulio hilo.

Mtu mmoja alifariki papo hapo mara tu baada ya bomu hilo kulipuka na mwingine amefariki wakati akipokea matibabu. 

Watu watatu waliripotiwa kuuawa kufuatia shambulizi hilo.Picha: Hajarah Nalwadda/XinHua/picture alliance

Msemaji wa Polisi Fred Enanga amefafanua kuwa wameanzisha uchunguzi kuhusiana na kisa hicho na miongoni mwa taarifa wanazofuatilia ni kwamba watu hao walikuwa wamevalia fulana za chama kikuu cha upinzani NUP. 

Hata hivyo, watu mbalimbali wameelezea kuwa mtu kuvalia mavazi ya upinzani isimaanishe kuwa wao ndiyo wamehusika kwani hata mataifa ya kigeni yalitoa tahadhari kuhusu shambulio hilo wiki iliyopita, polisi ikapuuza. Aidha wanashangaa kwa nini sehemu hiyo ya stahere ilikuwa wazi saa za kutotoka nje kudhibiti COVID-19.

Baaada ya shambulio hilo, rais Museveni amesisitiza kuwa waliohusika katika  kisa hicho cha ugaidi watakamatwa haraka iwezekavyo.