1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hisia za chuki dhidi ya wayahudi zalaaniwa Ujerumani

Oumilkheir Hamidou
15 Desemba 2017

Rais wa Ujerumani Steinmeier ametoa wito wa kuchukuliwa hatua dhidi ya hisia za chuki kwa wayahudi. Wawakilishi wa makanisa waelezea wasi wasi wao pia huku balozi wa Israel akitoa wito mitindo ya bendera kutiwa moto.

Demonstranten verbrennen Fahne mit Davidstern in Berlin
Picha: picture-alliance/dpa/Jüdisches Forum für Demokratie und gegen Antisemitismus e.V.

Rais wa shirikisho Steinmeier ameonya vikali dhidi ya kuongezeka hisia za chuki dhidi ya wayahudi nchini Ujerumani."Kwamba katika viwanja vya Ujerumani bendera za Israel zinachomwa moto, ni jambo lililonishitua na la fadhaa kwangu" amesema rais wa shirikisho alipomkaribisha balozi wa Israel, katika kuadhimisha miaka 70 tangu taifa la Israel lilipoundwa, sherehe zinazotarajiwa kuanza mwakani. "Mwenye kuchoma bendera, sio tu anaonyesha chuki dhahiri dhidi ya Israel bali pia haelewi au haheshimu  tafsiri ya kuwa mjerumani

Kanisa kuu la kikatoliki la mjini ColognePicha: picture-alliance/Geisler-Fotopress/C. Hardt

Makanisa mawili makuu ya Ujerumani yalaani chuki dhidi ya wayahudi

Wawakilishi wa makanisa yote mawili  makuu nchini Ujerumani wameeleza pia wasi wasi wao kutokana na visa vya hivi karibuni vya chuki dhidi ya wayahudi. Katika  ripoti yao iliyochapishwa na shirika la habari la KNA, viongozi hao wa makanisa wameonya na kusema visa vya chuki dhidi ya wayahudi vimeongezeka barani ulaya na hasa katika nchi za ulaya ya mashariki.

Nae balozi wa Israel Jeremy Issacharoff akatoa wito ipigwe marufuku mitindo ya bendera kuchomwa moto.

Katika maandamano yaliyoitishwa hivi karibuni, wapalastina na waturuki wanaoishi humu nchini , waliichoma moto bendera ya Israel yenye nyota ya David mbele ya lango la Brandenburg kulalamika dhidi ya uamuzi wa rais wa Marekani Donald Trump kuutambua mji wa Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel. Miongoni mwao kuna waliokuwa wakipaza sauti kudai "wayahudi wauliwe.

Msemaji wa serikali kuu Steffen SeibertPicha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

Serikali kuu pia inalaani chuki dhidi ya wayahudi

"Hakuna hisia yoyote ya chuki , si ndogo si kubwa, si dhaifu na wala si kali inayoweza kuvumiliwa nchini Ujerumani. Ujerumani inaheshimu jukumu lake la kihistoria na kujifunza kutokana na yaliyotokea katika vita vikuu vya pili vya dunia na inapinga aina yyoyote ya ubaguzi na chuki dhidi ya wayahudi" amesisitiza rais wa shirikisho Frank-Walter Steinmeier.

Serikali kuu ya Ujerumani pia ilisema imefadhaishwa na maandamano ya mwishoni mwa wiki dhidi ya kutambuliwa mji wa Jerusalem na rais wa Marekani kuwa mji mkuu wa Israel. Msemaji wa serikali Steffen Seifert amewaambia maripota kwamba hata kama Berlin haiungi mkono uamuzi wa raisTrump, hata hivyo serikali inalaani vikali maandamano ya chuki dhidi ya Israel na wayahudi.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/epd/KNA(AFP

Mhariri:Yusuf Saumu