1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hoffenheim kuwapunguzia mishahara wachezaji

Josephat Charo
5 Machi 2021

Klabu ya Bundesliga Hoffenheim inatafakari kuwapunguzia misharaha wachezaji wake kutokana na athari za kiuchumi zilizosababishwa na janga la corona.

TSG Hoffenheim v SV Werder Bremen - Bundesliga
Picha: Alex Grimm/Getty Images

"Ni jambo lisiloepukika kutafakari kupunguza bajeti ya mishahara ya kikosi cha wachezaji wa kulipwa hali zikiwa ngumu kama zilivyo sasa," Alexander Rosen, mkurugenzi wa klabu hiyo, aliliambia gazeti la kila siku la Heilbronner.

"Matumizi na mishahara ni mambo ambayo lazima yawe katika uwiano. Iwapo mapato ya televisheni, mapato ya watazamaji na uhamisho wa wachezaji yanakoma, unaweza tu kupunguza matumizi kama hakuna njia nyingine mpya za kuingiza mapato. Hilo ni rahisi kuelewa," aliongeza kusema Rosen.

Hoffenheim bado wana fedha wanazoweza kuzitumia kuwasaidia kupitia kipindi hiki kigumu kutokana na mapato ya uhamisho wa wachezaji takriban euro milioni 120 ya msimu wa kiangazi mnamo mwaka 2019.

"Katika kipindi kirefu hiyo haitafanya kazi. Si kwetu sisi, wala kwa klabu yoyote," alisema mkurugenzi huyo mwenyewe umri wa miaka 41.

Rosen alisema pia huenda akafikiria kuchukua hatua kutegemea na mabadiliko katika soko la uhamisho wakati huu wa janga la corona. Wachezaji kama Andrej Kramarich au Florian Grillitsch, ambao mikataba yao inafika mwisho mwaka 2022, watalazimika kuuzwa mwishoni mwa msimu huu.

"Ikishindikana kurefusha mkataba mapema na wakati huo huo hakuna hali nzuri katika soko kwa mchezaji, na hivyo uwezekano wa kupata mapato makubwa ya uhamisho, katika kesi moja moja unaweza kulazimika kutafakari ikiwa utatia dau katika uhamisho wa bure bila malipo ili kuendeleza ubora wa mchezo," alisema Rosen. "Lakini hatujafikia hapo bado."

(dpa)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW