Hoffenheim yatamba Bundesliga
7 Novemba 2008Baada ya jana FC Cologne kufungua duru ya mwishoni mwa wiki hii ya Bundesliga-Ligi ya ujerumani, mashabiki wankodoa macho na kutega masikio kujua iawapo klabu chipukizi ya Hoffenheim itaendelea kuwika kesho ikipambana na Hertha Berlin. Changamoto ya kusisimua zaidi pengine ni ile kati ya mabingwa Bayern Munich na mahasimu wao Schalke 04 mjini Gelsenkirchen.
Katika Premier League-Ligi ya Uingereza,leo ni leo ,asemae kesho muongo:madume wawili Manchester united na Arsenal wanakutana.Bingwa wa dunia wa wezani wa juu ulimwenguni Vitali Klitschko kutoka Ukrain alazimishwa kuingia ringini kutetea taji lake la WBC.
Mashabiki wa Bundesliga wanajiuliza lini gari moshi la Hoffenheim litazimwa.Kwani timu hii iliopanda msimu huu kutoka daraja ya pili, inarudi uwanjani kesho ikiwa bado kileleni mwa Bundesliga na ikithubutu kutamba Berlin dhidi ya Hertha, utakua ushindi wake wa 6 mfululizo na hii ni rekodi katika Bundesliga .Hoffenheim iliikomea Karlsruhe mabao 4-1 jumamosi iliopita na kutia mfukoni ushindi wao wa 5 mfululizo huku mshambulizi wao hatari Ibisevic akikomea tayari mabao 13 katika mechi 11.
Hoffenheim, imeshatia mabao 25 katika lango la adui.Kesho lakini itakua na kibarua kikubwa kutamba jiji kuu.Hertha Berlin lakini,inaingia uwanjani ikikumbuka ilizabwa mabao 5-1 na Werder Bremen.Kesho pia ni changamoto kati ya Schalke na mabingwa Bayern Munich waliopo nafasi ya 3.Schalke iko nafasi ya 4 katika ngazi ya Ligi .
Schalke imekuwa na siku 1 tu ya kupumua baada ya kupambana na Racing Santander wakati mabingwa Bayern Munich wamepumua via kutosha kufuatia sare yao ya bao 1:1 juzi jumatano na na Fiorentina ya Itali.Hamburg ina miadi na Borussia Dortmund leo wakati Bremen wanakutana na Bochum.Hii inafuatia pigo waliopata nyumbani la mabao 3-0 kutoka kwa wagiriki Panathniakos juzi jumaane katika kombe la champions League barani ulaya.Mpambano wa mwisho kesho jumapili utakua kati ya Stuttgart na Frankfurt.
Ama kileleni mwa changamoto za Premier League Leo ni mpambano kati ya Arsenal na Manchester United.Arsenal imeshindwa mara 3 tayari msimu huu na hivyo haidiriki pigo jengine hii Leo,kwani wako pointi 6 kutoka viongozi wa ligi Chelsea.Jogoo wa Manchester united Ryan Giggs akionea huruma Arsenal ameserma imeteseka sana na kuumia kwa wachezaji wake wengi na wengine kufungiwa kucheza kama vile mtogo Emmanuel Adebayor na Robin van Persie kutoka Holland .
Liverpool waliohitaji bao la penalty kati ya wiki kuondoka sare na Atletico Madrid katika Champions League ,wanatazamia kurejea kutamba mbele ya West Brom.Orodha ya Premier League inaoongozwa na Chelsea,ikifuatwa na Liverpool huku Manchester United ikinyatia nafasi ya 3.Arsenal iko nafasi ya 4.Chelsea itakuwa uwanjani kesho nyumbani mwa Blackburn Rovers.
Katika serie A, Ligi ya Itali, Catania ina miadi na Cagliari wakati Juventus itafunga safari kesho kucheza na Verona.Fiorentina iko nyumbani kwa changamoto na Atalanta Bergamo.
Nje ya dimba, bingwa wa mabondia wa wezani wa juu ulimwenguni , Vitali Klitschko wa Ukraine ,mwenyekambi yake Hamburg,Ujerumani ameamrishwa lazima aingie ringini kutetea taji lake la wezani wa juu ulimwenguni la shirika la WBC dhidi ya Juan Carlos Gomes mwenye pia kambi yake Ujerumani. Shirika la WBC liliafikiana katika kikao chake huko Chengdu,China juzi alhamisi ,kwamba ikiwa waandazi wa mabondia hao 2 wakishindwa kukubaliana juu ya mpambano huo ,changamoto hiyo itakuwa wazi kwa changamoto nyengine hapo desemba 19. Klitchko akiwa na umri wa miaka 37, alirejea ringini baada ya mapumziko ya miaka 4 na kutwaa taji la WBC mwezi uliopita alipomtwanga Samuel Peter wa Nigeria.Mnigeria huyo aliamua kutorudi ringini baada ya duru ya 8.
Nduguye mchanga Wladmir , atatetea taji lake la IBF na WBO kwa mpambano na bingwa wa zamani Hasim Rahman wa marekani huko Mannheim,Ujerumani desemba 13.
Ikiwa kila kitu kitaenda swa, changamoto kati ya Vitali klitschko na Gomez itakuwa mwezi machi mwakani pia nchini Ujerumani.Klitchko alitaka kuamua mwenyewe lini kutetea taji lake lakini bodi ya magavana ya Shirika la WBC limeamua lazima apigane na mbondia wa kwanza anaesubiri-nae ni Gomez kutoka Cuba.Mkuba huyu alimshinda muukraine Vladmir Virchis hapo Septemba 27 mjini Hamburg.