Hofu juu ya kuibuka tena IS baada ya Marekani kuondoka Syria
8 Oktoba 2019Kwa muda wa miezi kadhaa Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erogan amekuwa anatishia kupeleka majeshi yake katika nchi jirani ya Syria. Jumamosi iliyopita Rais huyo alisema ataitekeleza hatua hiyo kwa kuwapeleka askari wa anga na wa nchi kavu kwa lengo la kutenga ukanda wa usalama kwenye mpaka kati ya Uturuki na Syria.
Lengo la Erdogan ni kuyarudhisha nyuma majeshi ya Wakurdi wa Syria yanaoongozwa na kundi la YPG. Uturuki inayaona majeshi hayo kuwa ni tishio kwa usalama wa taifa lake.Hata hivyo majeshi hayo ya Wakurdi ndiyo yaliyoshirikiana na majeshi ya Marekani katika harakati za kupambana na kuwashinda wapiganaji wanaojiita dola la kiislamu IS.
Marekani imekuwa inatafuta suluhisho la kuiridhisha Uturuki na wakati huohuo ikijaribu kuyazingatia maslahi ya Wakurdi. Hata hivyo mkakati huo haukufua dafu, na badala yake Rais Donald Trump manmo Jumapili alitangaza hatua ya kuyaondoa mara moja majeshi ya Marekani yaliyokuwa yanashirikiana na majeshi ya Wakurdi.
Mapema jana majeshi ya kidemokrasia ya Syria SDF yalithibitisha kuanza kuondoka kwa majeshi ya Marekani kutoka kwenye eneo lililokuwa linadhibitiwa na majeshi ya Wakurdi. Pamoja na hayo Marekani imesema wazi kwamba majeshi yake hayatayalinda majeshi hayo ya SDF ikiwa majeshi ya Uturuki yataivamia sehemu hiyo ya kaskazini mwa Syria.
Hatua ya rais Erdogan itasababisha maafa siyo tu kaskazini mwa Syria na kwenye ukanda huo bali duniani kote. Maalfu kwa maalfu ya wapiganaji wanaojiita dola la kiislamu pamoja na wale wanaowaunga mkono wanashikiliwa kwenye kambi za wakurdi kaskazini mwa Syria.
Mbunge wa chama cha CDU hapa nchini Ujerumani Roderich Kiesewetter ametahadharisha juu ya hatari ya wapiganaji hao kukilimbilia nchini Irak. Amesema jambo hilo litahatarisha usalama wa dunia. Mbunge huyo pamoja na wanasiasa wengine wa Umoja wa Ulaya wanahofia kuimarika kwa wapiganaji wa IS baada ya Marekani kuyaondoa majeshi yake na pia kutokana na uamuzi wa Rais Erdogan wa kuivamia Syria kaskazini. Umoja wa Ulaya una wasi wasi mkubwa juu ya matukio hayo.
Kamishna wa Umoja huo Maja Kocijancic amesema ingawa jumuiya hiyo inayatambua maslahi ya Uturuki, inaunga mkono mamlaka ya Syria juu ya mipaka yake. Ameeleza kuwa hatua ya Uturuki ya kuivamia sehemu ya kaskazini mwa Syria haina uhalali.
Kamishna huyo amesema mapigano mapya kaskazini mashariki mwa Syria yataleta maafa makubwa zaidi kwa raia pamoja na kusababisha idadi kubwa ya wakimbizi wa ndani na kuvuruga juhudi za kuleta amani zinazoungwa mkono na Umoja wa Ulaya.
Mjumbe wa baraza la mahusiano ya nje kwenye Umoja wa Ulaya Julien Barnes-Dacey ametahadharisha kwamba Uturuki haijaandaa mipango yoyote endapo magaidi wa dola la Kiislamu wataibuka tena. Mjumbe huyo amesema Uturuki inalenga kuhakikisha kwamba majeshi ya Wakurdi yanaondolewa kaskazini mashariki mwa Syria.
Maalfu ya wapiganaji wanaojiita dola la kiislamu kutoka Ulaya bado wanashikiliwa kwenye kambi za Wakurdi. Baadhi yao ni raia wa Ujerumani. Marekani inazitaka nchi za Ulaya ziwarudishea watu hao ili wahukumie nyumbani. Hata hivyo mjumbe baraza la mahusiano ya nje kwenye Umoja wa Ulaya Julien Barnes-Dacey amesema nchi za Ulaya zimeziba masikio.
Mwandishi:Zainab Aziz/ https://p.dw.com/p/3QrIa