Hofu ya maambukizi mapya ya Ebola Mali
17 Novemba 2014Hofu ya Ebola nchini Mali ilianza na muuguzi mgonjwa katika hospitali inayowatibu matajiri na wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa mjini Bamako aliyegunduliwa kuwa na ugonjwa huo baada ya kufa. Muda mfupi baadaye madaktari walianza kumchunguza mzee wa umri wa miaka 70 aliyekufa kutokana na Ebola baada ya kufikishwa katika hospitali hiyo kutokea Guinea akiwa na matatizo ya figo. Mpaka sasa watu watatu wamekufa kutokana Ebola nchini Mali huku vifo vingine viwili vikishukiwa katika mji mkuu Bamako.
Mjumbe mkuu wa shirika la afya duniani WHO nchini Mali, Ibrahima Fall, ameonya kuhusu visa vipya vya maambukizi ya Ebola nchini humo. "Tunahitaji kuiangalia hali halisi. Kama tunawafuatilia watu zaidi ya 200, tunahitaji kugundua kwa haraka kisa kipya cha maambukizi. Hili linaweza kutokea na tunahitaji kujiandaa. Timu ziko nyanjani kuwafuatilia mara mbili kwa siku, tukitarajia kugundua visa vipya. Inawezakana."
Marekani imetangaza jana itawachunguza abiria wote wanaowasili kutokea Mali. Mali inajiunga na Sierra Leone, Guinea na Liberia kama nchi ambazo wasariri wake wanalazimika kuchunguzwa kama wana Ebola pindi wanapowasili Marekani. Uchunguzi huo unaanza leo kwa wasafiri 15 hadi 20 wanaowasili kila siku kutoka Mali. Uamuzi huo umechukuliwa huku daktari wa Marekani, Martin Salia, akitibiwa Ebola katika hospitali ya Nebraska huko Omaha, akiwa katika hali mbaya sana tangu alipowasili kutoka Sierra Leone.
Wataalamu wa China wawasili Liberia
Wakati haya yakiarifiwa timu kubwa ya wafanyakazi 160 wa afya kutoka China imewasili nchini Liberia kuzipiga jeki juhudi za kupambana na Ebola. Balozi wa China nchini Liberia, Zhang Yue, amesema madaktari, wataalamu wa magonjwa na wauguzi watafanya kazi katika kituo cha kutoa matibabu kwa wagonjwa wa Ebola watakachokijenga kwa thamani ya dola milioni 41 kitakachoanza kufanya kazi katika siku 10 zijazo.
Kiongozi wa timu hiyo, Wang Yungui, amesema watajikita katika masuala manne muhimu. "Kwanza tutaboresha utendaji katika wodi zinazojengwa ziwe bora zaidi kwa ajili ya matibabu ya magonjwa ya kuambikiza na zifae kwa kazi ya hospitali maalumu. Pili tutaweka vifaa vya matibabu na kuvizindua. Tatu, tutaimarisha mafunzo ya wafanyakazi wa afya na nne tutashirikiana na idara za Liberia na shirika la afya duniani na kujumuika na operesheni zao kuunda mtandao imara na madhubuti."
Liberia imeathirika zaidi na Ebola Afrika Magharibi huku raia wake 2,812 wakiwa wamekufa kutokana na ugonjwa huo, kati ya jumla ya watu 5,165 waliokufa katika nchi tatu Sierra Leone na Guinea na Liberia yenyewe, kwa mujibu wa data za shirika la afya duniani, WHO. Rais wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf, jana alitangaza lengo la kutokuwa na visa vya maambukizi mapya ya Ebola nchini humo kufikia sikukuu ya Krismasi Desemba 25 mwaka huu.
Mwandishi: Josephat Charo/RTRE/AFPE
Mhariri: Daniel Gakuba