1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaGeorgia

Hofu ya udikteta yawapelekea Wageorgia kuandamana

9 Machi 2023

Polisi ya Georgia imewafyatulia mabomu ya kutoa machozi maelfu ya waandamanaji walipokuwa wakiandamana kwa siku ya pili mfululizo kupinga sheria inayofanana na ile iliyowekwa Urusi kuwanyamazisha wakosoaji wa serikali.

Georgien | Protest gegen Gesetzentwurf zur Transparenz ausländischer Einflussnahme in Tiflis
Picha: Mikhail Yegikov/TASS/dpa/picture alliance

Mwandishi mmoja wa shirika la habari la Ufaransa AFP ameshuhudia makundi makubwa ya watu waliokuwa wamekusanyika nje ya majengo ya bunge katikati mwa mji mkuu Tblisi wakiwa wamebeba bendera za Umoja wa Ulaya na Georgia wakipinga kile walichokiita "sheria ya Urusi" nchini humo.

Mswada wa sheria hiyo uliidhinishwa na wabunge wiki hii uliposomwa bungeni kwa mara ya kwanza. Mswada huo iwapo utapitishwa na kuwa sheria, utahitaji vyombo vya habari na mashirika yasiyo ya kiserikali yanayopokea zaidi ya asilimia 20 ya ufadhili wao kutoka mataifa ya kigeni, kujiandikisha kama "mawakala wa ushawishi wa kigeni."

Waandamanaji Tbilisi baada ya kurushiwa mabomu ya kutoa machoziPicha: IRAKLI GEDENIDZE/REUTERS

Wabunge wazuiwa kuingia bungeni

Sheria hiyo itakuwa sawa na ile ya Urusi ambayo imekuwa ikitumiwa kufunga au kuyanyamazisha mashirika yanayoikosoa serikali. Wapinzani wanasema ni sheria ambayo itakuwa kama kigingi kwa nchi hiyo kujiunga na Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya Kujihami ya NATO katika miaka ijayo.

Viongozi wa maandamano hayo hapo Jumatano waliwataka waandamanaji wawazuie wabunge kurudi bungeni hadi pale mswada huo utakapoondolewa.

Marekani imeitaka Georgia kuwapa waandamanaji uhuru wa kuandamana ikisema inasimama na waandamanaji hao. Ned Price ni msemaji wa ikulu ya White House.

"Tunahofia kwamba kupitishwa kwa sheria hii kutakuwa na athari kwa kuwa hatutoweza tena kuwa mshirika wa kimkakati wa Georgia na watu wake kama tulivyotaka kwa miongo sasa," alisema Price.

Mswada huo ulikuwa unatarajiwa kujadiliwa leo bungeni ila vyombo vya habari nchini humo, vimeripoti kwamba mjadala huo umesimamishwa. Spika wa bunge la Georgia Shalva Papuashvili ametaka mswada huo uchunguzwe na Tume ya Vienna ya sheria ya katiba ya Baraza la Ulaya, ambayo ndiyo tume kuu ya haki za binadamu Ulaya.

Hofu ya Georgia kuchukua mwelekeo wa kidikteta

Rais wa Georgia Salome Zurabishvili, yeye amesema atautia saini mswada huo na kuufanya kuwa sheria na waliouandika wanasema ni sheria inayohitajika ili kuhakikisha kwamba kuna uwazi katika mashirika yanayopata ufadhili kutoka mataifa ya kigeni.

Rais wa Georgia Salome ZurabishviliPicha: Irakli Gedenidze/REUTERS

Kuna hofu nchini humo kwamba nchi hiyo ambayo ina malengo ya kujiunga na Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya Kujihami ya NATO inachukua mwelekeo wa kidikteta na kuelekezwa katika njia ya chama tawala.

Georgia ilikuwa sehemu ya Umoja wa Sovieti uliokuwa unaongozwa na Urusi na raia wengi wa nchi hiyo wanaiunga kmono Ukrainen katika vita inavyopigana na Urusi.

Wageorgia wengi wanaipinga Urusi kufuatia hatua yake ya kuyaunga mkono maeneo mawili nchini humo yaliyokuwa yanataka kujitenga. Sababu nyengine ni hatua ya Urusi kuivamia Georgia kwa muda mfupi mwaka 2008.

Chanzo: DPAE/Reuters

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW