1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hofu ya UNHCR kuhusu wakimbizi wa Eritrea nchini Ethiopia

15 Januari 2021

Mkuu wa shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR Fillipo Grandi amesema ana wasiwasi kuhusu hali ya kibinadamu inayowakumba wakimbizi wa Eritrea katika eneo la Kaskazini mwa Ethiopia

Schweiz Filippo Grandi Flüchtlingskommissar UN
Picha: Getty Images/AFP/F. Coffrini

Filippo Grandi amesema kuwa ana wasiwasi kuhusu usalama na hali ya wakimbikizi wa Eritrea katika kambi mbili za wakimbizi katika eneo la Tigray ambazo mashirika ya Umoja wa Mataifa yameshindwa kuzifikia kufuatilia mashambulizi ya kijeshi kutoka Ethiopia.

Grandi alipongeza hatua ya ruhusa ya kufikia kambi za Mai Aini na Adi Harush huku mashirika ya msaada yakiweza kusambaza chakula kwa baadhi ya wakimbizi elfu 25 wa Eritrea na kuanza kazi ya kutoa huduma za maji na afya.

Hata hivyo amesema kuwa licha ya maombi ya mara kwa mara,shirika la UNHCR pamoja na washirika wake hayajaweza kufikia kambi za wakimbizi za Shimelba na Hitsats tangu kuanza kwa operesheni ya kurejesha sheria na utulivu miezi miwili iliyopita. Grandi amesema ana wasiwasi kuhusu usalama na hali ya wakimbizi katika kambi hizo ambao hawajapata msaada wowote kwa muda wa wiki kadhaa sasa.

Kinachotia hofu zaidi

Ameongeza kuwa kile kinachotia wasiwasi zaidi ni kwamba anaendelea kupokea ripoti za kuaminika kuhusu hali ya ukosefu wa usalama inayoendelea na madai ya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu ikiwa ni pamoja na mauaji, utekaji nyara wa kulengwa na kurejeshwa kwa nguvu kwa wakimbizi wa Eritrea nchini mwao.

Mwezi uliopita Marekani ilitaja ripoti za uwepo wa jeshi la Eritrea katika eneo la Tigray kuwa za kuaminika na nzito. Balozi wa Ethiopia nchini humo Fitsum Arega akakanusha mara moja na kuzitaja ripoti hizo kuwa za uongo. Wakazi wa Tigray pia wamewashtumu wanajeshi wa Eritrea kwa dhulma na uporaji katika eneo hilo.

Sudan yapiga marufuku kupaa kwa ndege katika mpaka wa al-Fashaqa

Picha: Nariman El-Mofty/AP Photo/picture alliance

Mamlaka ya usafiri wa anga ya Sudan imetoa ilani ya kimataifa ya safari za anga na kusema ni marufuku kwa ndege kupaa katika eneo la mpaka la al-Fashaqa.

Afisa mmoja wa juu ameliambia shirika la habari la Ufaransa AFP kwamba uamuzi huo ulimaanisha ndege za kijeshi.

Hofu imekuwa ikitanda kati ya Sudan na Ethiopia kuhusiana na eneo la al-Fashaqa ambalo limekumbwa na mapigano katika wiki za hivi karibuni. Eneo hilo limekaliwa na wakulima wa Ethiopia wanaolima katika ardhi hiyo iliyo na rutuba inayodaiwa na Sudan. Siku ya Jumatano, Sudan ilisema kuwa ndege ya kijeshi ya Ethiopia ilipaa katika mpaka kati yake na Ethiopia katika eneo hilo na kuonya kuhusu athari kali.

Msemaji wa jeshi la Ethiopia Jenerali Mohamed Tessema ameliambia shirika la AFP kwamba hana habari zozote kuhusu madai hayo ya Sudan kuhusu ndege hiyo lakini hali katika eneo hilo la mpaka ilikuwa ya kawaida siku ya Jumatano. Sudan na Ethiopia zimekuwa zikilaumiana kuhusiana na ghasia katika eneo la al-Fashaqa tangu mwezi Desemba.

Wiki hii Ethiopia ilidai kuwa vikosi vya kijeshi vya Sudan vilikuwa vinaingia ndani zaidi katika eneo hilo la mpaka huku Sudan ikisema kuwa genge la Ethiopia liliwauwa takriban raia sita wa Sudan katika mpaka huo.

Chanzo: ap,reuters, afp