1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Hofu yazuka ya vita kamili kati ya Israel na Hezbollah

John Juma Rola Farhat, Cathrin Schaer
14 Juni 2024

Tayari takriban watu 150,000 wamefurushwa kutoka maeneo yanayozunguka mpaka wa nchi hizo mbili.

Lebanon I Mzozo kati ya israel na Hezbollah
Wanajeshi wa Israel na Wanamgambo wa Hezbollah wamekuwa wakirushiana makombora karibu kila siku kwa miezi kadhaa sasa.Picha: AFP

Hofu inazidi kuongezeka kuhusu uwezekano wa kutokea vita kamili kati ya wanamgambo wa Hezbollah wa Lebanon na Israeli.

Tangu shambulio lililofanywa na Hamas kusini mwa Israel mnamo Oktoba 7, 2023, ambalo liliua takriban watu 1,200, hali katika mpaka wa Israel na Lebanon imezidi kuwa ya wasiwasi.

Mapema mwezi Juni, mashirika ya kutetea haki za binadamu yaliripoti kuwa Israel ilirusha mabomu ya fosforasi kulenga miji ya Lebanon. Jambo ambalo ni ukiukaji wa sheria za kimataifa za kibinadamu.

Wakati huo huo, Hezbollah ilirusha zaidi ya maroketi 160 ndani ya Israel, ili kulipiza kisasi dhidi ya Israel kwa kuwaua makamanda wao wawili. 

Soma pia: Kundi la Hezbollah ladai kuishambulia Israel kwa roketi

Hali hii imezusha wasiwasi kwamba machafuko kwenye mpaka yanaweza kugeuka kuwa vita kamili.

Viongozi wa siasa kali Israel wataka Hezbollah kushambuliwa

Kutokana na mvutano huo uliopo kwenye mpaka, wanasiasa kadhaa wenye msimamo mkali wa Israel, tayari wamesema hadharani kwamba Israel inapaswa kushambulia Hezbollah.

Uchunguzi wa maoni wa hivi majuzi ulionyesha kuwa zaidi ya asilimia 60% ya raia wengi wa Israel wanakubaliana na msimamo huo.

Mfumo wa ulinzi wa israel 'Iron Dome ukirusha makombora ili kudungua yaliyorushwa kutoka upande wa Lebanon.Picha: Ayal Margolin/JINI/XinHua/picture alliance

Soma pia: Watu 37 wauawa Gaza katika shambulizi la Israel

Haijulikani ikiwa vita vikubwa zaidi vitazuka. Juhudi za sasa za kidiplomasia za kimataifa zinalenga kuzuia hilo.

Wataalam wengi wanahoji kuwa wakati Israel inapoendelea na operesheni zake za kijeshi huko Gaza, haitakuwa busara ya kimkakati kwake kufungua uwanja mwingine wa vita na Hezbollah.

Isitoshe, wanahoji kuwa Hezbollah, kundi ambalo nchi kadhaa ikiwemo Marekani na Ujerumani zimeliorodhesha kuwa kundi la kigaidi, lina uwezo, silaha na nguvu zaidi kuliko Hamas ambalo pia limeorodheshwa kuwa la kigaidi huko Gaza. 

Mzozo wa Israel na Hamasumeendelea kuwa pasua kichwa na changamoto kubwa katika Mashariki ya Kati.

Wakaazi wa mpakani waingiwa wasiwasi

Wakati wimbi la karibuni zaidi la mapigano kati ya Israel na kundi la wanamgambo wenye makao yake nchini Lebanon, Hezbollah, yalipoanza, Malak Daher, mwanamke kutoka Lebanon alitarajia lingedumu kwa siku chache tu.

Soma pia: Blinken ataka suluhisho la kidiplomasia kati ya Israel na Lebanon 

Lakini mapigano kati ya Hezbollah, na majeshi ya Israel bado hayajamalizika. Kwa hakika, katika wiki chache zilizopita, inaonekana kuwa yameongezeka.

Mamlaka ya Lebanon inasema kumekuwa na zaidi ya vifo 375 nchini humo tangu Oktoba 2023, wakiwemo raia 88, kutokana na mashambulizi ya Israel.

Jeshi la Israel kwa upande wake limesema wanajeshi wake 18 na raia 10 wameuawa kufuatia mashambulizi ya Hezbollah.

Soma pia: UN yaishtumu Israel kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu, Hamas kwa uhalifu wa kivita

Maelfu wakimbia mpaka wa Israel na Lebanon

Wakati huo huo, makumi ya maelfu ya raia, karibu 100,000 wa Lebanon na zaidi ya 60,000 Waisraeli, wanaoishi pande zote mbili za mpaka wamekimbia makazi yao kutokana na mapigano.

Daher, mwenye umri wa miaka 30, ambaye alihamishwa kutoka mji wa kusini wa Mais al-Jabal, ulioko karibu na mpaka wa Lebanon na Israel ambako mapigano yamejikita, amesema ni vigumu sana kuwa mbali na maisha yako, "unahisi kama maisha yako yamesimama.

Soma pia: Vikosi vya Israel bado vyaushambulia mji wa Rafah

Baada ya vita viwili vya 1996 na 2006 ambavyo havikumalizika, vikosi vya Israel na Hezbollah vimekuwa vikifanya mashambulizi ya ‘nipige nikupige' katika himaya ya kila upande, lakini bila ya kutokea vifo vingi.

Daher alinusurika katika vita vya mwaka 2006 kusini mwa Lebanon kati ya Israel na Hezbollah.

Lakini anapokadiria machafuko ya wakati huo na ya sasa, anaona ya 2006 kama si kitu, ikilinganishwa na mzozo wa sasa.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW