1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hofu ya vita yarejea Yemen kwa kushindwa kurefusha mkataba

3 Oktoba 2022

Mkataba wa kusitisha mapigano nchini Yemen ambao umedumu kwa miezi sita, umemalizika Jumapili huku juhudi za kuurefusha zikigonga mwamba.

Symbolbild Kämpfe im Jemen
Picha: AP Photo/picture alliance

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen, anahangaika kuyafufua makubaliano ya miezi sita ya kusitisha mapigano Yemen, ambayo muda wake ulimalizika Jumapili bila ya maelewano, hivyo kuibua wasiwasi wa kurejea kwa vita na kusababisha waasi kutoa vitisho dhidi ya Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu. 

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen, Hans Grundberg aliahidi kufanya juhudi kadha wa kadha kuyafufua mapatano hayo ambayo muda wake ulimalizika Jumapili. Tangu mapatano hayo yalipoanza kutekelezwa mwezi Aprili, kumekuwa na upungufu mkubwa wa mashambulizi.

Je,Yemen itaunda makubaliano mapya?

Waasi wa Kihouthi wanaoungwa mkono na Iran, wamekuwa wakipigana na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia, tangu 2015. Vita hivyo vimesababisha vifo vya mamia ya maelfu ya watu. Kulingana na Umoja wa Mataifa, vita hivyo pia vimesababisha mgogoro mbaya zaidi wa kibinadamu ulimwenguni.

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen Hans Grundberg.Picha: Fayez Nureldine/AFP

Mpango wa Grundberg kuyarefusha mapatano hayo kwa mara nyingine, ulipingwa na Wahuthi. Awali mapatano hayo yalipaswa kudumu kwa miezi miwili pekee kuanzia Aprili, lakini hadi Jumapili, yalikuwa yamerefushwa mara mbili.

Mpango huo mpya wa Grundberg, ulijumuisha kuwalipa mishahara wafanyakazi wa serikali, kufungua njia mpya kuingia mji wa Taez ambao umezuiwa na waasi, kuongeza idadi ya ndege za kibiashara zinazopaa kutoka mji mkuu wa Sanaa unaoshikiliwa na waasi, na kuruhusu meli zaidi za kusafirisha mafuta kuingia mji wa bandari wa Hodeida, ambao pia unadhibitiwa na Wahouthi.

Mjumbe Maalum wa Yemen ataka usitishwaji mapigano urefushwe

Aidha mpango huo ulipendekeza kuachiliwa kwa wafungwa, kurejesha mchakato jumuishi wa kisiasa kushughulikia masuala ya uchumi ikiwemo huduma za umma.

Lakini waasi hao wa Kihouthi kutoka kaskazini mwa nchi hiyo, ambao waliukamata mji mkuu Sanaa mwaka 2014 na ambao hadi sasa wanadhibiti maeneo makubwa ya nchi hiyo maskini zaidi katika rasi ya Arabia,  wamesema mpango mpya wa Grundberg, "haujashughulikia matakwa ya raia wa Yemen, na hauanzishi mchakato wa amani".

Kulingana na shirika la habari la Wahouthi nchini Yemen, Baraza kuu la kisiasa  limesema "watu wa Yemen hawatadanganywa na ahadi za uwongo". Baraza hilo limetaka mapato kutokana na raslimali za nchi hiyo ikiwemo mafuta na gesi.

Kulingana na Umoja wa Mataifa, vita hivyo pia vimesababisha mgogoro mbaya zaidi wa kibinadamu ulimwenguni.Picha: Abdulnasser Alseddik/AA/picture alliance

Pamoja na mapigano ya ardhini, uhasama kati ya pande husika umeshuhudia pia mashambulizi ya mabomu yanayofyatuliwa angani na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudia, na vilevile makombora yanayofyatuliwa na waasi dhidi ya vituo vya mafuta nchini Saudi Arabia na ndani ya Umoja wa falme za Kiarabu.

UN: Waasi wa Houthi kutowatumia tena watoto kama wanajeshi

Kupitia ujumbe kwenye ukurasa wake wa Twitter Jumapili usiku, msemaji wa kijeshi wa Wahouthi Yahya Saree alizitahadharisha kampuni za mafuta kutoka Saudi Arabai na kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) nchini Yemen, kufunga virago vyao na ziondoke.

Hakukuwa na jibu la moja kwa moja kuhusu hayo kutoka Riyadh au Abu Dhabi, lakini serikali ya Yemen inayotambuliwa kimataifa, ilisema kupitia ujumbe kwenye ukurasa wa Twitter wa ubalozi wake mjini Washington, ililihimiza Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa kushughulikia ipasavyo vitisho vya hivi karibuni vya Wahouthi, pamoja na kukataa kwao kukubali kurefushwa kwa makubaliano ya kusitisha vita.

Grundberg ambaye amekuwa akifanya ziara kati ya Sanaa na Oman katika juhudi zake za upatanishi amesema ataendelea kufanya kazi na pande zote mbili kujaribu kupata suluhisho.

(AFPE)

Tafsiri: John Juma

Mhariri: Jacob Safari

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW