1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hofu ya waislamu yaongezeka Marekani

Josephat Charo12 Mei 2005

Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na baraza la waislamu wa Marekani, visa vya mateso, ubaguzi na uhalifi dhidi ya waislamu viliongezeka sana nchini Marekani mwaka uliopita.

Baraza hilo linasema lilipokea ripoti za kuaminika 141 za mateso yaliyofanywa au yaliyopangwa kufanywa dhidi ya waislamu au misikiti nchini kote, idadi inayoonyesha kuongezeka kwa visa hivyo kwa asilimia 52.

Mwaka wa 2004 visa vya mateso vilivyofanywa na polisi au hujuma za utekelezwaji wa sheria kama vile waislamu kutiwa mbaroni pasipo sababu za maana, kuzuiliwa gerezani na misako isiyoisha, viliongezeka sana, na kujumulisha zaidi ya asilimia 25 ya kesi zote za ukiukaji wa haki na ubaguzi.

Kwa mujibu wa baraza hilo la waislamu wa Marekani, kesi hizo zilijumulisha asilimia 7 tu ya visa vyote vilivyoripotiwa mwaka wa 2003. Hata hivyo limesisitiza kwamba ripoti yake haiwezi kuorodheshwa kuwa ya kisayansi kwani ilitegemea sana habari zilizotolewa na watu binafsi ambao aidha waliathirika ua walishuhudia visa hivyo vya mateso.

Mkurugenzi wa baraza hilo anayeshughulikia maswala ya sheria, Arsalan Iftikhar, aliyeiandika ripoti hiyo ya kurasa 62, alisema idadi ya visa hivyo ni ya kushangaza, hususan ikizingatiwa kuna ongezeko la hofu juu wa dini y kiislamu na watu kukosa kuilewa dini hiyo na waislamu wote kwa jumla.

Takwimu za mwaka wa 2000 zinaonyesha watu milioni 1.2 walijitambulisha kama warabu nchini Marekani. Takwimu za waislamu zinatatanisha huku ikikadiriwa kwamba idadi yawaislamu nchini Marekani ni kati ya milioni tatu na milioni saba.

Mkurugenzi wa mawasiliano wa kamati ya kupambana na ubaguzi wa wamarekani walio na asili ya kiarabu, ADC, Laila al Qatani, amesema kuna idadi ya kubwa ya visa vya ubaguzi ikilinganishwa na miaka iliyopita. Kundi hilo huchunguza visa vya uhasama na ukiukaji wa haki za wamarekani alio na asili ya kiarabu na linataraji kutoa ripoti yake mwishoni mwa mwaka huu.

Makundi yote mawili yamesema kuongezka kwa takwimu hizo ni kufuatia utayarifu wa waathiriwa pamoja na jamii zao kuripoti kuhusu visa vya mateso, ikilinganishwa na muda mfupi baada ya mashambulio ya kigaidi ya Septemba 11 dhidi ya Marekani. Uvamizi dhidi ya waislamu na waarabu uliongezeka na serikali ya Marekani ikawakamata mamia ya wahamiaji waislamu waliotuhumiwa kuhusika na mashambulio hayo.

Mkurugenzi wa mawasilano wa baraza la waislamu, Ibrahim Hooper, amependekeza kuwa hatua ya shirika la ujasusi la Marekani, FBI, kuzishughulikia ripoti za uhalifu wa chuki dhidi ya waislamu wa Marekani, kumewahimiza waathiriwa kujitokeza na kusema ukweli. Hata hivyo ripoti hiyo inalitaka shirika la FBI kuongeza juhudi zake badala ya kutegemea sana ripoti za makundi mengine.

Mbali na hayo ripoti hiyo inalaumu kuongezeka kwa hali ya hofu inayoelekezwa kwa jamii ya waislamu, warabu na raia wa Asia Kusini, baada ya matukio ya Septemba 11. Hooper amesema asilimia 99 ya waandishi habari na watangazaji wanafanya kila juhudi kuiondoa hofu hii, lakini kuna idadi ndogo ya waandishi ambao wameifanya kazi yao kubwa kuitenga jamii ya waislamu.

Mkurugenzi mtendaji wa baraza la waislamu, Nihad Awad, amesisitiza hofu hiyo bado ni tatizo kubwa sana na kumtaka rais George W Bush, ambaye amesifiwa sana kwa msimamo wake juu ya waislamu, azungumzie tena juu ya haki za waislamu, ili Marekani iweze kuaminiwa katika ulimwengu wa waislamu. Awad amesema waislamu wa Marekani ni daraja inayoweza kutumiwa kupunguza tofauti zilizopo kati ya wamarekani na waislamu ulimwenguni kote.

Huku visa vya chuki dhidi ya waislamu na mateso ya polisi vikiwa vimeongezeka mwaka wa 2004, baraza la waislamu linasema lilipokea ripoti chache kuhusu ubaguzi katika sehemu za kazi na katika maafisi ya serikali, ikilinganishwa na mwaka jana. Kulikuwa pia na idadi ndogo ya visa vya mateso ya waislamu katika mtandao wa internet.

Mfano wa visa vya matesi dhidi ya waislamu ni kesi ya James Yee, mwanajeshi mwenye asili ya kimarekani aliyesilimu na kuwa muislamu mwaka wa 1990. Alitiwa mbaroni mwaka wa 2003 na kuzuiliwa kwa tuhuma za kufanya upelelezi kwa niaba y a kundi la kigaidi la al-Qaeda, wakati alipokuwa akifanya kazi katika jelöa ya Guantanamo Bay nchini Cuba.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW