1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hofu yaongezeka Darfur baada ya kambi za UNAMID kuporwa

2 Julai 2021

Kikosi cha kulinda amani katika jimbo la Sudan linalokumbwa na machafuko, Darfur, hatimaye kimemaliza kuwaondoa wanajeshi wake kutoka eneo hilo.

Sudan West Darfur | Rauchwolken im Abu Zar Camp
Picha: AP/picture alliance

Hofu ya machafuko kurejea zaidi imetanda hasa baada ya waporaji kuharibu zilizokuwa kambi za kikosi hicho cha kulinda amani.

Darfur, eneo kubwa ambalo ni kame, maskini na ambalo limejaa bunduki magharibi mwa Sudan, bado linakumbwa na mzozo mbaya ulioanza mwaka 2003, chini ya kiongozi wa kimabavu ambaye pia ni rais wa zamani wa nchi hiyo, Omar al Bashir. Mzozo huo ulisababisha vifo vya mamia kwa maelfu ya watu.

Soma kuhusu: Kesi ya uhalifu wa kivita Darfur yaanza kusikilizwa ICC

Mkaazi mmoja wa jimbo hilo Ahmed Awad aliyeshudia tukio hilo la mwezi Machi, amesema waporaji walivamia kambi moja iliyoko katika kijiji cha Menwashie, ikiwa ni kilomita 65 kaskazini mwa mji mkuu wa kusini mwa Darfur, Nyala, amesema kila kitu katika kambi hiyo kiliporwa kwa muda wa saa chache.

Kikosi cha UNAMID kilidumu eneo la Darfur kwa miaka 13.Picha: AFP via Getty Images

Mnamo Januari, ujumbe wa pamoja wa kulinda amani kutoka Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika katika jimbo la Darfur (UNAMID), uliamua kuondoa wanajeshi wake wa kulinda amani katika awamu mbalimbali, licha usalama wa eneo hilo ukiwa bado katika hali tete.

Soma pia : Vita vya kikabila huko Darfur vyazusha hofu kubwa

Hali tete ya siasa na uchumi Sudan

Isitoshe uamuzi na utekelezwaji wa hatua hiyo ulijiri mnamo wakati Sudan ikikumbwa na hali ngumu ya mpito wa kisiasa, pamoja na ugumu wa kiuchumi.

Kwa wengi, ujumbe wa UNAMID ambao ndio ulikuwa mkubwa zaidi ulimwenguni wa kulinda amani wenye jumla ya wanajeshi 16,000, ulikuwa kikosi cha kuzuia machafuko japo walishinda kuzuia mashambulizi kadhaa.

Ujumbe huo ulianzishwa kama sehemu ya juhudi za kumaliza vita vilivyoanza baada ya waasi wa kabila la wachache kulalamika kuhusu ubaguzi, na kuanza mashambulizi dhidi ya serikali ya Omar al-Bashir iliyotawaliwa na Waarabu.

KIkosi cha UNAMID kilijumuisha jumla ya wanajeshi 16,000 wa kulinda amani kutoka Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.Picha: UN Photo/Albert Gonzales Farran

Kulingana na Umoja wa Mataifa, vita hivyo vilisababisha vifo vya takriban watu 300,000 na watu milioni 2.5 walipoteza makao yao.

Lakini baada ya Omar al-Bashiri kupinduliwa Aprili 2019 na serikali ya mpito kubuniwa Khartoum na vilevile mkataba wa amani kusainiwa kati ya makundi makuu ya waasi, muda wa ujumbe wa UNAMID ambao ulishadumu kwa miaka 13 ulikamilika Disemba 31.

Kinachotia wasiwasi ni kwamba muda mfupi tu baada ya ujumbe huo kumaliza hatamu yake, mamia ya watu waliuawa kufuatia makabiliano kati ya makundi pinzani katika baadhi ya maeneo ya Darfur. Miongoni mwa vyanzo vya mizozo baina ya jamii katika eneo hilo ikiwa ni ardhi na maji.

 Waporaji waiba mamilioni ya dola

Waporaji kutoka Darfur wamekuwa wakivamia kambi za UNAMID na kuiba mamilioni ya dola pamoja na vitu vingine vya thamani mathalan runinga na mitambo ya nishati kama majenereta.

Awad amesema kwamba serikali ya Sudan haikuonyesha kujitolea kuzilinda kambi hizo.

Mnamo Juni 30, ujumbe wa UNAMID ulitangaza kwamba umewaondoa walinda amani wake wote. Ujumbe huo ulitumai kwamba kambi zake 14 ambazo ulizikabidhi serikali ya Sudan, zitatumiwa kwa manufaa ya jamii kwa muda mrefu.

Walinda amani wa UNAMID wakishika doria Darfur Sudan. (Picha ya maktaba, Disemba 31, 2020)Picha: AFP

Vituo vinne vilivyoachwa na UNAMID vimeharibiwa

Lakini badala yake, kambi nane tayari zimeharibiwa na kuporwa na watu wasiojulikana. Hayo ni kulingana na Umoja wa Mataifa. Wakaazi wa Darfur wanasema serikali ya mpito ya Sudan ilishindwa kutimiza ahadi zake.

Moussa Ibrahim ambaye ni kiongozi wa jamii eneo la Khor Abeche amesema maafisa wa serikali waliahidi kulinda moja ya kambi ya walinda usalama kijijini mwake lakini wakashindwa.

Mwandishi na mchambuzi kutoka Darfur, Abdallah Khater, alidai matukio ya baada ya UNAMID kuondoka ni ukosefu wa uhamasishaji wa jamii pamoja hali ya serikali kutokuwa imara.

Mwanachama mmoja wa kamati iliyosimamia kuondoka kwa ujumbe wa UNAMID amekiri kwamba serikali ilikosa pesa kuweza kuwapeleka maafisa zaidi wa usalama jimbo la Darfur baada ya UNAMID kutoka.

(AFPE)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW