1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroSudan

Hofu yaongezeka Sudan baada ya RSF kuuteka mji wa El Fasher

29 Oktoba 2025

Hofu imeongezeka nchini Sudan siku kadhaa baada ya wanamgambo wa RSF kuuteka mji muhimu wa El-Fasher huko Darfur, huku kukiwa na ripoti za vitendo vya ukatili, mauaji na ukiukwaji mkubwa wa haki za binaadamu.

Sudan | Wapiganaji wa RSF wakishangilia kuchukua udhibiti wa mji wa El-Fasher
Wapiganaji wa kundi la RSF wakishangilia kuchukua udhibiti wa mji wa El-FasherPicha: Rapid Support Forces (RSF)/AFP

Kutekwa kwa mji wa  El-Fasher  kumezua hofu ya kushuhudia eneo hilo likikumbwa tena na mauaji makubwa ya kikabila kufuatia hatua ya wapiganaji wa RSF kuuzingira mji huo kwa miezi 18 chini ya mashambulizi makali na kusababisha njaa. Hofu hiyo imetokana na kwamba chimbuko la waasi wa RSF ni wanamgambo wa Janjaweed ambao tayari waliwahi kushutumiwa kwa mauaji ya kimbari karibu miongo miwili iliyopita.

Wasiwasi pia unashuhudiwa katika maeneo jirani na Darfur ambapo katika jimbo la Kordofan Kaskazini, Shirikisho la Kimataifa la Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu limesema wafanyakazi wake watano wameuawa huko Bara na kwamba wengine watatu hawajulikani walipo tangu wanamgambo wa RSF kuchukua udhibiti wa mji wa El-Fasher siku ya Jumamosi. Umoja wa Ulaya siku ya Jumatano ulilaani kile ulichosema ni "ukatili" wa kundi la RSF.

Aidha,  Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP)  limesema leo Jumatano kwamba wawakilishi wake wawili nchini Sudan wameamriwa kuondoka nchini humo ndani ya saa 72 bila hata hivyo kupewa sababu zozote za uamuzi huo. Waliofukuzwa ni mkurugenzi wa WFP nchini humo Laurent Bukera, pamoja na mratibu wake wa masuala ya dharura Samantha Chattaraj.

Hofu ya Sudan kugawanyika

Wanawake wa Sudan waliokimbia mapigano huko El-Fasher wakiwasili katika mji wa Tawila: 28.10.2025Picha: AFP/Getty Images

Wachambuzi wanaelezea pia hofu ya kushuhudia mgawanyiko wa kudumu nchini Sudan kwa kuwa na tawala mbili ambapo wanamgambo wa RSF wataongoza eneo la Darfur huku jeshi likidhibiti maeneo ya katikati mwa nchi, kaskazini na mashariki.

Siku ya Jumanne, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alitoa wito wa kufanyika mazungumzo ya haraka ya kusitisha mapigano nchini  Sudan  na kuzitaka pande zote mbili kuchukua hatua za haraka ili kupata makubaliano ya amani katika mgogoro unaotajwa kuwa mkubwa zaidi wa kibinadamu duniani kwa sasa. Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric ametoa wito wa kuwalinda raia:

"Sisi na washirika wetu wa kibinadamu tunahimiza jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua za haraka ili kuwalinda raia na wafanyakazi wa mashirika ya kibinadamu nchini Sudan ili kuhakikisha njia salama na ufikiaji wa kibinadamu kwa watu walionaswa huko el-Fasher, pamoja na kuongeza ufadhili wa kusaidia shughuli za kibinadamu katika mji huo na kwingineko nchini Sudan," alisema Dujarric.

Guterres  alilaani ukiukaji wa sheria za kimataifa za kibinadamu na alielezea wasiwasi wake mkubwa kutokana na ongezeko la silaha na wapiganaji wanaoingia Sudan, jambo alilosema linazidisha hali ambayo tayari ni mbaya mno.

// AP/AFP/DPA

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW