1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hofu yatanda kufuatia mlipuko mpya wa homa ya nyani

8 Agosti 2024

Miaka miwili baada mlipuko wa ugonjwa wa homa ya nyani (mpox), hofu imetanda kwamba ugonjwa huo uliogunduliwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, na sasa unaweza kuenea zaidi nchi jirani.

Kirusi kinachosababisha homa ya nyani (mpox)
Kirusi kinachosababisha homa ya nyani (mpox) Picha: Isai Hernandez/imago images

Kituo cha Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa CDC barani Afrika kimerekodi visa 14,479 vilivyothibitishwa na kushukiwa vya aina mpya ya ugonjwa huo wa mpox pamoja vifo 455 nchini Kongo kufikia Agosti 3, hii ikiwakilisha kiwango cha takriban asilimia 3 ya vifo.

Lakini watafiti katika taifa hilo, wanasema kiwango cha vifo kutokana na ugonjwa huo kinaweza kuwa asilimia 10 miongoni mwa watoto.

Louis Albert Massing, mratibu wa matibabu wa shirika la Madaktari Wasio na Mipaka nchini Kongo, amesema mwezi uliopita, serikali ya Kongo ilithibitisha ongezeko kubwa la maambukizi ya ugonjwa huo na kwamba umegunduliwa katika kambi za wakimbizi karibu na Goma huko Kivu Kaskazini ambapo msongamano mkubwa wa watu hufanya hali kuwa mbaya mno.

Massing ameongeza kuwa athari ya kuongezeka kwa maambukizi hayo ni ya wazi kutokana na idadi kubwa ya watu katika eneo hilo lenye migogoro linalopakana na mataifa kadhaa.

Wasiwasi watokana na kusambaa kwa aina mpya ya kirusi cha Mpox

Chanjo ya mpox ipo lakini aina mpya za virusi vinatishia ufanisi. Picha: Sven Hoppe/dpa/picture alliance

Rosamund Lewis, kiongozi wa kiufundi kuhusu ugonjwa wa mpox katika shirika la Afya duniani WHO, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba tayari kirusi kipya aina ya Clade Ib cha ugonjwa huo kimeenea kuvuka mipaka ya kitaifa. Katika muda wa wiki mbili zilizopita, visa vya ugonjwa huo vimeripotiwa nchini Uganda, Burundi, Rwanda na Kenya.

Mamlaka katika nchi hizo nne zimethibitisha kuhusu visa hivyo vya mpox. Burundi haswa imeripoti visa 127 bila kutaja aina ya kirusi husika.

Lewis, anasema hii ni mara ya kwanza kwa mataifa hayo yalioko mashariki mwa Kongo kuripoti visa vya ugonjwa wa mpox.

Lewis ameongeza kuwa Rwanda, Burundi, Uganda ni mataifa ambayo kwa kawaida hayana ugonjwa huo , hii ikimaanisha kuwa ni kuenea kwa mlipuko wa ugonjwa huo unaoikumba Kongo na Afrika ya Kati kwa ujumla.

Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) yenye nchi wanachama nane imezitaka serikali kutoa elimu kwa wananchi wao jinsi ya kujikinga na kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo.

Vifo vyaripotiwa mataifa kadhaa ya Afrika ya Kati na Magharibi 

Kituo cha CDC Afrika, pia kimeripoti visa 35 vilivyothibitishwa na kushukiwa vya ugonjwa huo, ikiwa ni pamoja na vifo viwili nchini Cameroon, visa 146, ikiwa ni pamoja na kifo kimoja nchini Congo Brazzaville, na visa  227 katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, 24 nchini Nigeria, tano nchini Liberia  na visa vinne nchini Ghana.

Huko Afrika Magharibi, hivi karibuni, Ivory Coast iliripoti visa sita vilivyothibitishwa ambavyo havikuwa vya kuhatarisha, vitano katika mji mkuu wa kiuchumi wa Abidjan, bila kutaja aina ya kirusi cha ugonjwa huo.

Mpox iligunduliwa kwa mara ya kwanza kwa binadamu mnamo mwaka 1970 nchini Kongo wakati huo ikiitwa Zaire.

Miongoni mwa dalili ni kutoka vipele na malengelenge.Picha: Arlette Bashizi /REUTERS

Tangu wakati huo, ugonjwa huo umejikita hasa katika baadhi ya mataifa ya Afrika Magharibi na Kati. Wanadamu hupata maambukizi zaidi kutoka kwa wanyama walioambukizwa, kama vile wakati wa kula nyama ya porini.

Mnamo mwezi Mei mwaka 2022, maambukizo ya mpox yaliongezeka ulimwenguni kote, na kuwaathiri zaidi mashoga.

Mlipuko huo ulisababishwa na aina mpya ya kirusi kilichojulikana kama Clade II, ambacho kilichukuwa nafasi ya Clade I.

Takriban watu 140 walikufa miongoni mwa watu 90,000 walioambukizwa katika nchi 111.

Lewis anasema mlipuko huo bado unaendelea ikiwa ni pamoja na nchini Afrika Kusini, ambayo imeshuhudia visa 24, vitatu vilivyokuwa vibaya zaidi lakini akaongeza kuwa ulithibitiwa na kuenea kwa kiwango kidogo.

Mapema mwezi Julai, mkuu wa Shirika la Afya Duniani, WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus, alisema ugonjwa wa mpox bado ni tishio la afya duniani.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW