1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hofu yatanda Tigray kufuatia uwepo wa vikosi vya Ethiopia

18 Februari 2026

Hali ya wasiwasi imetanda kwenye jimbo la Tigray nchini Ethiopia, ripoti zikionesha kwamba wanajeshi wa Ethiopia wamejikusanya kwenye mpaka kati ya Ethiopia na Eritrea karibu na jimbo la Tigray Kaskazini mwa Ethiopia.

Wanajeshi wa Jeshi la Ulinzi la Taifa la Ethiopia (ENDF)
Wanajeshi wa jeshi la Ethiopia mwaka 2021 Picha: AMANUEL SILESHI/AFP/Getty Images

Kujipanga kwa vikosi vya wanajeshi kwenye mpaka kati ya Ethiopia na Eritrea katika jimbo la Kaskazini mwa Tigray kunatishia kuzuka kwa vita vingine kati nchi hizo mbili. Hii ni kwa mujibu wa vyanzo vya kidiplomasia vya mataifa ya Magharibi.

Kwa upande wao pia wapiganaji wa Tigray wanajipanga kuelekea mpaka huo hali ambayo inadhihirisha kuwa kuna uwezekano wa kuvunjwa kwa mkataba wa amani uliopelekea kumalizika kwa vita vilivyodumu kati ya mwaka 20220 na mwaka 2022.

Vita vya Tigray vya miaka hiyo miwili ambavyo vilihusisha hata majeshi ya Eritrea vilisababisha vifo vya zaidi ya watu laki sita. Hii ni kwa mujibu wa takwimu za makadirio za Umoja wa Afrika.

Duru za Kidiplomasia

Kulingana na vyanzo vya kidiplomasia idadi kubwa ya majeshi kujipanga kwenye eneo hilo la mpaka wa nchi hizo mbili ni ishara kwamba vita vinafukuta. Vyanzo vingine miongoni mwa raia wa eneo hilo ambavyo viliomba kutotambulishwa vimetoa kilio kwa jamii ya kimataifa kuweka shinikizo kwa pande zote katika mgogoro huo kuachana na vita na badala yake wafanye mazungumzo ya amani. Mchambuzi wa masuala ya sheria na siasa Mustafa Abdu kutoka Mekelle ameelezea kuwa mazingira hayo yanatia hofu.

Mpiganaji wa Kikosi cha Ukombozi wa Watu wa Tigray (TPLF) katika kituo cha ulinzi nje kidogo ya mji wa Hawzen, ambao wakati huo ulikuwa ukidhibitiwa na kundi hilo lakini baadaye ukachukuliwa tena na vikosi vya serikali, katika eneo la Tigray kaskazini mwa Ethiopia.Picha: Ben Curtis/AP/picture alliance

"Hali hii inatia hofu ambapo majeshi ya Ethiopia yamejipanga kwenye mipaka yote na kuna kila dalili kwamba vita vitatokea. Kulingana na makubaliano yaliyosainiwa Pretoria Afrika Kusini serikali ina jukumu ya kulinda mipaka lakini hali ilivyo ni kwamba hii inazusha vita.” 

Mahusiano kati ya Ethiopia na Eritrea yameshuhudiwa yakizorota tangu walipojikuta wakikabiliana katika vita hivyo dhidi ya waasi wa Tigray. Kwa sasa utawala wa Ethiopia unaikosoa Eritrea kwa kutoa silaha kwa waasi hao, madai ambayo Eritrea inayakanusha vikali.

Mwenyekiti wa shirikisho linalopigania demokrasi Tigray Amdom Gebreselassie amesema uwepo mkubwa wa majeshi ya wapiganaji wa Tigray  katika eneo hilo ambao baadhi wamevalia mavazi ya kiraia unazidisha mashaka ya mapigano kutokea wakati wowote.

TPLF yafanya ujasusi kuhusu ripoti hizo

Wapiganaji wa chama cha ukombozi wa watu wa Tigray TPLF wamo katika eneo hilo na wamepenyeza katika sehemu kadhaa wakionekana kufanya ujasusi Kwa hiyo kuna hatari ya vita kuzuka.

Wiki iliyopita Kamishna mkuu wa shiriki la Umoja Mataifa la haki za binadamu Volker Turk alitoa mwito kwa pande zote husika katika mzozo huo kutuliza hali hiyo. Eritrea ilipata uhuru wake mwaka 1993 kutoka kwa Ethiopia baada ya mapigano yaliyodumu mwongo mmoja. Baadaye kati ya mwaka 1998 na 2000 mataifa hayo mawili ya pembe la Afrika yalipigana tena na kusababisha vifo vya maelfu ya watu.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW