1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hollande afanya ziara ya kwanza Ujerumani

16 Mei 2012

Rais mpya wa Ufaransa, Francois Hollande amefanya ziara yake ya kwanza hapa Ujerumani ambapo alikutana na Kansela Angela Merkel. Masharti ya mkataba wa kubana matumizi ni moja ya mada zilizozungumziwa na viongozi hao.

Angela Merkel na Francois Hollande
Angela Merkel na Francois HollandePicha: Reuters

Hali mbaya ya hewa nusura ingezuia safari ya kwanza ya nje ya nchi ya rais mpya wa Ufaransa, Francois Hollande. Ndege aliyokuwa ameipanda akielekea Ujerumani ilipigwa na radi, na hivyo ilibidi igeuze njia na kurejea Paris, mji mkuu wa Ufaransa, kwa sababu za kiusalama. Hollande, mwenye umri wa miaka 57, alipanda ndege nyingine na hatimaye akawasili katika mji mkuu wa Ujerumani, Berlin, akiwa amechelewa kwa saa moja na nusu.

Kansela Merkel anafahamu kwamba ni lazima ajenge mahusiano mazuri na ya karibu na rais Hollande. Lakini hii itakuwa kazi ngumu kwa sababu ya tofauti za kisiasa walizonazo viongozi hawa wawili.

Kama ilivyo ada kwa mapokezi ya viongozi wa mataifa mengine, Merkel alimkaribisha mgeni wake mbele ya ofisi ya Kansela. Zulia jekundu lilitandikwa kwa ajili ya Hollande na kikosi cha heshima cha jeshi la Ujerumani pia kilikuwepo. Merkel alimsalimia Hollande kwa kumpa mkono na si kwa kumbusu shavuni kama ilivyokuwa kwa rais wa zamani wa Ufaransa, Nicholas Sarkozy. Kansela wa Ujerumani alikuwa na mengi ya kuzungumza na Hollande. Mazungumzo yao yalichukua muda wa masaa mawili. Baadaye Merkel aliwaeleza waandishi wa habari kwamba yeye na Hollande walijadili juu ya umuhimu wa uhusiano baina ya nchi yake na Ufaransa.

Merkel na Hollande wakikagua gwaride la heshimaPicha: Reuters

Hollande na Merkel waahidi kuisaidia Ugiriki

Ni dhahiri kabisa kwamba wanasiasa hawa wawili wako tofauti kabisa. Hollande alieleza kuwa yeye angependa kujadili tena kuhusu mkataba wa kubana matumizi wa nchi zinazotumia sarafu ya Euro. Rais huyo aliongezea kwamba angependa kuona pakiwepo na ukuaji halisi wa kiuchumi, na hivyo pendekezo lake ni kwamba pawe na mkataba utakaoratibu shughuli zinazowezesha ukuaji wa kiuchumi.

Lakini, kwa upande wake, Kansela Merkel aliweka wazi kwamba hayuko tayari kujadili tena juu ya mkataba wa kubana matumizi na kuhusu wazo la kuandaa mkataba juu ya ukuaji wa kiuchumi, Merkel alisema: "Ukuaji ni neno lenye maana pana, ukuaji lazima uwafikie raia. Kwa sababu hiyo ninafurahi kwamba tumekubaliana kuwa tutazungumza juu ya njia  mbali mbali zinazoweza kutumika kuleta ukuaji. Ninaamini kwamba tutakuwa na mawazo yanayowiana, lakini katika jambo moja au jingine tutakuwa na mawazo tofauti. "

Lakini katika suala la Ugiriki, Merkel na Hollande wana mtazamo sawa. Wote wawili walieleza kwamba wanatamani nchi hiyo ibakie katika ukanda wa sarafu ya Euro. Viongozi hao waliahidi kufanya kila liwezekanalo kuunyanyua uchumi wa Ugiriki.

Mwandishi: Sabine Kinkartz

Tafsiri: Elizabeth Shoo

Mhariri: Othman Miraji