Hollande aishutumu DRC
14 Oktoba 2012Ni viongozi 15 tu wa shirikisho la mataifa yanayozungumza Kifaransa , Francophonie, lenye wanachama 75 wamehudhuria mkutano huo unaofanyika katika jengo la bunge mjini Kinshasa pamoja na mwenyeji wa mkutano huo , rais wa Kongo, Joseph Kabila. Hollande , ambaye ameikasirisha jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo kwa kusema hali ya haki za binadamu nchini humo haikubaliki, amerudia tena usemi wake huo katika mazungumzo ya ana kwa ana na ya uwazi , pamoja na rais Kabila muda mfupi kabla ya mkutano huo kuanza.
Akizungumza baada ya mikutano mingine na wawakilishi wa upande wa upinzani na asasi zisizokuwa za kiserikali, Hollande amesema: "Francophonie sio tu lugha ya Kifaransa," na kuongeza kuwa "kuzungumza Kifaransa pia kuna maana ya kuzungumzia juu ya haki za binadamu, kwasababu haki ya mtu imeandikwa kwa Kifaransa, " akimaanisha mkataba wa umoja wa mataifa juu ya haki za binadamu, ulioandikwa na wanamapinduzi wa Kifaransa.Kiongozi huyo wa Ufaransa pia alikutana na kiongozi wa upinzani Etienne Tshisekedi.
Mada muhimu mashariki ya DRC
Uasi wa matumizi wa nguvu na mizozo ya kikabila inayolikumba eneo la mashariki ya jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo inatarajiwa kuwa mada muhimu katika mkutano huo. Hali nchini Mali pia itakuwa mada muhimu, ambako wanamgambo wa Kiislamu wenye msimamo mkali wamechukua udhibiti wa eneo la kaskazini mwa Mali.
Hollande amekanusha madai yaliyotolewa na kiongozi wa kundi moja la wapiganaji kuwa uungaji wake mkono wa kuingilia kati kijeshi dhidi ya Waislamu wenye itikadi kali wanaodhibiti eneo la kaskazini ya Mali , umeweka maisha ya raia wa Ufaransa waliotekwa nyara katika hatari. Oumar Ould Hamaha, kiongozi wa moja ya makundi ya waasi wenye mafungamano na kundi la al-Qaeda katika eneo la Maghreb (AQIM), amesema Hollande pia ameweka maisha yake binafsi katika hatari.
Maisha ya mateka hatarini
"Maisha ya mateka raia wa Ufaransa hivi sasa yamo katika hatari kwasababu ya matamshi ya rais wa ufaransa ambaye anataka kupigana vita dhidi yetu, " amesema Hamaha, kutoka kundi la harakati za umoja na jihad katika Afrika magharibi (MUJAO)."Maisha yake binafsi pia yamo hatarini. Anapaswa kufahamu hilo," aliongeza.
AQIM kwa hivi sasa inawashikilia mateka tisa kutoka mataifa ya Ulaya katika eneo la Sahel, sita kati yao ni Wafaransa. Hollande amekanusha matamshi hayo, wakati akiwa mjini Kinshasa. "Ni kutokana na kuonyesha nia halisi katika kusisitiza sera zetu, ambazo ni kupambana na ugaidi, ambapo tunaweza kuwashawishi wateka nyara kwamba umefika wakati wa kuwaachia huru ," amewaambia waandishi habari.
Kabila alikaribishwa kwa shangwe kubwa wakati mkutano huo ukifunguliwa. Kwingineko mjini Kinshasa hata hivyo, polisi walitumia mabomu ya kutoa machozi dhidi ya waandamanaji kadha wanaoipinga serikali , ambao walikuwa wakitupa mawe na ambao walikaidi amri ya kutofanya maandamano. Wanadai kuwa kuchaguliwa tena kwa rais Kabila katika mwaka 2011 kulihusika mno na udanganyifu.
Kabila amezungumzia kuhusu vita ambavyo ni kinyume na sheria , vinavyofanywa na watu kutoka nje katika eneo la mashariki ya nchi hiyo.
"Wakati watu wetu wanachukua juhudi zote kuendeleza maisha yao, makundi fulani yenye maslahi kutoka nje yamekuwa kwa miezi kadha yakifanyakazi kuidhoofisha nchi yetu katika jimbo la Kivu ya kaskazini, katika mpaka wa mashariki na Rwanda," Kabila amesema katika mkutano huo.
Hakuitaja Rwanda kwa jina , nchi ambayo imeshutumiwa kwa kuwaunga mkono waasi katika eneo hilo, dai ambalo lilisababisha kuletwa kwa wachunguzi wa umoja wa mataifa . Rwanda inakana madai hayo, na rais wa Rwanda Paul Kagame hakuhudhuria mkutano huo.
Mwandishi :Sekione Kitojo
Mhariri : Iddi Ismail Ssessanga