Hollande, Merkel, Misri magazetini
15 Januari 2014Juu ya mpango wa kufufua uchumi wa rais wa Ufaransa Francois Hollande, mhariri wa gazeti la Tagesspiegel anasema:
Ni danadana ya kisiasa pale rais Hollande anapoanza kujitetetea wakati huu. Hali mbaya imekuwa nzito kama risasi nchini mwake. Kila siku habari ni juu ya kufilisika kwa makampuni na ukosefu wa ajira. Kwamba katika mwaka huu mpya ataweza kubadili chochote kuhusu hali mbaya ya kiuchumi ni jambo ambalo wafaransa wengi wana mashaka nalo. Hollande alikuwa sahihi kuchukuwa mkondo wa tahadhari wa kisoshalisti na kiliberali ambao unayawezesha makampuni kukua. Lakini ikiwa hili litatoa hisia kuwa ikulu ya Elysee inajishughulisha na kumhami Hollande kuliko ukuaji wa dhati wa uchumi, basi anguko la mwisho la Hollande linaweza kuwa karibu.
Lakini maoni ya mhariri wa gazeti la Handelsblatt yamejikita katika madai yaliyotolewa na jarida moja la Ufaransa kuwa rais huyo alikuwa na uhusiano wa siri na muingizaji wa kike, jambo ambalo limempelekea mwandani wake kulazwa hospitalini. Mhariri huyo anasema:
Kwa miaka 30 Hollande amekuwa katika siasa, na tangu mwezi Mei mwaka 2012 anaishi katika ikulu ya Elysee. Muda huo ulikuwa unamtosha kabisaa kujibadili kutoka kuwa mtu msiri na kuwa kiongozi mwenye kudhamiria. Huwezi kumpata mtu kama Gerhard Schröder kutoka Francois Hollande. Maamuzi yayiso pendeza siyo nguvu ya Hollande. Msoshalisti huyo pia siyo mtu mwenye bahati. Kubainika kwa uhusiano wake wa siri na muigizaji Julie Gayet kumezidi kushusha umaarufu wake wakati huu muhimu.
Wahariri wa magazeti ya Wetzlarer Neue Zeitung, Mittelbayerishe, na Straubinger Tagblatt wametoa maoni kuhusiana na mkataba wa kutopelelezana baina ya Marekani na Ujerumani na ziara ijayo ya Kansela Angela Merkel katika ikulu ya White House. Juu ya mada hii, mhariri wa gazeti la Straubinger Tagblatt anasema.
Bila shaka Ujerumani imetia chumvi msimamo wake. Badala ya kulikabili taifa kubwa zaidi kiuchumi duniani kupitia mfumo wa Umoja wa Ulaya na kufanya kazi pamoja kulinda uhuru wa raia wake, serikali ya Ujerumani iliangalia tu maslahi yake, na kwa hatua yake hiyo imeshindwa. Hakuna uwezekano kwamba wakati wa ziara yake ijayo nchini Marekani, Kansela Angela Merkel ataweza kubadilisha mawazo ya Obama na kuweka wazi kwake kwamba kuchunguzana baina ya marafiki ni jambo lisilokubalika.
Kwa upande wake, mhariri wa gazeti la Cellesche Zeitung anatoa maoni juu ya kura ya maoni nchini Misri kwa kusema.
Iddi: Jeshi la Misri linakosa uhalali wa kidemokrasia, na hata kura hii ya maoni haitato uhalali huo hata kama raia wengi watajitokeza kuunga mkono rasimu ya katiba. Kitachorudisha uhalali huo ni uchaguzi ulio huru na wa haki, na hilo litategemea namna ulivyoendeshwa na wagombea wa aina gani watapambanishwa na Jenerali Abdel Fattah al-Sissi ikiwa ataamua kugombea nafasi ya urais.
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga
Mhariri: Mohammed Khelef