1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hong Kong inashikilia wahalifu wakahukumiwe China bara

Oumilkheir Hamidou
10 Juni 2019

Serikali ya Hong Kong inakataa kuachana na mswaada wa sheria inayozusha mabishano na ambayo itafungua njia kwa wahalifu kuhamishiwa China Bara, licha ya maandamano makubwa katika koloni hilo la zamani la Uingereza.

Hongkong Demonstration gegen das Zulassen von Auslieferungen nach China
Picha: picture-alliance/Zumapress/J. Russel

Jamhuri ya Umma wa China inaunga mkono kikamilifu msimamo wa serikali ya jimbo la Hong Kong inayoongozwa na mwanasiasa mkakamavu Carrie Lam na kuelezea upinzani wake dhidi ya ushawishi wa nchi za nje kufuatia maandamano makubwa yaliyofanyika jana dhidi ya mswaada huo wa sheria.

Kiongozi wa serikali ya jimbo la Hong Kong anasema serikali yake itaendelea na mjadala kuhusu kuhamishiwa China bara wahalifu licha ya maandamano. Akizungumza na waandishi habari bibi Cararie Lam amesema:"Mswaada wa sheria utajadiliwa tena Juni 12 inayokuja na tunawatolea wito wabunge wa jimbo na mashirika kadhaa pamoja na makundi ya huduma za jamii yaendelee kujadiliana kwa utulivu, busara na amani."

Wapinzani wa mswaada huo wametoa wito wa kuandamana tena jumatano inayokuja au kuitisha mgomo. "Anaijiongeza Hong Kong ukingoni mwa balaa," amesema mbunge wa vuguvugu linalopigania demokrasia, Claudia Mo.

Wahong Kong waandamana pia mjini BerlinPicha: Reuters/H. Hanschke

Chama cha kikominssti cha china kinatuhumiwa kuwa nyuma ya mswaada huo

Serikali kwa upande wake inadai sheria hiyo itadhihirisha kwamba Hong Kong inaheshimu majukumu yake ya kimataifa linapohusika suala la uhalifu katika maeneo ya mpakani na pia wa ndani.

Kiongozi wa Hong Kong, Carrie Lam, anayataja maandamano ya jana kuwa ushahidi serikali yake inaheshimu uhuru wa raia.

Mswaada huo wa sheria unakosolewa pia na nchi za magharibi na baadhi ya wakaazi wa Hong Kong wanaovituhumu vyombo vya sheria vya China bara kuwa nyuma ya mpango huo. Wapinzani wanahofia watakaopelekwa China bara hawatojivunia hajki sawa na zile wanazoweza kupata wakifikishwa mahakamani Hong Kong.

Jimbo la Hong Kong lina haki ya kuendelea na mfumo wake wa kijamii, kisheria na kisiasa kwa kipindi cha miaka 50, kufuatia makubaliano yaliyofikiwa mwaka 1997 yaliyopelekea koloni hilo la zamani la Uingereza kurejeshewa China bara. Chama tawala cha kikoministi cha China kinadhihirika kutaka kuyabadilisha makubaliano hayo.

 

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/AFP/Reuters/

Mhariri: Mohammed Khelef

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW