Hong Kong: Jimmy Lai hana hatia ya kumtishia mwanahabari
3 Septemba 2020Uamuzi wa mahakama hiyo ni kuhusu kesi ya mwaka 2017 iliokuwa ikimkabili Lai na hauna uhusiano wowote na kukamatwa kwake hapo mwezi uliopita.
Lai ambaye pia ni mkosoaji wa serikali ya Beijing, anadaiwa kutumia matamshi yasiostahili katika majibizano na mwandishi mmoja wa gazeti la "Oriental Daily News” ambalo ni mshindani mkuu na gazeti analomiliki Lai la "Apple Daily.”
Licha ya tukio hilo kutokea mnamo mwaka 2017, polisi ilimshtaki Lai kwa makosa hayo mnamo Februari mwaka huu.
Waendesha mashtaka katika kesi hiyo walisema Lai alimtishia mwandishi wa gazeti la "Oriental Daily.”
Hata hivyo, mawakili wake walisema kuwa wandishi walimfuatilia Lai kwa kipindi cha miaka mitatu na kwamba matamshi yake dhidi ya mwandishi wa "Oriental Daily” hayakulenga kumdhuru mwandishi huyo bali mteja wao alikuwa akionyesha tu khasira zake.
Lai, aliezaliwa China bara na mmmiliki wa vyombo vya habari mjini Hong Kong amekana kuwa na hatia ya makosa hayo.
Kesi hiyo inakuja baada ya Lai kutiwa nguvuni mnamo Agosti 10 kwa mashtaka ya kupanga njama na mataifa ya kigeni, na kumfanya mtu wa kwanza mwenye umaarufu mkubwa kukamatwa tangu China kuanzisha sheria ya usalama wa taifa katika kisiwa cha Hong Kong.
Katika mahakama, Lai alionekana akiwa amevalia suti yenye rangi ya kijivu na shati la kijani huku akitabasamu baada ya uamuzi huo kutolewa na kuwasalimia wafuasi wake waliokuwa wamejaa katika chumba cha mahakama.
Msaliti
Lai mwenye umri wa miaka 71 amekuwa akiitembelea Washington mara kwa mara na kukutana na maafisa wa ngazi za juu wa Marekani akiwemo Waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo Mike Pompeo ili kutafuta uungwaji mkono wa harakati za demokrasia ya Hong Kong, hatua ambayo imeipelekea China kumtaja kama "msaliti.”
Baada ya kukamatwa kwake mnamo Agosti, takriban maafisa wa polisi 200 walipekua ofisi ya gazeti lake la "Apple Daily”
Sheria ya Usalama wa taifa inajumuisha makosa ambayo China inayatizama kama uchochezi, ugaidi, harakati za kutaka kujitenga kwa kisiwa hicho pamoja na kupanga njama au kushirikiana na mataifa ya kigeni kama makosa yanaoyohatarisha usalama wa taifa na yanaadhibiwa kwa kifungo cha maisha.
Wakosoaji wa sheria hiyo yenye utata wanasema inakandamiza uhuru na haki za binadamu lakini wanaoiunga mkono wanadai itaweza kurudisha utulivu Hong Kong hasa kufuatia maandamano ya mwaka jana ya kudai demokrasia na kuipinga China.
Gazeti lake Lai "Apple Daily” linalouunga mkono harakati za demokrasia limekuwa likishindana kupata wasomaji katika Hong Kong na lile la "Oriental Daily” ambalo maudhi yake yanaegemea upande wa Beijing.
Mnamo mwaka 2014, "Orientala Daily” ilichapisha taarifa za uongo ziliodai kuwa Lai alikuwa amefariki kutokana na Ukimwi na saratani.
Mwanaharakati huyo pia anakabiliwa na kesi nyingine ikiwemo kufanya mkutano kinyume na sheria hapo mwaka jana ambao ulikuwa na lengo la kuaanda maandamo dhidi ya serikali.
Chanzo: Reuters