Hong Kong yapinga mageuzi ya uchaguzi
18 Juni 2015Alan Leong mbunge mtetezi wa demokrasia na mwanzishili mwenza wa chama cha Civic amesema "Ujumbe tunaotuma kwa serikali kuu ya na Utawala Maalum wa Mkoa wa Hong Kong ni kwamba watu wa Hong Kong hawataki kuukubali mpango huu bandia wa demokrasia.Hatutaki kura zetu zitumiwe kuhalalisha mfumo wa kura zinazoamuliwa kabla."
Wabunge 28 wameukataa utaratibu huo wa kura na wanane kuunga mkono wakati mbunge mmoja hakupiga kura yake kati ya wabunge 37 waliokuwepo kura hiyo ilipopigwa kwenye bunge la Hong Hong lenye wabunge sabini.
Kukataliwa kwa pendekezo hilo kulikuwa kukitarajiwa na yumkini kukawatuliza baadhi ya wanaharakati ambao walikuwa wakidai kupingwa kwa kile walichokiita mfumo bandia wa demokrasia wa jinsi ya kumchaguwa kiongozi wa jimbo hilo la China hapo mwaka 2017 ambalo ni kitovu cha fedha barani Asia.
Kiroja cha wabunge kutoka nje
Kiroja ni kwamba muda mfupi kabla ya kupigwa kwa kura hiyo wabunge wengi wanaoiunga mkono serikali walitoka nje ya bunge na hiyo kukosa fursa ya kupiga kura zao.
Mbunge Jeffrey Lam baadae allisema hatua yao hiyo imetokana na kutokufahamiana kwamba walikuwa wakimsubiri mbunge mwenzao alie mgonjwa kurudi bungeni.Serikali ilikuwa ikihitaji angalau kura 47 kati ya 70 kuunga mkono utaratibu huo.
Serikali ya Hong Kong ilipendekeza kuwaruhusu wapiga kura kumchaguwa kiongozi wa jimbo hilo lilioko kusini mwa China kuanzia mwaka 2017 lakini ilisalimu amri kwa shinikizo la China kwamba wagombea wachujwe na jopo la vigogo jambo ambalo viongozi wa kutetea demokrasia wameliita kuwa ni demokrasia bandia.
Katibu Kiongozi wa serikali ya Hong Kong Carrie Lam amesema amesikitishwa na kuhuzunishwa na matokeo ya kura hiyo.Lam amekaririwa akisema "Kwa wakati huu najisikia uchungu na kuvunjika moyo kwamba mpango wa mageuzi ya kisiasa umepingwa. Siwezi kutabiri lini demokrasia ya Hong Kong inaweza kusonga mbele."
China yasikitishwa
Serikali ya China Alhamisi imeelezea masikitiko yake kutokana na kushindwa kwa mpango huo wa mageuzi ya uchaguzi wa Hong Kong ambapo imesema ni kitu ambacho wasingependa kukiona.
Hata hivyo msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Lu Kang amesisitiza serikali ya China kuendelea kuunga mkono mapendekezo hayo ambayo amesema ni matumaini mazuri kwa jimbo hilo lenye kujitawala kwa kiasi fulani.
Hong Kong koloni la zamani la Uingereza linaendelea kuwa na mfumo wake wenyewe wa kisheria,kifedha na uhuru wa kiraia kama vile uhuru wa kujieleza ambao haupatikani nchini China.
Mji huo ulikuwa umekabiliwa na machafuko makubwa kabisa kuwahi kushuhudiwa mjini humo tokea China ianze kulibiti jimbo hilo hapo mwaka 1997 ambapo maelfu ya watu waliandamana mitaani kipindi cha mapukutiko mwaka jana kupinga mpango wa serikali wa kuwachuja wagombea wa uchaguzi.
Mwandishi: Mohamed Dahman/AP
Mhariri: Josephat Charo