1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hong Kong yaufuta muswada tata wa sheria

9 Julai 2019

Kiongozi wa Hong Kong Carrie Lam amesema leo kuwa muswada tata wa sheria ambao ungewezesha watuhumiwa kupelekwa China bara na ambao umezusha mgogoro mkubwa wa kisiasa katika eneo la Hong Kong umefutwa.

Hongkong PK Carrie Lam
Picha: Getty Images/AFP/A. Wallace

Lam amekiri kuwa pendekezo la  muswada huo lilikuwa anguko la aina yake kwa serikali ya Hong Kong.

Katika mkutano wa nadra na waandishi wa habari mjini Hong Kong, Lam amesema ingawa bado kuna wasiwasi juu ya nia ya serikali ya kuufuta muswada huo, amewataka raia wa Hong Kong waamini kwamba pendekezo la muswada huo halitojadiliwa tena na hakuna mipango ya kuurejesha mezani.

Katikati ya Mwezi Juni, Lam aliitikia miito ya waandamanaji kwa kuuondoa kwa muda muswada huo wa sheria lakini matamshi yake ya leo yameashiria kuwa serikali yake haina tena nia ya kuendelea na mjadala kuhusu kupitishwa kwa muswada huo.

"Nilisitisha mara moja zoezi la kufanyia marekebisho muswada ule, lakini bado kuna shaka shaka juu ya dhamira ya serikali au kuna wasiwasi kuwa serikali huenda ikaanzisha tena mchakato wa muswada huo bungeni. Nataka nisisitize hapa, hakuna mipango hiyo, muswada huo umekufa” Lam amewaambia waandishi habari mjini Hong Kong.

Lam akiri serikali ilifanya kosa kubwa

Picha: picture-alliance/AP Images/The Yomiuri Shimbun

Lam ambaye ni ni mwasiasa anayegemea China bara, ameuelezea uamuzi wa serikali yake wa kujaribu kupitisha muswada tata uliopata upinzani mkali lilikuwa kosa kubwa na amesema yupo tayari kufanya mazunguzmo na waandamanaji bila kuwepo masharti

Mkutano wa leo wa kiongozi huyo umefanyika wiki moja tangu alipozungumza na waandishi wa habari baada ya waandamanaji kuzingira na kulivamia jengo la bunge katikati ya mji wa Hong Kong.

Muswada tata wa sheria ambao ungewezesha raia wa Hong Kong kupelekwa China Bara na kushtakiwa ulizusha maandamano makubwa kuwahi kushuhudiwa mjini Hong Kong yaliyolitumbukiza koloni hilo la zamani la Uingereza katika mzozo mkubwa wa kisiasa.

Uamuazi wa Lam unaashiria kuwa ushindi kwa wapinzani wa muswada huo lakini haijawa wazi iwapo utafanikiwa kutuliza hasira na kuwaridhisha waandamanaji.

Madai ya waandamanaji yatatimizwa?

Picha: Reuters/T. Peter

Wakati wa tangazo la leo, kiongozi huyo alikwepa kuzungumzia madai ya msingi ya waandamanaji ikiwemo miito ya kutaka tume huru ya kuchunguza mwenendo wa polisi akisema madai ya sasa dhidi ya polisi yaHong Kong yanachunguzwa na mfumo wa ndani wa chombo hicho.

Katika wiki za karibuni tangu maandamano ya kwanza, waandamanaji wamekuwa wakishinikiza kujiuzulu kwa Carrie Lam, pamoja na kufanyika uchunguzi dhidi ya ukandamizaji wa polisi.

Hong Kong ilirejeshwa kwa China mwaka 1997 chini ya ahadi ya kuwa na mamlaka mapana ya kiutawala lakini katika miaka ya karibuni kumekuwa na wasiwasi kuhusu kumomonyoka kwa haki na uhuru wa Hong Kong kwenye mikono ya utawala wa China Bara.

Mzozo kuhusu muswada huo tata umekuwa changamato kubwa kwa serikali ya China mjini Beijing tangu iliporejesha tena  utawala wake kwa Hong Kong miaka 22 iliyopita.

Mwandishi: Rashid Chilumba/Reuters/AFP

Mhariri: Buwayhid, Yusra

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW