1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hong Kong:Wanaharakati wa maandamano ya demokrasia wakamatwa

Zainab Aziz Mhariri: Josephat Charo
30 Agosti 2019

Wanaharakati hao wanatuhumiwa kwa kuandaa maandamano haramu. Mamlaka inapambana kudhibiti machafuko ambayo yameitumbukiza Hong Kong kwenye mgogoro mkubwa wa kisiasa kuwahi kutokea katika kipindi cha miongo miwili.

Joshua Wong Hongkong Aktivist Protest
Picha: Phoebe Kong

Mwanaharakati Joshua Wong amekamatwa pamoja wanaharakati wenzake mapema Ijumaa wakati ambapo kuna mipango ya kufanyika maandamano mwishoni mwa wiki. Wong mwenye umri wa miaka 22 ambaye pia ni Katibu Mkuu wa chama cha Demosisto, mapema mwaka huu alitumikia kifungo cha miezi miwili gerezani kutokana na kushiriki kwenye maandamano ya mwaka 2014 yaliyoongozwa na vuguvugu lililojulikana kwa jina "Mwamvuli" lililokuwa linapinga mpango wa China wa kuwachagua wagombea wa nafasi za juu katika jiji la Hong Kong.

Chama hicho cha Demosisto kimeandika kwenye ukurasa wake rasmi wa Twitter, kwamba Katibu mkuu wao amekamatwa asubuhi ya leo saa 7:30, wakati alipokuwa akienda kwenye kituo cha treni cha Kusini cha MTR. Ujumbe huo umeeleza kwamba Wong alitumbukizwa kwa lazima ndani ya gari kweupee huku kila mtu akiona.

Mkutano wa hadhara wa siku ya Jumamosi umepigwa marufuku kwa sababu za kiusalama, ambapo polisi wamesema upo uwezekano wa vurugu kutokea kati ya polisi na waandamanaji, ambao watajitokeza kupinga marufuku hiyo.

Kamanda wa kisiwa cha Hong Kong, Patrick Kwok, amesema katika mkutano na waandishi wa habari kwamba polisi wamepiga marufuku maombi ya mkutano huo wa hadhara na maandamano ya umma katika wilaya za Kati na Magharibi yaliyopangiwa kufanyika Jumamosi hii.

Katika barua kwa waandaaji wa mkutano huo wa hadhara kundi la kutetea Haki za Binadamu (CHRF), polisi wamesema wanahofia waandamanaji wanaweza kufanya vurugu na uharibifu.

Wafuasi wa chama cha DemosistoPicha: Imago/ZUMA Press

Zaidi ya watu 850 wamekamatwa kuhusiana na maandamano tangu mwezi Juni, ikiwa ni pamoja na mwanaharakati mwingine maarufu Andy Chan ambaye alitiwa kizuizini na polisi kwenye uwanja wa ndege wa Hong Kong hapo jana Alhamisi usiku.

Chan alisimamishwa na polisi wakati alipokuwa anaelekea kupanda ndege kwenda Japan.  Wavuti ya waandishi wa habari wa Hong Kong imemnukuu msemaji wa polisi kwenye ripoti yake, akisema kwamba Chan anatuhumiwa kwa kufanya ghasia na kumshambulia afisa mmoja wa polisi.

Hong Kong imekumbwa na machafuko ya kisiasa kwa muda wa miezi mitatu sasa, na maandamano makubwa yamekuwa yakiongeza mapambano kati ya polisi na waandamanaji.

Waandamanaji wanasema China inakiuka uhuru wa jiji la Hong Kong. Chini ya sheria ya makubaliano ya mwaka 1997, China ilipoutwaa tena mji huo kutoka kwa Uingereza, mji wa Hong Kong una haki ya kuwa na mahakama huru na uhuru wa kujieleza lakini wengi wanasema haki hizo zinabanwa, huku wakitolea mifano ya kutoweka na kuzuiliwa kwa wauzaji wa vitabu, kutoruhusiwa wanasiasa mashuhuri kushiriki kwenye siasa na kufungwa kwa viongozi wa maandamano ya demokrasia.

Mkutano wa Jumamosi, ambao umepigwa marufuku, ulikuwa ni wa kuadhimisha kumbukumbu ya tano tangu serikali ya mjini Beijing ilipoanzisha mateso katika kisiwa cha Hong Kong. Uamuzi huo ulisababisha kuanzishwa kwa harakati za Mwamvuli, ambazo ziliongozwa hasa na waandamanaji vijana akiwemo Joshua Wong. Siku ya Alhamisi, China iliwapeleka wanajeshi katika jiji la Hong Kong katika kile inachokieleza kuwa ni hatua za kawaida.

Vyanzo:/RTRE7DPA/AFP/Permalink https://p.dw.com/p/3OjJU

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW