Hospitali ya taifa Tanzania yazindua huduma ya kujifukiza
4 Machi 2021Huduma hiyo ambayo inatolewa kwa mara ya kwanza na hospitali hiyo ya kutegemewa nchini huenda ikawasukuma mamia ya watu hasa kutokana na kampeni kubwa inayoendeshwa na mamlaka za kiserikali zinazohimiza utumiaji kwa wingi njia za asili kwa ajili ya kukabiliana na janga la maambukizi ya virusi vya corona.
Mkurugenzi wa hospitali ya Taifa Mumbili, Profesa Lawrance Museru, amesema vifaa vinavyotoa huduma hiyo ni mashine zilizotengenezwa hapa nchini humo na hutumia dawa za asili.
Tanzania ikiwa miongoni mwa nchi chache katika eneo la Afrika mashariki ambayo haijaruhusu chanjo dhidi ya ugonjwa wa Covid 19, haijaweka vizingiti vyovyote kwa raia wake na ujio wa huduma ya kufukiza ni mwendelezo wa huduma nyingine nyingi kama hizo zinazoendelea kupatikana nchini.
Kwa hospitali ya Muhimbili ambayo pia hivi karibuni ilianza kutengeneza barakoa zake, huduma hiyo itakuwa ikitolewa kwa gharama ya shilingi 5,000 na mtumiaji anaweza kufanya hivyo zaidi ya mara moja lakini atalazimika kuongeza malipo kama hayo.
Soma pia:Corona: Tanzania na Zanzibar zavunja kimya chao
Katika siku ya kwanza ya utoaji huduma hiyo, umati mkubwa wa watu umejitokeza kupata huduma hiyo na kuna kila dalili idadi ya watu watakaofika hapo kwa ajili ya mahitaji hayo ikaongezeka katika siku za usoni.
George Buchafwe ambaye taasisi yake ndiyo iliyofanya utafiti na kuja na mashine hii anasema ana matumaini makubwa mfumo huu wa ufukizaji utatoa majibu ya uhakika kwa watakaotumia.
Ongezeko la idadi ya vifo
Tanzania ambayo tangu katikakati ya mwaka jana haijatoa takwimu zozote kuelezea idadi ya watu waliokumbwa na maambukizi hayo wala wale waliopoteza maisha, imekuwa ikijadiliwa mara kwa mara katika medani za kimataifa namna inavyoshughulikia janga hilo.
Katika miezi ya hivi karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa la vifo vya watu vinavyohusiana na tatizo la upumuaji, tatizo ambalo limewasukuma wengi kutumia dawa za asili kama hatua mojawapo ya kunusuru maisha yao.
Soma pia: Tanzania yazipiga marufuku taasisi kuzungumzia Corona
Kama hatua mojawapo ya kukabiliana na janga hilo, Kanisa Katoliki nchini limetoa mwongozo mpya kwa waumini wake namna wanavyopaswa kushiriki ibada makanisani na wakati huu wa kuelekea Sikukuu ya Pasaka.
Kanisa hilo limekiri kupoteza makasisi wake 25 kutokana na changamoto za upumiaji huku likipoteza pia watumishi wengine kama watawa wa kike na wauuguzi wapatao 60.