Hotuba ya Emmanuel Macron Magazetini
27 Septemba 2017Tunaanza na mapendekezo ya rais wa Ufaransa Emmanuel Macron juu ya namna ya kuujenga na kuimarisha Umoja wa ulaya ili uweze kujitosheleza na kukabiliana na changamoto za karne ya 21. Gazeti la "Volksstimmen" linaisifu hotuba ya rais wa Ufarasa na kuleta uwiano kati ya hotuba hiyo na ile iliyotolewa hivi karibuni na mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Juncker. Gazeti linaandika:"Hotuba ya Emmanuel Macron ina maelezo yote ambayo yalikosekana katika hotuba iliyotolewa hivi karibuni na mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Juncker. Rais wa Ufaransa hajakosea alipokosoa uzembe ndani ya Umoja wa Ulaya. Jean-Claude Juncker anahisi Umoja wa Ulaya unanawiri. Macron amezungumzia hofu za wananchi na kusema ufumbuzi utapatikana kwa kuhakikisha usalama na kudhibitiwa. Juncker anawatisha wananchi kwa kuzungumzia juu ya kupanuliwa eneo la Schengen ambalo watu wanaweza kuingia na kutoka bila ya viza. Macron anatoa mfano wa jinsi ya kuundwa jeshi la pamoja la Umoja wa ulaya, hata kama majeshi ya nchi wanachama yatakuwa yakijiunga hatua baada ya hatua na jeshi hilo la pamoja. Hata mada iliyowekwa kando ya kodi ya hisa ameizungumzia, mada inayoungwa mkono na wengi barani Ulaya. Mfumo wa kiuchumi wa nchi za ulaya bado si wa aina moja kuweza kurahisisha kuwa na bajeti ya pamoja hata hivyo pendekezo lake la jinsi ya kuimarisha Umoja wa sarafu linaingia zaidi akilini kuliko maelezo ya Juncker."
Hotuba ya Macron ni kwa masilahi ya Ufaransa
Baadhi ya wahariri wanahisi hotuba ya Emmanuel Macron lengo lake ni moja tu nalo kuinufaisha nchi yake Ufaransa. Mfano wa mhariri wa gazeti la "Nordwest-Zeitung" anaesema:"Hotuba ya Emmanuel Macron imeleta kile kilichokuwa kikitarajiwa: Si chochote chengine isipokuwa muongozo wa kuwa na Umoja wa Ulaya kuambatana na masharti ya Ufaransa na kwa masilahi ya Ufaransa. Kuhusu fedha, Macron anailinganisha Ujerumani na ng'ombe wa kukama maziwa. Bila ya shaka Ufaransa ambayo ina nguvu za kijeshi itaudhibiti Umoja wa Ulaya na kama hakuna budi , basi kuigeuza Ujerumani kama jeshi la kutumikia masilahi yake nchi za nje mfano barani Afrika. Walinzi wa mazingira tayari wanaisifu hotuba ya Macron. Kilichosalia ni kuwaona waliberali wa FDP kama wataruhusu sera hiyo ya Macron ifuatwe au la na serikali kuu ya Ujerumani."
Nani achaguliwe kuwa spika wa bunge jipya la Ujerumani?
Mada yetu ya mwisho magazetini inaturejesha Ujerumani na mitihani inayolikabili bunge jipya la shirikisho-Bundestag. Gazeti la "Hannoversche Allgemeine" linaandika: "Nini kitatokea katika bunge jipya?Je, litakuwa jukwaa la mijadala ya maana au uwanja wa kutolewa matamshi ya chuki, watu kutukanana na hujuma zisizokuwa na maana? Suala hilo ni la kina. Kwa sababu linahusiana na desturi inayostahiki mbele ya katiba. Ndio maana kuna umuhimu wa kuchaguliwa spika mwenye fasaha na uwezo wa kudhibiti hali ya mambo. Na upande huo, hakuna mwengine isipokuwa Wolfgang Schäuble.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir
Mhariri: Josephat Charo