Angela Merkel: Demokrasia hustawi kwa mabadiliko
31 Desemba 2018Katika hotuba yake ya kuukaribisha mwaka mpya, kansela wa Ujerumani anaanza kuelekeza maneno yake kwa watu wa taifa lake. "Wapendwa raia wenzangu." Lakini maneno hayo yanapaswa pia kusikilizwa kwa umakini nje ya mipaka ya Ujerumani. Merkel anapozungumzia kile anachokiona kama "hali mgumu zaidi kisiasa," anafanya hivyo kwa mitazamo mwili: wa ndani na wa kimataifa.
Kansela huyo anaanza hotuba yake kwa mtazamo wa ndani juu ya mchakato mgumu wa kuunda serikali baada ya uchaguzi wa shirikisho wa mwaka 2017. Mchakato huo ulidumu kwa miezi sita "na baada ya kuipata, kulikuwa na malumbano mengi na kushughulishana wenyewe." Merkel, mwanachama wa chama cha Christian Democratic Unioni (CDU), hataji mifano yoyote.
Lakini miwili inakumbukwa sana: Mgogoro usiobadilika na waziri wake wa mambo ya ndani Horst Seehofer kutoka chama ndugu na CDU cha jimboni Bavaria, Christian Social Union (CSU), na mizozo na chama mshirika mdogo katika serikali cha Social Democratic (SPD). Sehemu kubwa ya migogoro hii ilihusu sera ya uhamiaji ya Ujerumani.
Maswali ya majaliwa: Mabadiliko ya tabianchi, uhamiaji, ugaidi
Lakini Merkel hataki hali ya mgogoro ndani ya serikali ya muungano kueleweka kama sababu ya nia yake ya kuachia nafasi ya kansela mwishoni mwa muhula huu wa bunge mwaka 2021. Anasema angefanya hivyo "bila kujali ni kwa kiasi gani mwaka uliopita ulikuwa hauridhishi." Kipindi chake cha uongozi, ambacho kimedumu kwa miaka 13, ni "sababu tosha." Tunajengea juu ya kile "watangulizi wetu walichotuachia" na kuunda wakati wa sasa kwa ajili ya watakaokuja baada yetu. "Demokrasia," anasema Merkel, inastawi kwa mabadiliko."
Merkel anaamini kwamba changamoto za wakati huu zinaweza kutatuliwa "ikiwa tutaungana pamoja na kushirikiana na wengine nje ya mipaka yetu." Changamoto hizi zihahusisha siyo tu "maswali ya majaliwa kuhusu mabadiliko ya tabianchi," lakini pia uhamiaji na mapambano dhidi ya ugaidi wa kimataifa. "Tunataka kutatua maswala haya yote kwa sababu ni katika maslahi yetu."
Jukumu la Ujerumani katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa
Hata hivyo, utayarifu wa kukubali changamoto nyingi umezungukwa na mashaka. Merkel anasema uhakika wa jadi wa ushirikiano wa kimataifa umekabiliwa na shinikizo. Hata hapa hatowi mifano. Lakini hakuna shaka kwamba hii inajumlisha siasa za kizalendo katika pande mbili za kanda ya Atlantiki. Hitimisho lake: "Katika hali kama hiyo, tunapaswa kutetea, kujenga hoja na kupigania imani zetu kwa kusadikisha zaidi."
Akizungumzia kiti cha Ujerumani katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambacho itaanza kukikalia kuanzia Januari Mosi na chenye ukomo wa miaka miwili, Merkel anasema Ujerumani itafanya utetezi kwa ajili ya masuluhisho ya kimataifa. "Tunaendelea kuongeza ufadhili wetu wa masuala ya kibinadamu na misaada ya kimaendeleo, na pia tunaimarisha matumizi yetu ya kijeshi."
Ujerumani pia itafanya kazi kuufanya Umoja wa Ulaya kuwa wenye nguvu na uwezo zaidi na kutafuta kuendeleza ushirikiano na Uingereza licha ya mpango wake wa kujiondoa katika Umoja wa Ulaya. Kansela Merkel pia amewatolea mwito Wajerumani kuusaidia Umoja wa Ulaya kuendelea kuwa "mradi wa amani, mafanikio na usalama" wakati kanda hiyo ikijiandaa na uchaguzi wa Ulaya mwezi Mei.
'Uwazi, kuvumiliana na heshima'
Mwishoni mwa hotuba yake, Merkel anatazama ndani tena. Kuhusu juhudi za kufanikisha lengo la mazingira sawa ya kuishi, anasema serikali ya Ujerumani inataka kuhakikisha kwamba kila mmoja anapata elimu nzuri, makazi na huduma za afya. Anasema ni kujaribu kutafuta "masuluhisho bora" kwa matatizo hayo.
"Zaidi na zaidi hata hivyo, pia ni kuhusu mfumo wetu wa maingiliano, kuhusu maadili yetu: uwazi, kuvumiliana na heshima." Merkel ana wasiwasi kuhusu mazingira ya kisiasa nchini Ujerumani, ambayo yamegeuka magumu zaidi katika mwaka wa 2018. Na licha ya ukweli huo anaedelea kuwa na imani: "Tunapoamini katika maadili yetu na kutekeleza mawazo yetu kwa ari, jambo jipya na zuri linaweza kujitokeza."
Mwnadishi: Marcel Fürstenau
Tafsiri: Iddi Ssessanga
Mhariri: Sekione Kitojo