1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UchumiUswisi

Hotuba ya Trump yasubiriwa kwa hamu kwenye Jukwaa la WEF

21 Januari 2026

Mkutano wa Jukwaa la Kimataifa la Uchumi, WEF unaingia siku ya pili na kubwa linalosubiriwa likiwa ni hotuba ya Rais wa Marekani Donald Trump siku moja baada ya hotuba za viongozi wa Ulaya.

Kambi ya Pamoja ya Marekani ya Andrews 2026 | Donald Trump apanda ndege ya Air Force One kuelekea Davos
Rais Donald Trump akipanda Air Force One anapoondoka Washington kuelekea Uswisi mnamo Januari 20, 2026 katika Kambi ya Pamoja ya Andrews, Maryland.Picha: Chip Somodevilla/Getty Images

Ziara hii ya tatu ya Trump kama rais inafanyika huku washirika wa Marekani wakiwa na wasiwasi kuhusu azma yake ya kukichukua kisiwa cha Greenland, na kwa upande mwingine, huku Amerika ya Kusini nayo ikijizatiti kukabiliana na juhudi zake za kunyakua mafuta ya Venezuela.

Lawama zilisikika jana Jumanne wakati viongozi wa Ulaya walipotoa hotuba kwenye jukwaa hilo na kumlaumu vikali Trump juu ya juhudi zake mpya za kutaka kukinyakua kisiwa cha Greenland na kuibua upinzani mkali kutoka kwa viongozi wa Ulaya na Canada.

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen alisema katika hotuba maalumu katika jukwaa hilo kwamba "Uhuru na uadilifu wa eneo la Denmark haviwezi kujadiliwa," akithibitisha tena mshikamano kamili wa Umoja wa Ulaya na Greenland pamoja na Denmark.

Scott Bessent, Waziri wa Fedha wa Marekani, akitoa hotuba katika Ikulu ya Marekani kuhusu Mkutano wa Mwaka wa Jukwaa la Uchumi Duniani huko Davos, Uswisi, Jumanne, Januari 20, 2026.Picha: Markus Schreiber/AP Photo/picture alliance

Lakini, mapema leo Waziri wa Fedha wa Marekani Scott Bessent aliitaka Ulaya kuacha kutoa majibu ya haraka na yaliyojaa ghadhabu na badala yake wakutane na Trump kwenye kongamano hilo ili kusikiliza hoja zake kuhusu Greenland.

Bessent amesema hayo alipozungumza na waandishi wa habari saa chache kabla ya Trump kuwasili katika jukwaa hilo la kila mwaka.

Canada yaonya dhidi ya mipasuko ulimwenguni

Lakini, Waziri Mkuu wa Canada Mark Carney kwa upande wake ameonya kuhusu mipasuko ya kimataifa inayopindukia vitisho vya Marekani dhidi ya Greenland.

Waziri Mkuu wa Canada Mark Carney akitoa hotuba wakati wa mkutano wa kila mwaka wa Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF) huko Davos mnamo Januari 20, 2026.Picha: Fabrice Coffrini/AFP/Getty Images

"Ningesema kwamba kuna vitisho. Urusi, bila shaka, ni kitisho katika eneo la Arctic, bila shaka. Urusi hufanya mambo mengi mabaya na ninachukua fursa hii kulaani uvamizi wao usio wa haki na wa kutisha dhidi ya Ukraine, karibu katika mwaka wake wa nne.''

Carney amesisitiza kwamba nguvu za Marekani zinamaanisha kwamba utaratibu unaotegemea sheria haukukamilika, huku utekelezaji wa sheria za biashara na sheria za kimataifa zikitumika kwa msingi wa nguvu za kijeshi na kiuchumi.

Canada, mwanachama mwanzilishi wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO pia ilitishiwa na Marekani, na rais Trump aliwahi kumtaja Waziri Mkuu huyo kama "gavana" tu wa nchi hiyo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi akitoa hotuba huku kukiwa na machafuko yanayoendelea kupinga serikali, mjini Tehran, Iran, Januari 12, 2026, katika picha hii iliyochukuliwa kwenye videoPicha: IRIB/REUTERS

Iran yaionya Marekani, mwaliko wa WEF wafutwa

Katika hatua nyingine, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi ametoa vitisho vya moja kwa moja hii leo dhidi ya Marekani, siku moja baada ya mwaliko wake kwenye jukwaa hilo kufutwa kutokana na hatua kali za serikali yake dhidi ya waandamanaji.

Kwenye maoni yake yaliyochapishwa na Jarida la The Wall Street la Marekani, Araghchi ameionya tena Marekani ikiwa ina mipango ya kuivamia. Aliandika, tofauti na namna Iran ilivyojizuia Juni 2025, vikosi vyao vyenye nguvu havina wasiwasi wowote kuhusu kujibu mapigo kwa kutumia kila walichonacho ikiwa watashambuliwa upya," akimaanisha vita vya siku 12 vya mwaka jana ambavyo Israel ilivianzisha dhidi ya Iran.

Akaonya uvamizi kamili utakuwa ni mkali, utakaochukua muda mrefu zaidi na utakaoenea katika eneo lote na kuwaathiri watu wa kawaida kote ulimwenguni.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW