1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HOTUBA YA RAIS WULFF.

Mohamed Dahman25 Desemba 2010

Rais wa Ujerumani Christian Wulff amewataka wananchi wajenge moyo wa mshikamano katika maisha yao ya kila siku.

Rais wa Ujerumani Christian Wulff.Picha: Bundesregierung/Steffen Kugler/dapd

Rais Wulff ametoa mwito huo kwa wananchi wa Ujerumani katika hotuba ya kuadhimisha Sikukuu ya Krismasi.

Katika hotuba yake Rais Wulff pia amesisitiza juu ya maadili ya umoja, uelewano na mshikamano.

Amesema wote wapo pamoja, wanasaidiana na wamefungamana.

Rais huyo wa Ujerumani amesisitza juu ya maadili ya kusaidiana na moyo wa kujitolea.

Hata hivyo ameeleza kuwa hayo hayajileti yenyewe. Panahitajika matendo ili kuyaleta.

Rais Wulff amesema jamii ya Ujerumani inawategemea wanajamii wanaotambua wapi wanahitajika, bila ya kufikiria kwa muda mrefu iwapo wakubali kutimiza majukumu.

Kiongozi huyo wa Ujerumani amewapongeza wananchi wanaowashughulikia watoto,wanaowasaidia walemavu na watu wengine wote ikiwa pamoja na wagonjwa.

Akizungumzia juu ya sera za nje kiongozi huyo wa Ujerumani amesema kuwa Ujerumani inaheshimika sana kutokana na moyo wake wa stahamala na kutokana na kuaminika miongoni mwa mataifa madogo na makubwa.

Rais Wulff amesema

Ujerumani inaonyesha mshikamano na ipo tayari pia katika siku za usoni kutekeleza wajibu wake pia barani Ulaya.

Bwana Wulff ameeleza kuwa anatumai kuwa nchi nyingine washirika nazo zitakuwa na moyo kama huo. Amesisitiza msimamo wa Ujerumani juu ya umoja wa Ulaya na mchango wa Ujerumani katika kudumisha amani,kuleta maendeleo na kupambana na ugaidi duniani.

Amesema Ujerumani ina imani na Umoja wa Ulaya na nguvu zake.

Amefahamisha kuwa wananchi wengi wa Ujerumani wanatimiza majukumu katika nchi za nje kama polisi na wanajeshi, katika kudumisha amani, kushiriki katika ujenzi mpya na katika harakati za kupambana na ugaidi .Rais wa Ujerumani ametoa mwito wa kuleta amani duniani kote na amewataka watu wajizatiti upya katika kusimama pamoja.

Amesisitiza umuhimu wa kuyazingatia yale yanayowaleta watu pamoja.Na ameeleza kuwa hayo yanaanza kwa hatua ndogo tu. Ametoa mwito wa kuheshimiana katika jamii ambapo pana wanajamii wenye nasaba na dini mbalimbali.

Ameeleza kuwa pana haja ya kuheshimu na kutambua kwamba wanajamii fulani ni tofauti na wengine.

Katika salamu zake za Krismasi Rais wa Ujerumani bwana Wulff pia amewataka wazazi watenge muda zaidi kwa ajili ya kuwa pamoja na watoto wao.

Rais Wulff amesema sawa na ujumbe uliotoka Bethlehem miaka zaidi ya 2000 iliyopita, yeye pia amewatakia

watu wote duniani amani sikukuu ya furaha na baraka za mwaka mpya wa 2011."

Mwandishi/Wulff,Christian/

Tafsiri/Mtullya abdu/

Mpitiaji: Dahman