1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hotuba ya waziri mkuu wa Zimbabwe Tsvangirai bungeni yaahirishwa.

12 Mei 2009

Ilikua ni ya kutathimini kazi za serikali ya umoja wa taifa miezi mitatu tangu ilipoundwa.

Waziri mkuu Morgan TsvangiraiPicha: AP

Msemaji wa Tsvangirai, James Maridadi aliliambia shirika la habari la AFP kwamba hotuba hiyo sasa itatolewa bungeni wiki ijayo,lakini bila ya kutaja tarehe . Duru za serikali zikasema kwamba waziri mkuu huyo alikua akihudhuria mkutano wa kila wiki wa baraza la mawaziri na hiyo ndiyo sababu ya kuahirisha kutoa hotuba yake bungeni.

Tsvangirai alichukua wadhifa wa Waziri mkuu kugawana madaraka na Rais Robert Mugabe tarehe 11 Februari katika serikali ya umoja wa taifa kati ya Zanu-Pf na kilichokua chama kikuu cha upinzani Movement for Democratic Change MDC cha Tsvangirai na tawi lililojitenga la naibu waziri mkuu Arthur Mutambara.

Hatua hiyo iliirejesha Zimbabwe katika hali ya utulivu baada ya mgogoro ulizuka kutokana na matokeo ya uchaguzi mwaka jana.

Kuundwa kwa serikali hiyo kulirejesha kwa kiwango fulani imani ya wafadhili huku shirika la fedha la kimataifa IMF likisema litaanza tena kutoa misaada ya kiufundi kwa Zimbabwe. Vitu vimeanza kuonekana tena madukani na bei ambazo sasa zimefungamanishwa na dola ya Marekani kutokana na kuanguka kabisa dola ya Zimbabwe, zimeanza kuwa za nafuu.

Wachambuzi lakini pamoja na hayo , wanasema hakuna kikubwa kilichobadílika katika maisha ya raia tangu mahasimu wa kisiasa waliposaini makubaliano ya kuunda serikali ya umoja wa taifa.

Mhadhiri mmoja katika kitivo cha sheria cha chuo kikuu cha Zimbabwe Lovemore Madhuku anasema, lililo jipya ni kuwa kinyume na zamani hauonekani tena ule uhasama wa wazi.

Vyama vya kisiasa katika serikali hiyo bado havijajaza nafasi za magavana wa mikoa, kukizidi kupatikana taariafa za kuvamiwa mashamba, pamoja na kukamatawa wiki iliopita kwa wanaharakati wa haki za binaadamu ambao baadae waliachiwa kwa dhamana.

Jana wahariri wawili wa gazeti moja huru walikamatwa wakati chama cha wakulima wa mazao ya biashara CFU kinasema zaidi ya wakulima 100 wamekumbwa na visa vya kusumbuliwa kwenye mashamba yao au kushtakiwa, mezi mitatu baada ya kuundwa serikali hiyo ya umoja wa taifa.

Wakulima wa kizungu bado wanaedelea kubughudhiwa.Picha: AP

Serikali hiyo ambayo waziri mkuu Tsvangirai ameitaja kuwa muflisi baada ya hali mbaya ya kiuchumi ilozusha kiwango kikubwa kabisa cha ughali wa maisha duniani , tarehe 22 mwezi huu wa Mei itatimia siku 100 tangu iundwe.

Hadi sasa inaweza tu kuwalipa wafanyakazi posho ya dola 100 bila kujali wadhifa wao na na hospitali za serikali bado hazina madawa licha ya kufunguliwa. Waalimu wametishia kugoma, wakidai mishahara ili kuweza kuwapa karo za shule kwa watoto wao wenyewe.

Wakati ikikaribia siku 100 tangu kuundwa na sasa ikisubiriwa kwa hamu hotuba ya Waziri mkuu Tsvangirai wiki ijayo, yaelekea bado serikali hiyo ya umoja wa taifa inakabiliwa na changa moto kubwa.