1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Viongozi wa dunia kuhutubia Baraza Kuu la UN kuanzia Jumanne

Angela Mdungu
23 Septemba 2024

Viongozi wa dunia juma hili wako jijini New York nchini Marekani kuhudhuria Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Hotuba za kuashiria kuanza kwa mkutano huo zinatarajiwa rasmi Jumanne.

USA UN-Vollversammlung Srebrenica Genozid Anerkennung Abstimmung
Picha: Selcuk Acar/Andalou/picture alliance

Mamia ya viongozi hao wa dunia wanakutana wakati Umoja wa Mataifa ukikabiliwa na changamoto kadhaa zikiwemo mabadiliko ya hali ya hewa, mgogoro wa Mashariki ya Kati, na vita vya Urusi na Ukraine.

Mkutano wa 79 wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa unaofanyika kila mwaka utakaochukua muda wa siku sita unahudhuriwa na mataifa 193 wanachama. Viongozi wa mataifa hayo watatoa hotuba zao huku Palestina ikitarajiwa kushiriki.

Kama ilivyo utamaduni katika katika hotuba rasmi zitakazoanza kutolewa Jumanne, Brazil inatazamiwa kuwa msemaji wa kwanza huku Marekani ambayo ni mwenyeji ikipewa nafasi ya pili kutoa hotuba yake. Wakuu wa nchi wanachama ndiyo watakaoanza kuhutubia wakifuatiwa na manaibu wao,wakuu wa serikali, mawaziri na viongozi wengine.

Wapalestina wakikagua jengo lililoharibiwa baada ya shambulizi la anga la Israel kwenye shule inayohifadhi watu waliokimbia makazi yao katika kitongoji cha Zeitoun kusini mwa Jiji la Gaza, Septemba 21, 2024. Mzozo huu utajadiliwa kwenye mkutano wa UNGAPicha: Mahmoud Zaki/Xinhua/IMAGO

Mizozo ya Ukraine na Gaza kuangaziwa kwa upana

Kauli mbiu ya mwaka huu ni "kutomuacha mtu nyuma, kuchukua hatua kwa pamoja ili kuendeleza amani, maendeleo endelevu na heshima ya utu kwa kizazi cha sasa na vizazi vijavyo."

Miongoni mwa mada zinazotarajiwa kuangaziwa kwenye mkutano huo ni pamoja na vita vya Gaza ambako hadi sasa zaidi ya wa 41,00 wameuwawa. Mzozo wa Ukraine pia unatazamiwa kupewa nafasi kwenye mkutano huo huku miito ya kumalizwa kwa mizozo hiyo ikitarajiwa kutolewa.

Mabadiliko ya hali ya hewa ni mada itakayozungumziwa pia wakati huu ambapo dunia inapambana na ongezeko la joto.

Wakati wa mkutano huo wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa, viongozi wengi hasa wa Afrika na mataifa makubwa yakiwemo Brazil, Ujerumani, India, na  Japan  wanatazamiwa kutoa wito wa kufanyiwa mabadiliko kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lenye jukumu la kihakikisha amani na usalama katika ngazi ya kimataifa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameonya juu ya mabadiliko ya kiulimwengu na kutaka hatua kuchukuliwa haraka Picha: Yuki Iwamura/AP Photo/picture alliance

Guterres azindua mkutano juu ya changamoto za ulimwengu

Kabla ya kuanza rasmi kwa mkutano huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres mapema Jumapili alizindua mkutano wa pembezoni uliojadili changamoto nzito zinazoukabili ulimwengu zikiwemo mabadiliko ya tabia nchi, vita,  umasikini na teknolojia ya akili mnemba.

Soma pia:WFP yatahadharisha juu ya kuongezeka kwa njaa

Katika Mkutano huo Guterres alisisitiza kuwa, "Dunia yetu inapitia misukosuko na mabadiliko. Lakini hatuwezi kukaa tu na kusubiri hadi kuwe na hali nzuri.

Tunapaswa kuchukua hatua za kwanza  za maamuzi katika kusasisha na kurekebisha ushirikiano wa kimataifa ili uwe wa haki zaidi na unaojumuisha. Na ninawashukuru kwa juhudi zenu kuwa leo tumefanikiwa."

Viongozi mbalimbali walihutubia wakati wa mkutano huo baada ya kupitisha kile walichokiita ''Azimio la hatma ya ulimwengu" linalolenga kuhakikisha ushirikiano zaidi kati ya mataifa. Wengi wa viongozi wakati wa mkutano huo walisisitiza  juu ya umuhimu wa kupata fedha zaidi ili kufadhili masuala ya mazingira.