HRW: Majeshi ya Sudan Kusini yaliwaua na kuwabaka raia
16 Agosti 2016Human Rights Watch imesema watafiti wake walirekodi mauaji, ubakaji, mateso, uporaji na unyanyasaji dhidi ya raia wa kabila la Nuer katika kipindi cha siku nne za mapigano yaliyozuka mwezi uliopita.
Shirika hilo pia limesema mnamo tarehe 11 mwezi Julai, wanajeshi wa serikali waliivamia hoteli moja inayowahifadhi wafanyakazi wa mashirika ya kigeni ambapo walimuua mwanahabari ambaye anatokea kabila la Nuer na kuwabaka wanawake, kuwapiga na kuwaibia raia wa kigeni.
Wanajeshi wa kulinda amani wa kikosi cha Umoja wa Mataifa na balozi za kigeni ukiwemo ubalozi wa Marekani haukuwasaidia waathiriwa hao licha ya wito wao.
Wanajeshi wa UN hawakutoa ulinzi
Human Rights Watch imesema wanajeshi wa Umoja wa Mataifa hawakutoka katika kambi zao kutelekeza jukumu lao la kuwalinda raia waliokuwa katika hatari katika uvamizi huo uliodumu masaa manne.
Umoja wa Mataifa umesema watu 73 waliuawa katika mapigano hayo ya Juba lakini vyanzo vingine vinaarifu mamia ya watu waliuawa na maelfu ya raia wa Sudan Kusini walikimbilia katika nchi jirani.
Mengi ya mashambulizi yaliyofanywa na majeshi yaliwalenga watu wa kabila la Nuer analotokea kiongozi wa waasi Riek Machar. Wanajeshi hao wanadaiwa waliendelea kuwashambulia raia hata baada ya serikali kutangaza makubaliano ya kusitisha mapigano tarehe 11.
Msemaji wa jeshi la Sudan Kusini Lul Ruai Koang amesema hajaisoma ripoti hiyo ya Human Right Watch lakini akaongeza kusema hajashangzwa na ripoti hiyo kwani shirika hilo linaiga yale yaliyosemwa na Umoja wa Mataifa.
Koang amesema hakuna mtu yeyote aliyewapa taarifa za kina kuliruhusu jeshi kuwachukulia hatua wanaodaiwa kuhusika na uhalifu huo dhidi ya raia.
Maelfu wameuawa Sudan Kusini
Mvutano kati ya Rais Kiir na aliyekuwa makamu wake wa Rais Riek Machar ulisababisha kuzuka vita mwaka 2013 katika taifa hilo changa zaidi duniani, vita ambavyo vimeasababisha mauaji a maelfu ya watu na kuwaacha zaidi ya watu milioni 2 bila ya makaazi.
Matumaini ya kupatikana amani yamefifia kufuatia mapigano hayo ya hivi karibuni na kufutwa kazi kwa Machar, ambaye chini ya makubaliano yaliyofikiwa mwezi Agosti mwaka jana aliteuliwa tena makamu wa Rais miezi michache iliyopita lakini alilazimika kwenda mafichoni baada ya mapigano kuzuka mwezi uliopita na wadhifa wake kuchukuliwa na Taban Deng Gai.
Hapo jana Rais Kiir alisema anatafakari uamuzi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la kuwatuma wanajeshi 4,000 zaidi wa kulinda amani nchini humo.
Awali kabla ya baraza hilo la usalama kupitisha azimio siku ya Ijumma wiki iliyopita la kupeleka majeshi zaidi nchini humo, serikali ya Sudan Kusini ilikuwa imekataa pendekezo la kupelekwa majeshi ya Umoja wa Mataifa.
Mwandishi: Caro Robi/dpa
Mhariri:Hamidou Oumilkheir