1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HRW: Malawi ihakikishe uchaguzi huru na salama

4 Juni 2020

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu, Human Rights Watch, limewataka maafisa wa Malawi kuhakikisha kwamba uchaguzi ujao wa urais unakuwa huru na unafanyika kwa uwazi katika wakati huu wa janga la COVID-19.

Kampeni za uchaguzi Malawi
Picha: Getty Images/AFP/A. Gumulira

Uchaguzi wa marudio nchini Malawi umepangwa kufanyika Julai 2 baada ya Mahakama ya Juu Mei 8 kubatilisha matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi Rais Peter Mutharika katika uchaguzi wa Mei 2019, ikielezea kuwepo kwa dosari na ukiukaji wa taratibu za uchaguzi na hivyo kuamuru uchaguzi ufanyike ndani ya siku 150.

Katika uchaguzi huo Rais Mutharika wa chama tawala cha Democratic Progressive, DPP atakuwa anapambana na Lazarus Chakwera mgombea anayeungwa mkono na muungano wa vyama vya upinzani, kikiwemo chama cha Malawi Congress na United Transformation Movement. 

Taarifa zaidi: Malawi kufanya uchaguzi wa marudio Julai 2

Muungano wa mashirika ya kutetea haki za binaadamu nchini Malawi, HRDC, umeripoti kuwa tangu mwezi Mei kumekuwa na ongezeko la ghasia za kisiasa zinazochochewa dhidi ya wanasiasa wa upinzani, wanaharakati wa haki za binaadamu pamoja na waandishi habari. Hata hivyo, HRDC imesema wale wanaoshukiwa kuhusika na ghasia hizo bado hawajakamatwa.

Dewa Mavhinga, mkurugenzi wa shirika la Human Rights Watch katika ukanda wa kusini mwa Afrika, anasema viongozi wa Malawi wanapaswa kuendeleza mara moja mchakato utakaohakikisha kuwa uchaguzi unakuwa huru, salama na unafanyika kwa uwazi. Mavhinga amesema maafisa hao wanapaswa kuweka hatua kadhaa za kuwalinda raia dhidi ya ghasia na kuwashitaki ipasavyo wote wanaohusika.

Baadhi ya makundi yatishia kufanya vurugu

Picha: Getty Images/AFP/A. Gumulira

Kampeni za uchaguzi wa marudio wa Malawi zinaendelea wakati ambapo kuna janga la COVID-19, huku nchi hiyo ikiwa imerekodi visa 284 vya virusi vya corona hadi Juni Mosi. Serikali imesema kwamba virusi hivyo havitoingiliana na uchagauzi.

Usiku wa Mei 4, watu wasiojulikana walirusha mabomu ya mkono kwenye ofisi ya chama cha United Transformation Movement, kinachoongozwa na makamu wa Rais Saulos Chilima kwenye mji mkuu, Lilongwe na kusababisha vifo vya watu watatu na kuwajeruhi wengine watatu.

Wiki iliyopita, video ambazo zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha makundi ya wanaume waliokuwa wamevalia sare za chama cha Democratic Progressive, wakitishia kufanya vurugu na kuutangaza mji wa Mangochi, ulioko mashariki mwa Malawi kuwa ni eneo ambalo vyama vya upinzani havipaswi kwenda.

Waandishi wa habari wajeruhiwa

Mei 4, maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini Malawi waliandika barua ya pamoja ya kichungaji wakiainisha mambo manane yanayoleta wasiwasi nchini humo, ikiwemo kuongezeka kwa vitendo vya ghasia za kisiasa, ambavyo wamelaani vikali.

Mei 29, msafara wa kampeni wa Chilima, ambaye ametofautiana na Rais Mutharika na ni mgombea mwenza wa Chakwera, ulipigwa mawe kwenye mji wa Phalombe, ambako ni nyumbani kwa Mutharika kusini mwa nchi hiyo. Chombo binafsi cha habari cha Zodiak kiliripoti kuwa waandishi habari kadhaa waliokuwepo kwenye msafara huo walijeruhiwa.

Nchi za Afrika zaendelea kupambana na Corona

This browser does not support the audio element.

HRDC imeripoti kuwa wiki ya mwisho ya Mei, watu 12 wanaoshukiwa kuwa wafuasi wa chama tawala walimshambulia kiongozi wa shirika hilo, Timothy Mtambo mjini Blantrye. Mlinzi wake aliwakamata washambuliaji hao na kuwakabidhi kwa polisi, lakini waliachiliwa huru bila kufunguliwa mashtaka.
 

Mavhinga anasema maafisa wa Malawi wanapaswa kutekeleza jukumu lao kuhakikisha haki za raia wote wa Malawi wanaostahili kupiga kura zinalindwa na uchaguzi unafanyika kwa uwazi na unakuwa huru. Amesema ghasia za kisiasa zinahitaji kumalizika ili kuhakikisha mazingira mazuri ya kuwepo uchaguzi wa kuaminika.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo

Mhariri: Iddi Ssessanga

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW