1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HRW: Mali sharti ichunguze madai ya mauaji

23 Oktoba 2021

Shirika la kimataifa la kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch limeutolea wito Umoja wa Mataifa kuishinikiza Mali kuchunguza madai ya uhalifu uliofanywa na vikosi vyake vya usalama.

Mali Premierminister Choguel Kokalla Maïga
Picha: Presse- und Kommunikationsdienst des Premierministers von Mali

Human Rights Watch inautaka Umoja wa Mataifa kuyatumia mazungumzo yake na serikali ya Mali yaliyopangwa kufanyika siku ya Jumamosi kushinikiza uchunguzi wa ripoti ya juu ya mauaji na kupotezwa kwa watu, visa vinavyotajwa kutendwa na vyombo vya dola vya taifa hilo.

Mwito huo umetolewa wakati ujumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa unatarajiwa kuwasili mji mkuu wa Mali, Bamako, leo Jumamosi kuzishinikiza mamlaka za taifa hilo kuruhusu kurejea kwa utawala wa kiraia baada yakutokea mapinduzi ya kijeshi mara mbili chini ya mwaka mmoja.

Ujumbe huo unaojumuisha mabalozi wa nchi wanachama 15 wa Baraza la Usalama ikiwemo China, India, Urusi na Marekani utalitembelea pia taifa jirani la Niger siku ya Jumapili.

Wakiwa mjini Bamako, watakutana na "viongozi waandamizi wa serikali ya mpito pamoja na makundi ya kiraia yanayofanya kazi ya kuimarisha taasisi za kidemokrasia nchini humo"

"Ziara hii itausaidia ujumbe huo kufahamu kwa undani changamoto za kisiasa na kiusalama nchini Mali na kuhakikisha mchakato wa kurejea kwa utawala wa kiraia uliochaguliwa kidemokrasia ifikapo Februari 2022 kama ilivyopangwa" imesema taarifa iliyotolewa na Marekani kuelekea ziara hiyo.

Human Rights Watch yaongeza joto kwa watawala wa Mali

Waziri Mku wa Mali, Choguel Kokalla MaïgaPicha: Presse- und Kommunikationsdienst des Premierministers von Mali

Taarifa iliyotolewa na shirika la Human Rights Watch inazitaka "mamlaka nchini Mali kuchunguza mfululizo wa madai ya kutokea visa vya watu kunyongwa, kupotezwa na kushikiliwa kinyume na sheria na vikosi vya serikali"

Shirika hilo lenye makao yake mjini New York pia limetoa mwito wa kufanyika uchunguzi wa matendo ya kihalifu yaliyofanywa na pande zote kwenye mzozo huo wa Mali.

Human Rights Watch limetoa mfano wa wanaume 14 walionekana kwa mara ya mwisho mwezi Septemba wakiwa kwenye kizuizi kinachoendeshwa na vikosi vya usalama na ambao tangu wakati huo "wamepotea au wanashikiliwa bila kufunguliwa mashtaka"

 Kadhalika limeorodhesha kisa cha miili mitatu iliyopatikana karibu na kambi moja ya jeshi kwenye mji wa Sofara ambayo inasadikiwa kuwa ni ya watu "walionyongwa baada ya kukamatwa na wanajeshi mwezi Oktoba"

"Serikali ya mpito ya Mali haipaswi kusimama kanda wakati wanajeshi wake wanapohusishwa na wimbi la matendo ya uhalifu na ukatili" amesema mkurugenzi wa kanda ya Sahel wa shirika la Human Rights Watch.

Mali, taifa lililo kwenye mkwamo 

Mali, taifa masikini magharibi mwa Afrika na nyumbani kwa karibu makundi 20 ya kikabila inapambana na mashambulizi ya itikadi kali na vurugu miongoni mwa koo za jamii mbalimbali.

Tangu mwaka 2012 uasi wa makundi ya itkadi kali ya Kiislamu umesambaa katikati ya taifa hilo na kuingia hadi nchi jirani za Niger na Burkina Fasso.

Licha ya juhudi za Umoja wa Mataifa na msaada wa kijeshi kutoka Ufaransa, mzozo huo umesababisha maelfu ya watu kufa na mamia kwa maelfu wengine wamepoteza maakazi yao.

    

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW