1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HRW: Rwanda inakiuka haki za binaadamu magerezani

15 Oktoba 2024

Shirika la kimataifa la utetezi wa haki za binaadamu la Human Rights Watch limechapisha ripoti mpya inayosema, mamlaka nchini Rwanda zinafanya ukiukaji mkubwa wa haki za binaadamu magerezani, ikiwemo kuwatesa wafungwa.

Muonekano wa lango kuu la gereza la Mageragere nchini Rwanda.
Muonekano wa lango kuu la gereza la Mageragere nchini Rwanda.Picha: Jean Bizimana/REUTERS

Chini ya utawala wa miongo mitatu wa Rais Paul Kagame, upinzani wa kisiasa na uhuru wa kujieleza unaelezwa kukandamizwa, huku wanaharakati kutoka katika jumuiya ya kimataifa wakilaani kwa muda mrefu nafasi ya haki za kiraia katika nchi hiyo ndogo ya Afrika Mashariki.

Ripoti ya Human Rights Watch inatokana na mahojiano yaliyofanywa kati ya mwaka 2019 na 2024 ikihusisha watu 30, wakiwemo wafungwa wa zamani, pamoja na nyaraka za mahakama na mahojiano yaliyochapishwa mtandaoni.

Serikali kutochukua hatua kwa tuhuma za mateso magerezani

Wanajeshi wa Rwanda kutoka Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF) na polisi wa Rwanda wakijiandaa kupanda ndege ya "Rwandair" kwa safari ya kijeshi kuelekea Msumbiji katika uwanja wa ndege wa Kanombe, Kigali, Rwanda Julai 10, 2021.Picha: Simon Wohlfahrt/AFP

Ripoti ya shirika hilo imeelezea jinsi ukiukaji mkubwa wa haki za binaadamu ulivyoenea katika magereza mengi nchini Rwanda, ikisema inaamini kwamba afisa mmoja tu mkuu wa magereza likimtaja kwa jina la Innocent Kayumba ndiye aliyewajibishwa.

Mwezi Septemba shirika hilo limeeleza lilijaribu kufanya mawasiliano na serikali ya Rwanda kuhusu matokeo ya utafiti huo, lakini halikufanikiwa kupata majawabu hadi wakati ripoti hiii mpya inachapishwa. Mahojiano na wafungwa wa zamani wa Kwa Gacinya, kizuizi ambacho shirika hilo limekiita "kizuizi kisicho rasmi" chini ya udhibiti wa polisi katika mji mkuu Kigali, yalifichua taarifa za unyanyasaji, maigizo ya kumtoa mtu uhai, vipigo na utesaji ambao ulianzia ambao unalezwa ulianta tangu 2011.

Ushuhuda wa madai ya yanayofanyika magerezani

Katika mahojiano yake aliyofanyiwa mwaka 2020, mmoja kati ya wapinzani nchini humo, Venant Abayisenga alisema "Palikuwa mahala pa hofu." Mpinzani huyo alishikiliwa katika kizuizi hicho mwaka 2017. Abayisenga  ambaye alitoweka miezi mitano baada ya mahojiano kutolewa kwenye mtandao wa YouTube  alisema alisikia watu wakinyongwa, na alihojiwa na polisi bila uwepo wa wakili.

Kadhalika katika simulizi yake hiyo anasema aliwahi kuelekezewa mtutu wa bunduki na kutishiwa kwamba angeuawa. "Kuna watu wanauawa Kwa Gacinya, unasikia sauti ya mtu anayeuawa, halafu unasikia mtu anaingia kusafisha chumba."

Human Rights Watch inasema ilizifanyia mapitio nyaraka za mahakama za watu takriban 25 wanaotuhumiwa kwa makosa yanayohusiana na usalama, huku kadhaa wakidai kuwekwa kizuizini kati ya miezi mitano hadi sita. Shirika hilo pia ilikusanya ushahidi kutoka kwa wafungwa wa zamani katika magereza ya Rubavu na Nyarugenge, ambapo kumeelezwa kufanyika mateso mabaya huku mfungwa mmoja wa zamani akiita ni kama hali ya kuzimu.

Soma zaidi: Marekani yatoa tahadhari kwa raia wake kuelekea Rwanda

Shirika hilo la haki za binadamu lilidai kuwa Rwanda "imeshindwa kuchunguza au kushughulikia madai ya mara kwa mara na ya kuaminika ya mateso yaliyotolewa na wafungwa au wafungwa wa zamani tangu 2017.

Chanzo: AFP