1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

HRW: Safisha safisha ya kikabilia Darfur Magharibi

9 Mei 2024

Shirika la Human Rights Watch (HRW) limesema kwamba mashambulizi ya kikosi cha wanamgambo cha RSF katika eneo la El Geneina, mji mkuu wa jimbo la Darfur, magharibi mwa Sudan, yalisababisha vifo vya maelfu ya watu

Waasi wenye silaha wa SLA wakiwa kwenye lori la mizigo kwenye eneo la Shangil Tobaya katika jimbo la Darfur  nchini Sudan, mnamo Desemba 4, 2005
Waasi wenye silaha wa SLA mjini Shangil Tobaya katika jimbo la Darfur nchini SudanPicha: Camera4/Jim/imago images

Ripoti ya HRW ya kurasa 218 kwa jina, '' Wamassalit Hawatarudi Nyumbani': Safisha safisha ya Kikabila na Uhalifu dhidi ya Binadamu El Geneina, Darfur Magharibi, Sudan,'' iliyotolewa Alhamisi, imesema kuwa kikosi cha RSF na washirika wao hasa wanamgambo wa Kiarabu, wanaolijumuisha kundi la wapiganaji wenye silaha la Tamazuj, walilenga vitongoji vya El Geneina vyenye idadi kubwa ya watu wa kabila la Massalit katika msururu wa mashambulizi ya kuanzia Aprili hadi Juni.

Soma pia:Umoja wa Mataifa umeonya kuwa vikosi vya kijeshi vya Sudan vinauzingira mji mkuu wa Darfur magharibi

Mashambulizi na unyanyasaji mwingine ukazuka tena mnamo mwezi Novemba huku washambuliaji hao wakifanya unyanyasaji mwingine mbaya kama vile mateso, ubakaji na uporaji.

Zaidi ya wakimbizi nusu milioni wakimbilia Chad

Ripoti hiyo imeendelea kusema kuwa zaidi ya wakimbizi nusu milioni kutoka Darfur Magharibi wamekimbilia Chad tangu Aprili 2023 na kufikia mwishoni mwa Oktoba 2023, asilimia 75 ya wakimbizi walikuwa ni wa kutoka El Geneina.

Ukatili mkubwa uliofanywa El Geneina unapaswa kuonekana kama ukumbusho 

Mkurugenzi mkuu wa Human Rights Watch, Tirana Hassan, amesema kuwa wakati Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na serikali zinaamkia uwezekano wa kutokea kwa maafa katika eneo la El Fasher, ukatili mkubwa uliofanywaEl Geneina unapaswa kuonekana kama ukumbusho wa ukatili ambao unaweza kutokea iwapo hakutachukuliwa  hatua za pamoja.

Mkurugenzi mkuu wa Human Rights Watch - Tirana HassanPicha: Human Rights Watch

Hassan ameongeza kuwa mataifa, Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa zinapaswa kuchukuwa sasa hatua za kuwalinda raia.

HRW yasema mashambulizi ya RSF ni safisha safisha ya kikabila 

Ripoti hiyo ya HRW pia imesema kuwa kuwalenga watu wa Massalit na jamii nyingine zisizo za Kiarabu kwa kufanya ukatili mkubwa dhidi yao kwa lengo wazi la kuwataka waondoke kabisa katika eneo hilo, kunajumuisha safisha safisha ya kikabila.

Kati ya mwezi Juni mwaka 2023 na Aprili 2024, HRW, iliwahoji zaidi ya watu 220 nchini Chad, Uganda, Kenya, na Sudan Kusini.

Soma pia:Vikosi vya RSF vyawaua wanakijiji 28 na kujeruhi wengine 280

Watafiti pia walipitia na kuchambua zaidi ya picha na video 120 za matukio, picha za setilaiti, na hati zilizotolewa na mashirika ya kibinadamu ili kuthibitisha kutokea kwa matukio hayo ya unyanyasaji mkubwa.

HRW imeendelea kusema kuwa wakati dhuluma hizo zilipokuwa zikifanyika, wanawake na wasichana walibakwa na kufanyiwa aina nyingine za ukatili wa kijinsia huku wafungwa wakiteswa.

Vitendo vya kikatili vilivyofanywa na RSF

Washambuliaji waliharibu miundombinu muhimu ya kiraia, wakilenga vitongoji na maeneo, yaliojumuisha shule, haswa katika maeneo ya jamii za Massalit zilizohamishwa. Washambuliaji hao pia walipora mali kwa kiwango kikubwa, kuchoma, kurusha makombora na kuharibu vitongoji baada ya kuwafurusha wakaazi.

Hassan awataka waliohusika katika mashambulizi kuwajibishwa

Hassan amesema kuwa kutochukuliwa kwa hatua za kimataifa dhidi ya ukatili huo mkubwa, hakuna sababu na ametoa wito kwa serikali kuhakikisha wale wote waliohusika wanawajibishwa ikiwa ni pamoja na kuwawekea vikwazo wahusika na kuimarisha ushirikiano na  Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC.



 

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW